Saturday, November 29, 2014

MAAZIMIO YA BUNGE KUHUSU HOJA YA TAARIFA MAALUM YA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI KUHUSU TAARIFA YA UKAGUZI MAALUM KUHUSIANA NA MIAMALA ILIYOFANYIKA KATIKA AKAUNTI YA ‘ESCROW’ YA TEGETAPAMOJA NA UMILIKI WA KAMPUNI YA IPTL
1. KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali Kuhusu Ukaguzi Maalum wa Malipo yaliyofanyika katika Akaunti ya Escrow ya Tegeta uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (‘CAG’) pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (‘TAKUKURU’) imeonesha kwamba kwamba Harbinder Singh Sethi, James Rugemalira (VIP), Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Waziri wa Nishati na Madini, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (‘TANESCO’) walihusika kwa namna moja au nyingine katika kufanikisha kufanyika miamala haramu ya fedha za Akaunti ya Escrow ya Tegeta kwenda kwa makampuni ya Pan African Power Solutions Ltd. (‘PAP’), na VIP Engineering & Marketing (‘VIP’)

KWA KUWA, kwa sababu ya kuhusika kwa watu hao na miamala iliyofanyika kwenye Akaunti ya Escrow imeliingizia Taifa hasara ya mabilioni ya fedha za umma zinazotokana na kutokulipwa kwa kodi mbali mbali za Serikali na kushindwa kwa TANESCO kukokotoa upya kiwango cha malipo ya gharama za uwekezaji (‘capacity charges’) wa IPTL;
KWA KUWA, mabilioni ya fedha yaliyotolewa kwenye Akaunti ya Escrow yametumika kuwapa kile kinachoonekana kuwa ni rushwa baadhi ya viongozi na maafisa wa serikali kama vile Mawaziri, Majaji, Wabunge, Wenyeviti wa Kamati za Bunge, wakuu wa taasisi za umma, viongozi wa dini, mawakili wa kujitegemea na watu binafsi.
NA KWA KUWA, vitendo vilivyofanywa na watu hawa vinaashiria makosa mbali mbali ya jinai kama vile uzembe, wizi, ubadhirifu, kutakatisha fedha haramu, matumizi mabaya ya madaraka, rushwa na kupokea mali ya wizi;
HIVYO BASI, BUNGE LINAAZIMIA KWAMBA, TAKUKURU, Jeshi la Polisi na vyombo vingine husika vya ulinzi na usalama viwachukulie hatua stahiki za kisheria, kwa mujibu wa sheria za nchi yetu, watu wote waliotajwa na Taarifa Maalum ya Kamati kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na miamala ya Akaunti ya Escrow, na watu wengine watakaogundulika kuhusika katika vitendo hivyo vya jinai kufuatia uchunguzi mbali mbali unaoendelea;
2. KWA KUWA, vitendo vya kijinai wanavyhohusishwa navyo viongozi wa umma na maafisa wa ngazi za juu serikalini vinakiuka pia maadili ya viongozi wa umma na kuwanyima viongozi na maafisa hao uhalali wa kuendelea kushikilia nafasi za mamlaka katika uongozi wa umma;
HIVYO BASI, BUNGE LINAAZIMIA KWAMBA, Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO wawajibishwe, kwa kuishauri mamlaka yao ya uteuzi kutengua uteuzi wao;
3. KWA KUWA, katika watu walioshiriki kwa namna moja au nyingine katika kashfa ya miamala ya Akaunti ya Escrow wapo pia viongozi wa Kamati za Kudumu za Bunge kama vile Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TANESCO;
NA KWA KUWA, Bunge na/au Kamati zake za Kudumu zina uwezo na mamlaka, kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge, ya kuwawajibisha viongozi hawa wa Kamati kwa kuwavua nyadhifa zao;
HIVYO BASI, BUNGE LINAAZIMIA KWAMBA, Kamati husika za Kudumu za Bunge zichukue hatua za haraka, na kwa vyovyote vile kabla ya Mkutano wa Kumi na Nane wa Bunge, kuwavua nyadhifa zao Wenyeviti tajwa wa Kamati husika za Kudumu za Bunge;
4. KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati imeonesha kwamba katika watu waliotajwa kuhusika kwa namna moja au nyingine katika kashfa ya miamala ya Akaunti ya Escrow wapo pia Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania;
KWA KUWA, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 (‘Katiba’) imeweka utaratibu mahsusi wa kushughulikia nidhamu ya Majaji;
KWA KUWA, utaratibu wa kushughulikia nidhamu ya Majaji kwa mujibu wa Katiba unamtaka Rais kuunda Tume ya Uchunguzi ya Kijaji kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya Majaji;
NA KWA KUWA, utaratibu wa kushughulikia nidhamu ya Majaji kwa mujibu wa Katiba unamruhusu Rais kumsimamisha kazi Jaji au Majaji husika wakati uchunguzi wa tuhuma dhidi yake unaendelea;
