Thursday, December 18, 2014

Baada Ya Werema, Kwanini Kichwa Cha Muhongo Kibiringike Kwenye Vumbi?


Ndugu zangu,

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema ameshajiuzuru. Ni hekima na busara kwa Jaji Werema kuchukua uamuzi huo. Maana, alikiri hata ndani ya Bunge, kuwa ni kweli kuwa alitoa ushauri wa kuidhinisha fedha kutolewa. Hata kama ni kwa kuchelewa, bado ni uungwana, kwa Jaji Werema kuwajibika kwa ushauri aliutoa na hata kuleta mtafaruku wa kisiasa na kijamii katika nchi.
Hata hivyo, kuna hamu, miongoni mwa wanajamii, kuwa na kichwa cha Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo, nacho kibiringike kwenye vumbi. Hamu hii inaonekana kupandikizwa pia kwenye jamii ili kutimiza malengo ya wachache wenye kutaka Muhongo ang'oke kwa sababu zao, ama za kisiasa au kiuchumi.

Maana, mtu mzima ukiisoma ripoti ya CAG na kisha PAC, na kisha ukiliangalia jambo hili kwa macho maangavu, na kwa kuyatafakari mazingira , fursa na changamoto tulizonazo, kama taifa, kwenye sekta ya madini na nishati, na kwa kuangalia mwenendo wa harakati za mataifa makubwa kwenye kupigania rasilimali muhimu kama gesi na mafuta, huoni mantiki ya Tanzania yetu, pamoja na mapungufu ya kibinadamu aliyonayo Profesa Muhongo, kufanya maamuzi ya kujitia hasara kama taifa, kwa kumtoa kafara mmoja wa Watanzania wachache wenye weledi wa kupigiwa mfano kimataifa kwenye sekta ya madini kwa kuegemea mapendekezo ya ripoti ya PAC iliyoandaliwa na wanadamu wenye utashi wenye kutofautiana na iliyothibitika, kuwa nayo ina mapungufu. Na tuwe na ujasiri, kwa maslahi ya taifa, kuyapa mgongo hata yale ambayo, kwa matashi yetu ya kisiasa hata kijamii, tungependa yawe ili tunufaike au tufurahi tu, basi.

Ningelikuwa miongoni mwa wenye kutaka Profesa Muhongo ang'oke, kama ripoti ya CAG ingeonyesha uhusika wa moja kwa moja wa Profesa Muhongo kwenye sakata la Escrow. Lakini, ripoti ya CAG haionyeshi hivyo. Na katika kufanya maamuzi, lililo muhimu ni kutompendelea mtu au kumuonea. Hivyo, ndio maana ya kutenda HAKI.
Niliouelezea hapo juu, ni mtazamo wangu unaotokana na kusumwa na mapenzi kwa nchi yangu niliyozaliwa, basi.
Maggid Mjengwa,
Iringa.
Post a Comment