Mkurugenzi
wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw.
Ephraimu Kwesigabo akitoa taarifa ya mfumuko wa bei nchini kwa mwezi
Septemba, 2014 leo jijini Dar es salaam. Kulia ni Meneja wa Takwimu za
Ajira na Bei wa Ofisi hiyo Bi. Ruth Minja.
Mfumuko
wa Bei wa Taifa kwa mwezi Septemba 2014 umepungua hadi kufikia asilimia
6.6 kutoka asilimia 6.7 iliyokuwepo mwezi Agosti kutokana na kupungua
kwa bei ya bidhaa na huduma katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Sensa na
Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Ephraim Kwesigabo
amesema kuwa bidhaa za vyakula zikiwemo mchele, mahindi, ulezi, matunda,
Sukari na vinywaji baridi zimechangia kupungua kwa mfumuko wa bei
nchini.
Bidhaa
nyingine zilizochangia kupungua kwa mfumuko wa bei nchini ni Sare za
shule, Simu za mkononi, runinga na viatu huku akibainisha kuwa Fahirisi
za bei kwa maana ya kipimo kinachotumika kupima mabadiliko ya bei za
bidhaa na huduma zinazotumiwa na kaya nchini zimeongeka na kufikia
149.93 kwa mwezi Septemba 2014 ikilinganishwa na 140.61 za mwezi
Septemba mwaka jana.
Kwa
upande wa mfumuko wa bei unaopimwa kwa kipimo cha mwezi ameeleza kuwa
umeongezeka kwa asilimia 0.4 kwa mwezi Septemba 2014 ikilinganishwa na
asilimia 0.1 za mwezi Agosti kutokana na kuongezeka kwa Fahirisi ya
baadhi ya bidhaa zikiwemo samaki, matunda, mbogamboga, mihogo na
vinywaji baridi, mkaa, mazulia na dawa za Binadamu kuwa na mchango
mkubwa katika ongezeko la fahirisi.
Aidha,
amesema mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula nyumbani na migahawani
umepungua hadi asilimia 8.3 mwezi Septemba 2014 kutoka asilimia 8.5 za
mwezi Agosti 2014 na kuongeza kuwa uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania
katika kununua bidhaa na huduma za jamii kwa mwezi Septemba, 2014
umefikia shilingi 66 na senti 70.
Kwa
upande wa mfumuko wa bei wa Tanzania na baadhi ya nchi za Afrika
Mashariki Bw. Kwesigabo amesema kuwa una mwelekeo unaofanana, Kenya
ukipungua na kufikia asilimia 6.6 kwa mwezi Septemba kutoka 8.34 za
mwezi Agosti huku Uganda ikiwa na mfumuko wa bei wa asilimia 1.4 mwezi
Septemba kutoka asilimia 2.8 za mwezi Agosti.Na. Aron Msigwa-MAELEZO.
No comments:
Post a Comment