HIVYO BASI, BUNGE LINAAZIMIA KWAMBA, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aunde Tume ya Kijaji ya Uchunguzi kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Eudes Ruhangisa wa Mahakama Kuu ya Tanzania;
5. KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati imeonesha kwamba Stanbic Bank (Tanzania) Ltd. ilishiriki kupokea na kutakatisha fedha zilizotolewa kwa njia haramu kutoka katika Akaunti ya Escrow na kupelekwa katika akaunti zilizofunguliwa na PAP katika benki hiyo;
KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati imeonesha kwamba akaunti za PAP katika Stanbic Bank Tanzania Ltd. zimekwishafungwa baada ya fedha zote zilizotolewa katika Akaunti ya Escrow kumalizika na Akaunti ya ya VIP katika Mkombozi Commercial Bank imebakiza kiasi fulani cha fedha;
NA KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati inaonesha kwamba kuna uwezekano fedha zilizotolewa kutoka kwenye akaunti za PAP na VIP zilipelekwa katika benki nyingine;
NA KWA KUWA, vitendo vya Stanbic Bank (Tanzania) Ltd., na benki nyingine kupokea na kutakatisha fedha zilizotolewa kwenye Akaunti ya Escrow ni vitendo vya jinai kwa mujibu wa Sheria ya Udhibiti wa Fedha Haramu;
HIVYO BASI, BUNGE LINAAZIMIA KWAMBA, mamlaka husika za kifedha na za kiuchunguzi ziitaje Stanbic Bank (Tanzania) Ltd. na benki nyingine yoyote itakayogundulika, kufuatia uchunguzi wa mamlaka za kiuchunguzi, kujihusisha na utakatishaji wa fedha zilizotolewa katika Akaunti ya Escrow, kuwa ni taasisi zenye shaka ya utakatishaji wa fedha haramu (institutions of money laundering concern);
6. KWA KUWA, vitendo vya wizi, ubadhirifu wa mali ya umma, hujuma ya uchumi na ufisadi vimeongezeka, kushamiri na kushirikisha viongozi wa kisiasa na maafisa wa serikali pamoja na wafanya biashara wakubwa;
KWA KUWA, kwa mujibu wa sheria iliyoiunda, TAKUKURU inashughulikia vitendo vya aina zote za rushwa zikiwemo rushwa ndogo ndogo (petty corruption) na rushwa kubwa na ufisadi (grand corruption) na matumizi mabaya ya madaraka;
NA KWA KUWA, kwa sababu ya majukumu yake mapana kisheria, TAKUKURU inaelekea kuelemewa katika vita ya kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa letu kiuchumi, kijamii na kisiasa;
HIVYO BASI, BUNGE LINAAZIMIA KWAMBA, Serikali iandae na kuwasilisha Muswada wa marekebisho ya Sheria iliyoiunda TAKUKURU kwa lengo la kuanzisha taasisi mahsusi itakayoshughulikia, kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa, ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa;
7. KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati imeonesha jinsi ambavyo TANESCO imekuwa ikitumia mabilioni ya fedha kulipa gharama za umeme unaozalishwa na IPTL na hivyo kuathiri hali ya kifedha ya Shirika hilo;
KWA KUWA, Taarifa Maalum ya Kamati inaonesha kwamba TANESCO itaendelea kulipa fedha nyingi kwa ajili ya gharama za umeme huo wa IPTL;
HIVYO BASI, Bunge linaazimia kwamba Serikali iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na kuimilikisha kwa TANESCO kwa lengo la kuokoa fedha za Shirika hilo.
8. KWA KUWA, kwa miaka mingi mikataba mibovu ya kuzalisha umeme kati ya TANESCO na makampuni binafsi ya kufua umeme imeisababishia TANESCO hasara ya mabilioni ya fedha na hivyo kutishia uhai wake wa kifedha;
KWA KUWA, Bunge lilikwishaazimia kwamba serikali iwasilishe mikataba husika Bungeni au kwenye Kamati zake kwa lengo la kuliwezesha Bunge kutekeleza vyema wajibu wake wa kuisimamia na kuishauri serikali;
NA KWA KUWA, Serikali haijatekeleza Azimio hilo la Bunge hadi sasa;
HIVYO BASI, Bunge linaazimia kwamba Serikali itekeleze Azimio husika la Bunge mapema iwezekanavyo na kwa vyovyote vile kabla ya kumalizika kwa Mkutano wa Bunge la Bajeti Serikali iwasilishe taarifa ya utekelezaji wa mapitio ya mikataba ya umeme.
Imewasilishwa leo hii tarehe 28 Novemba, 2014.
------------------------------------------------------
ZITTO ZUBERI KABWE (MB)
MWENYEKITI
KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI
Post a Comment