Makamu Mwenyekiti wa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi(NEC), pia na Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar Mhe. Hamid
Mahamoud Hamid(kushoto) akitoa ufafanuzi baada kusoma taarifa kuhusu
kuanza kwa shughuli za Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo jijini Dares
Salaam kwenye ukumbi wa mikutano wa NEC.Kulia ni Mkurugenzi wa Uchaguzi
Julias Malaba.
…………………………………………………………..
Na Magreth Kinabo,Maelezo
Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC)
imesema kwamba zoezi la majaribio ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu
la Wapiga Kura linatarajia kuanza rasmi katikati mwa mwezi Novemba
mwaka huu.
Aidha NEC imefafanu kwamba
zoezi hilo, litafanyika kwa kutumia mfumo mpya wa ‘Biometric Voter
Registration’(BVR) katika majimbo matatu ya uchaguzi ambayo ni Kawe
katika Manispaa ya Kinondoni, Kilombero, Halimashauri ya Mji wa
Kilombero na Mlele, Halimashauri ya Mlele, ambapo vituo vya uandikishaji
vimewekwa katika kata zilizomo katika majimbo husika.
Hayo yalisemwa na Makamu
Mwenyekiti wa NEC pia na Jaji Mkuu Mstaafu wa Zanzibar Mhe. Hamid
Mahamoud Hamid,wakati akisoma taarifa kuhusu kuanza kwa shughuli za
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika mkutano na
waandishi wa habari uliofanyika leo jijini Dares Salaam.
“Tume tayari imekwishapokea
baadhi ya vifaa muhimu vya uandikishaji zikiwemo fomu za unadikishaji,
hivyo kinachosubiriwa ni kupokea BVR kits 250 zinazotarajiwa kupokelewa
wakati wowote kuanzia leo. Zoezi la Uandikishaji litakapoanza, vituo
vitafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni,
vyama vya siasa vinaruhusiwa kuweka mawakala wao katika kituo ili
kushuhudia jinsi uandikishaji utakavyokuwa unafanyika,” alisema Hamid.
Makamu Mwenyekiti huyo alisema baada ya zoezi hilo kukamilika zoezi hilo litaanza katika maeneo mengine.
“ Tunatarajia Uboreshaji wa
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utafanyika kwa wakati mmoja katika
mikoa yote nchini isipokuwa mkoa wa Dares Salaam na
Zanzibar.Uandikishaji katika mikao ya Dares Salaam na Zanzibar
utafanyika baada ya uandikishaji katika mikoa yote utakapokamilika.Muda
wa uandikishaji utakuwa ni siku saba katika kila kituo,” alisema.
Aliongeza kwamba uandikishaji
katika mikoa yote umepangwa kufanyika kuanzia mwanzoni mwa mwezi
Januari, mwaka huu hadi katikati ya Februari mwaka huu, wakati katika
mikoa ya Dares Salaam na Zanzibar utafanyika mwishoni mwa mwezi Februari
mwaka huu.
Alisema uandikishaji katika
mikoa yote utafanyika katika awamu nne kwenye kila halimashauri ili
kutoa fursa ya kuhamisha vifaa vya uandikishaji kutoka eneo moja
kwenda eneo lingine.
“Uboreshaji wa Daftari la Kudumu
la Wapiga Kura utahusisha wapiga kura wote wapya na wa zamani. Wapiga
kura wa zamani yaani wale ambao walikuwa wamejiandikisha katika Daftari
la Zamani, watatakiwa kwenda katika vituo vya kujiandikisha vilivyoko
karibu na maeneo wanayoishi ili kuchukuliwa taarifa zao hasa alama za
vidole, picha na saini zao kuiongizwa katika mfumo Biometric Voter
Registration na hatimaye watapewa vitambulisho vipya.” Alisisitiza.
Alisema wapiga kura ambao
watakuwa na kadi zao za kupiga kura za zamani watatakiwa kwenda na kadi
zao katika kituo cha kujiandikisha ili kurahisisha zoezi la kuhamisha
taarifa zao za awali katika mfumo mpya wa BVR.
Aidha alifafanua kwamba kwa
wapiga kura waliopoteza kadi au wale ambao kadi zao zimeharibika
watatakiwa kwenta kituoni ili kujiandikisha na kupewa kadi mpya.
Hamid alisema kwa wapiga kura
wenye vitambulisho vya taifa Dares Salaam na Zanzibar watakuja na kadi
zao ambazo ni taarifa zao zitasomwa na vifaa maalum ili kupunguza muda
utakaotumika katika zoezi hilo, pia watapewa kadi mpya ya mpiga kura.
Alisema kwa wapiga kura
wanaoishi na ulemavu na wale ambao hawajui kusoma na kuandika
wanaruhusiwa kwenda kituoni na mtu mmoja katika familia wanayemuamini
ili kusaidia katika uandikishaji.
“Uboreshaji huu unahusisha pia
kuandikisha wapiga kura wote waliotimiza umri wa miaka 18 au zaidi na
wale ambao ifikapo siku ya upigaji kura ya maoni na uchaguzi mkuu wa
mwaka 2015 watakuwa wametimiza umri wa miaka 18. Pia wale wote ambao kwa
sababu mbalimbali hawakuwahi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu
la Wapiga Kura katika mazoezi yote uandikishaji yaliyopita,”
alisisitiza.
Hivyo jumla ya watu wenye umri wa miaka 18 na zaidi wapatao milioni 23.09 wanatarajiwa kujiandikisha.
Hamid aliongeza kwamba mpiga
kura atakayejiandikisha katika daftari hilo la sasa pekee na kupewa kadi
ndiye atakayeruhusiwa kupiga kura.
“Wakati wa uandikishaji,
kipaumbele kitatolewa kwa watu wanaoishi na ulemavu, wazee, wagonjwa
wakinamama wajawazito na wenye watoto wachanga. Hivyo hawatalazimika
kusimama kwenye mstari.
Naye Mkurugenzi wa Uchaguzi
kutoka NEC, Julias Malaba alisema tayari kiasi cha fedha cha Sh.
bilioni 15 zimeshatolewa kwa ajili ya zoezi hilo.Huku Makamu Mwenyekiti
wa NEC akisema bajeti halisi litafafanuliwa baadae.
Kwa upande wake, Sisti Cariah
ambaye ni Mkuu wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na Naibu Katibu NEC,
alisema daftari hilo litakamilika Aprili 14,mwaka huu na litawekwa
wazi kwa muda wa siku tano katika maeneo husika ili kumwezesha kila
mtu aliyejiandikisha aende kukagua na kujiridhisha kwa taarifa zake
zimeandikwa kwa usahihi.
Tume hiyo inatoa wito kwa
wananchi wote wenye sifa za kujiandikisha kujitokeza kwa wingi katika
vituo vyote vya uandikishaji kwa ajili ya kujiandikisha katika daftari
hilo.
Akizungumzia kuhusu mfumo wa BVR alisema unasaidia kupunguza ujiandikisha mara mbili na kuwa na taarifa sahihi.
No comments:
Post a Comment