Friday, September 5, 2014

SULUHU: HUYU NDIYE SHIBUDA ORIJINO

Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samia Suluhu.
Na MWANDISHI WETU
WAKATI Mbunge wa Bariadi Magharibi (Chadema), John Shibuda akiwasilisha maoni ya wachache ya Kamati namba 8 ya Bunge Maalum la Katiba linaloendelea na vikao vyake mjini Dodoma Jumatano mchana, Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samia Suluhu alimsifu na kusema kuwa mwakilishi huyo wa wananchi ndiye orijino, ukimuona mwingine ni photokopi.
Shibuda aliyeingia katika ukumbi huo akipingana na msimamo wa chama chake kilichoamua kususia vikao hivyo kwa kushirikiana na vyama vya CUF na NCCR-Mageuzi, alitumia pia nafasi hiyo kuwapiga vijembe viongozi wake, akisema hana matatizo na Chadema, isipokuwa ana ‘bifu’ na mfumo wa utumishi wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
Akifafanua kauli yake hiyo, Shibuda anayefahamika kwa mbwembwe na mikogo ya lugha, alisema yeye ni kama mchezaji wa mpira aliye staa, akiwatolea mfano Cristiano Ronaldo na Lionel Messi, ambao wanaponunuliwa na timu yoyote, huenda kwa ajili ya kuiimarisha na si vinginevyo.

Mbunge wa Bariadi Magharibi (Chadema), John Shibuda.
“Mimi nikihama timu naenda kuboresha timu nyingine, sijanunua chama chochote, nitahama kwa sababu mimi ni staa nitakayehitajika kwa ajili ya kwenda kukiimarisha, mtu kuhama msikiti hakumaanishi kwamba umehama dini,” alisema huku akishangiliwa na wajumbe wengi wa bunge hilo.
Chadema pamoja na vyama hivyo viwili vya upinzani vinavyounda umoja unaoitwa Ukawa, vimesusia kuendelea na vikao vya bunge hilo vinavyojadili Rasimu ya Katiba Mpya kwa maelezo kuwa wajumbe wa CCM wameondoa maudhui ya Tume ya Jaji Joseph Warioba na badala yake, wanaingiza vipengele ambavyo havikuwepo.
Kususa huko kwa Ukawa kumesababisha kuwepo kwa wito kutoka makundi mbalimbali yakitaka warejee bungeni ili kuendelea na majadiliano, hali iliyomfanya Rais Jakaya Kikwete aingilie kati kwa kuzungumza nao, lakini muafaka zaidi unatarajiwa kupatikana katika kikao kitakachokaa Jumatatu ijayo.
Kitendo cha Shibuda kuhudhuria kikao hicho, kinatarajiwa kuchukuliwa hatua kali na viongozi wa chama chake, hasa kutokana na historia yake ya kusigana mara kwa mara katika masuala mbalimbali ya chama hicho.GPL (P.T)

No comments: