Na Benedict Liwenga, Maelezo-DSM.
Kiongozi wa Chama cha
Kisoshalisti kilichojulikana kama “NAZI” Adolf Hitler (1889-1945)
alikuwa mmoja kati ya Madikteta dhalimu na mwenye nguvu kuwahi kutokea
katika karne ya 20.
Baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya
Dunia mbabe huyo aliamkakwa nguvu kupitia Chama hiko cha Wafanyakazi wa
Ujerumani na kuchukua udhibiti wa Serikali ya Ujerumani mnamo mwaka
1933.
Hitler aliamuru uanzishwaji wa
kambi za mateso dhidi ya Wayahudi na makundi ya watu wengine huku
akiamini kuwa kufanya hivyo ilikuwa
chachu na tishio tosha dhidi ya ukuu wa himaya ya Aryani na hatimaye
kusababisha vifo vya zaidi ya Wayahudi wapatao milioni Sita.
Mashambulizi ya Ujerumani dhidi
ya nchi ya Poland mwaka 1939 ndiyo yaliyoanzisha Vita Kuu ya Pili ya
Dunia ambapo mpaka kufikia mwaka 1941Ujerumani iliteka sehemu kubwa ya
ardhi ya Ulaya na Afrika Kaskazini.
Ili kuepuka kukamatwa kwa
kukwepa utumishi katika jeshi la Austria-Hungary, Adolf Hitler aliondoka
toka Vienna na kuelekea Munich mnamo Mei 1913 lakini baadaye
alilazimika kurudi tena.
Taarifa za kihistoria zinasema
kuwa Kiongozi huyo wa Nazi alijiunga na jeshi la Bavaria na kuanza
kufanya kazi za kujitolea ambapo mwaka uliofuata alishiriki kikamilifu
katika vita ya Kwanza ya Dunia akiwa mstari wa mbele upande wa Magharibi
ambapo uzoefu wake katika vita na mapambano uliathiri mawazo, fikra na
mitazamo yake yote baada ya hapo.
Baada ya Vita Kuu ya kwanza ya
Dunia, Hitler alichukua udhibiti wa chama hiko cha wafanyakazi wa
Ujerumani kama kiongozi hivyo alitumaini kingemwezesha kushika dola ya
Ujerumani punde si punde.
Aliposhindwa kwenye jaribio la
Mapinduzi la mwaka 1923 yeye na wenzake walikamatwa na kufungwa jela na
baada ya kutoka jela alijitahidi kukijenga chama hiko na kuanza mikakati
ya kukamata dola kwa njia zilizo halali.
Hitler alikusudia kufanya
mageuzi na kuendesha sera za kibaguzi ambazo zingetoa nafasi ya kutosha
kwa Wajerumani kuweza kuishi katika himaya kubwa duniani.
Kwanza alitabiri ingekuwa rahisi
kuiteka Czechoslovakia, na kufuatiwa na Ufaransa ambayo ilikuwa
kizingiti kigumu kwa wakati huo hatimaye kumalizia na nchi ya Uingereza.
Kwa mujibu wa mikakati ya Adolf
Hitler, vita ya Tatu ingefuata juu ya uvamizi dhidi ya Jumuiya ya
Kisovieti ambayo kwake ulikuwa ni mtihani ambao alipanga afaulu kwa
kufikiri vita ingepiganwa kwa haraka na kwa urahisi.
Kwa mujibu wa fikra zake za
kuipiga Urusi, hii ingempa utajiri wa malighafi za kutosha hususan
mafuta ambayo yangemwezesha kuandaa mkakati wa maandalizi ya vita ya Nne
dhidi ya Marekani.
Vita hiyo ingekuwa rahisi tu
kwake endapo Ujerumani ingeweza kuwa na ndege ziwezazo kusafiri masafa
marefu pamoja na meli za kivita na kwa upande mwingine ndege za kutosha
na jeshi la maji kubwa na imara lingemwezesha kumkabili adui kokote
aliko bila umbali kuwa kikwazo.
Mara baada ya Hitler kuingia madarakani mwaka 1933, maandalizi
ya Ujerumani kijeshi yalianza kufanyika, hivyo mkazo na mkakati wa muda
mfupi ulikuwa kutengeneza silaha kwa ajili ya vita dhidi ya mataifa ya
Magharibi na mkakati wa muda mrefu ulikuwa juu ya uzalishaji wa silaha
nzito kwa ajili ya vita dhidi ya Marekani.
Mnamo mwaka 1938 Hitler
aliachana na mpango wa uvamizi wa kijeshi dhidi ya Czechoslovakia na
kuangalia zaidi makubaliano ya amani na kiongozi wa nchi hiyo ambayo
yalifanyika mjini Munich na hilo lilikuwa kosa lake baya na kubwa kuwahi
kulifanya.
Alipoamua kuigeukia Ufaransa na
Uingereza Hitler hakuweza kuishawishi Serikali ya Poland kujiunga na
kuwa sehemu ya himaya ya Ujerumani kwa njia za amani ili kuhakikisha
hali ya utulivu inakuwepo katika Mashariki ya Ulaya, hivyo alichukua
maamuzi ya kuivamia na kuiharibu Poland kabla ya kuanza kuzikabili nchi
za Magharibi.
Uvamizi wa nchi ya Poland
ulikususudiwa kufanyika ifikapo Septemba 1, 1939 lakini, ili kufanikisha
adhma yake hiyo na ushindi wa haraka juu ya Poland kwa kuvunja kila
aina ya kikwazo mbele yake, alikusudia kuiingiza Ujerumani katika
makubaliano na Urusi ili mwisho wa siku iwe rahisi kwake kuzivamia nchi
za Magharibi bila pingamizi lolote baada ya Poland.
Hali kadhalika, Hitler
alikusudia kufanya uvamizi dhidi ya Mataifa ya Magharibi katika msimu wa
baridi mwishoni mwa mwaka 1939, lakini hali mbaya ya hewa ilikuwa ni
kikwazo kikubwa ambacho kingeathiri jeshi lake la anga, kwahiyo aliamua
kuhairisha mpango huo na kuhamishia uvamizi huo ifikapo mwanzoni mwa
mwaka 1940 katika majira yajoto.
Kutokana na ushauri alioupata
toka kwa Admiral Erich Raeder juu ya kuivamia na kuiteka Norway ili
kuwezesha upatikanaji wa njia rahisi kwa jeshi lake la maji katika
bahari ya Atlantiki kuelekea Kaskazini, aliivamia Norway mwaka Aprili
1940.
Baada ya kupokea ushauri tena
toka kwa Kamanda Mkuu Erich Von Manstein lengo la uvamizi kuanzia
Kaskazini lilibadilishwa na kuamua kupanga mashambulizi kuelekea nchi
zilizoko Kusini mwa Ulaya kwa lengo la kuzuia misaada ya kijeshi toka
jeshi la Washirika (Allied force) kuelekea nchi za Ubelgiji na Uholanzi.
Mkakati mpya wa Hitler kwa mara
ya kwanza ulionekana kufanya kazi wakati jeshi la Ujerumani
lilipofanikiwa kuvunja mstari wa ulinzi wa jeshi la Kifaransa na
kufanikiwa ndani ya siku kumi kufika kwenye mkondo wa pwani nyuma ya
vikosi vya majeshi ya Muungano.
Baada ya kuonekana wazi kuwa
majeshi ya Washirika yaliyokwama yanaweza kutotoroka kipigo cha jeshi la
Ujerumani, mwelekeo wa silaha na jeshi la Ujerumani ulibadilika tena,
lakini jeshi hilo lilikwisha chelewa kuweza kuzuia na kufanya
mashambulizi dhidi ya askari wa jeshi la Muungano kwasababu kikosi
maalumu cha jeshi la Uingereza na wanajeshi wa Ufaransa walifanikiwa
kuokolewa na kutoroka.
Pigo lililotokea mapema mwa
mwezi Juni 1940 lililopelekea anguko kwa mstari wa mwisho wa ulinzi wa
jeshi la Ufaransa ulikuwa ni ushindi kamili uliompa Hitler furaha na
shangwe huku akijua anapata msaada wa kutosha toka kwa Makamanda na
Majemedali wake wa kivita, ambao kila mara alikuwa akiwapandisha vyeo na
kuwapa namna nyingine za rushwa kama sehemu ya kuwapa motisha ya
kuendelea na mapambano.
Taarifa zinasema kuwa, kwasababu
ilionekana kama vita hii ilikuwa imeisha baada ya Ujerumani kuiteka
Ufaransa, Hitler alianza kupanga mipango mingine kwa ajili ya vita dhidi
ya Marekani na Umoja wa Kisovieti.
Mnamo Julai 11, 1940 Hitler
alitoa amri kuanza kwa ujenzi wa jeshi la maji ikiwemo ujenzi wa meli za
kivita na ilipofika Julai 31, 1940 baada ya mkakati wa kutaka kuvamia
Umoja wa Kisovieti katika msimu wa baridi wa 1940, Hitler kutokana na
ushauri wa wafanyakazi wake wa kijeshi aliamua kuishambulia Urusi katika
majira ya joto mwishoni mwa mwaka1941.
Wakati Uingereza ikikataa
kukubali kushindwa na kusalimu amri, Hitler alipanga kuchanganya hatua
tatu ambazo zingehakikisha Uingereza inasalimu amri;- Kwanza kabisa,
jeshi la anga la Ujerumani lingefanya uvamizi na kuharibu uwezo wa
Uingereza kujitetea; Pili Uingereza ingevamiwa ardhini iwapo kama
isingejisalimisha, na tatu ushindi ambao ungepatikana dhidi ya Urusi
ungeondoa uwezekano wa Uingereza kupata msaada wowote ule toka Urusi,
hivyo kuangamia zaidi na kumaliza hatari yoyote dhidi ya Japan, ambayo
ingehamasika kusafiri katika bahari ya Pasifiki na kuivamia Marekani
upande wa Magharibi.
Kwa upande mwingine Hitler
alitaka Japan kujiunga katika vita na Uingereza na kuahidi kujiunga na
Japan katika vita dhidi ya Marekani kama Tokyo ingeona umuhimu juu ya
hilo, na hii ingekuwa njia nyingine kwa Ujerumani kupata kuimarisha
jeshi la maji dhidi ya Marekani.
Kampeni dhidi ya eneo la Balkan,
kiongozi huyo mbabe wa enzi hizo (Hitler) alikusudia kupata alicho
amini kuwa ngome ya upande wa Kusini iliyokuwa katika hali tete lakini
hata hivyo aliona operesheni kubwa ya jeshi la anga katika eneo la
Balkani ingekuwa ya gharama ya juu sana kutokana na ugumu wa eneo
lenyewe na hivyo kutokusudia kufanya operesheni kama hiyo tena.
Ikumbukwe kuwa, uvamizi wa Ujerumani dhidi ya Umoja wa
Kisovieti, ulianza tarehe 22 Juni, 1941 ambapo hapo mwanzo uvamizi huo
ulionekana kwenda kama ilivyo pangwa, lakini gafla kila kitu kilianza
kwenda vibaya vipigo vya kwanza ambavyo vilikusudia kuangusha Umoja wa
Kisovieti ndani ya wiki chache havikuleta matokeo yaliyokusudiwa na
hayakuweza kuwa na athari katika nchi hiyo, hivyo baada ya hapo, swali
daima lilikuwa kwa Ujerumani ni sekta ipi nyeti na muhimu ishambuliwe
ili kuidhoofisha Urusi na sekta gani iachwe.
Katika hali hiyo, Hitler
alijikuta mara kwa mara akitofautiana na Majenerali wake walioko mstari
wa mbele katika kuamua mustakabali wa vita na baada ya vita kuonekana
ikiielemea na kuigeukia Ujerumani hali ya kutofautiana kati ya Makamanda
wa Hitler ilizidi kuongezeka.
Wakati jeshi la Ujerumani
likiendelea kurudi nyuma, Hitler alikuwa daima na wasiwasi kuhusu hasara
waliyokuwa wakiendelea kuipata ya watu hali kadhalika ya uharibifu wa
vifaa vyake vya kijeshi kwahiyo baadhi ya Majemadari kama Erwin Rommel
na Walther Model, mara kwa mara walikuwa wanapingana na amri ya Hitler
kwa kurudi nyuma wakati Majenerali wengine walikuwa wakirudishwa
nyumbani kukusanya kiinua mgongo chao cha kila mwezi na kustaafu kwa
kutofautiana na amri za kiongozi wao ingawa wengine walikuwa wakiendelea
na kazi zao.
Hitler alifikiri kwamba
kushindwa kwa Ujerumani katika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia kulitokana na
anguko lililotokea katika ardhi ya nyumbani mbele na kwa hivyo kudhani
kuwa uanzishwaji wa sera za kidikteta na mauaji ya kukusudiwa ya
Wayahudi ulikuwa uhakika wa ushindi wa vita dhidi ya majeshi washirika
na safari hii Hitler alipoona hana jinsi na majeshi washirika
yameshaingia mjini Berlin huku yakiongozwa na Jeshi Jekundu la Urusi,
Hitler alijawa na hofu ya kisasi ambacho Warusi wangetoa dhidi ya
Wajerumani, hivyo aliamua kumuoa mke wake na wote kwa pamoja kuamua
kujiua muda mfupi kabla ya jeshi la Urusi kuwasili.
(Makala imeandaliwa na Benedict Liwenga kwa msaada wa mtandao)
No comments:
Post a Comment