Friday, January 2, 2015

TAARIFA YA MWENYEKITI WA TUME YA UCHAGUZI KWA WAANDISHI WA HABARI LEO KUHUSU MAANDALIZI YA UBORESHAJI WA DAFTARI LA WAPIGA KURA

1
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Damian Lubuva akizunguza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya tume ya uchaguzi jijini Dar es salaam wakati alipozungumzia maandalizi ya uboreshaji wa daftari la wapiga kura, kura ya maoni ya Katiba mpya na uchaguzi mkuu mwezi oktoba mwaka huu, kulia ni Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Bw. Julius Mh.Julius Mallaba.
2
Baadhi ya waadishi wa  habari wakiwa katika kutano huo.
…………………………………………………………………………………………………..
Ndugu Waandishi wa Habari,
Mkurugenzi wa Uchaguzi,
Watendaji wa Tume,
Mabibi na Mabwana.
Kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, napenda kuchukua fursa hii kuwakaribisheni kwa mara nyingine katika Mkutano huu. Nawashukuru kwamba, pamoja na majukumu mengi mliyo nayo, mmeweza kuupa umuhimu wa pekee mkutano wetu huu na kuhudhuria kwa wingi. Kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, nasema Ahsanteni na Karibuni sana.
Katika mkutano huu, Tume inalenga kutoa taarifa kuhusu tathmini ya utekelezaji wa zoezi la majaribio ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura (Pilot Registration) kwa mfumo wa Biometric Voters Registration (BVR) zoezi ambalo lilikamilika wiki iliyopita.
Ndugu Wanahabari,
Tume ya Taifa ya Uchaguzi, imepewa jukumu la kisheria Kuandikisha Wapiga Kura katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kuliboresha Daftari hilo kwa ajili ya Uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge na Madiwani. Kwa mujibu wa Sheria ya Kura ya Maoni, Daftari hili la Kudumu pia litatumika katika Kura ya Maoni kuhusu Katiba Inayopendekezwa.
Ndugu Wanahabari; mtakumbuka kuwa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imekuwa katika mchakato wa Maandalizi ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa kutumia Teknolojia Mpya ya ”Biometric Voter Registration” (BVR) na mara kwa mara imekuwa ikiomba kukutana nanyi ili kuwapa taarifa kuhusu hatua mbalimbali ambazo Tume imekuwa ikizipitia.
Kwa kuwa Uboreshaji huu ulihusisha matumizi ya vifaa vya teknolojia ya kisasa, vifaa ambavyo vilikuwa havijawahi kutumika katika Uboreshaji nchini, tuliona si vyema kuagiza vifaa vingi kabla ya kuvifanyia majaribio. Zoezi la majaribio lilifanyika ili kuwa na uhakika kuwa vifaa hivi vya Biometric Registration vina uwezo wa kuandikisha Wapiga Kura katika mazingira ya nchi yetu. Zoezi hili liliangalia uwezo wa watendaji kutumia BVR katika uandikishaji na pia uwezo wa vyombo vyenyewe katika Software na Hardware kwenye uandikishaji. Katika zoezi hili tuliangalia changamoto zilizojitokeza ili kuzipatia ufumbuzi kabla ya kuanza Zoezi halisi la Uandikishaji wa nchi nzima.
Ndugu Wanahabari,
Kama nilivyosema, Tume inakutana nanyi ili kuwapa taarifa kuhusu Tathmini ya Utekelezaji wa zoezi la Majaribio la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililofanyika kwa siku saba (7) katika Kata za Bunju na Mbweni katika Jimbo la Kawe, Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es salaam; Kata za Ifakara, Kakingiuka, Ipangala, Mlabani na Viwanja Sitini katika Jimbo la Kilombero Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro; na Kata za Ikuba, Usevya na Kibaoni katika Jimbo la Katavi, Halmashauri ya Wilaya ya Mlele mkoani Katavi.
Tume kwa namna ya pekee, inawashukuru sana Waandishi wa Habari kwa kujitokeza na kufuatilia zoezi hili la majaribio ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Waandishi wa Habari wamesaidia sana katika kuhamasisha Wananchi wa Majimbo husika kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Vilevile, Waandishi wa Habari wamesidia katika kutoa taarifa za maendeleo ya zoezi hili kitu ambacho kimesaidia kufanikisha zoezi hili.
Jumla ya BVR Kits 250 zilitumika katika Uboreshaji huo kwa mgawanyo ufuatao:- Halmashauri ya Kilombero BVR Kits 80, Halmashauri ya Wilaya ya Mlele BVR Kits 80 na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni BVR Kits 90. Vituo katika Kata zote vilikuwa vinafunguliwa saa 2.00 asubuhi na kufungwa saa 12.00 jioni.

No comments: