Waziri wa
Uchukuzi, Dk Harisson Mwakyembe amesema watamaliza kipindi chao utawala
wa awamu ya nne kwa kuimarisha usafiri wa Reli ya Kati uliokuwa
'umekufa' kwa muda mrefu.
Dk
Mwakyembe aliyasema hayo Dar es Salaam juzi usiku katika Kipindi cha
Dakika 45 kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha ITV.
Alisema
licha ya sekta ya reli kukabiliwa na changamoto mbalimbali, wizara yake
imeendelea kuboresha sekta hiyo, ikiwamo kuchukua hatua za kinidhamu kwa
watumishi wanaohujumu fedha za umma.
Dk
Mwakyembe alisema tangu Serikali imtimue mwekezaji njia ya Reli ya Kati,
ambayo ni Kampuni ya India ya Rites, mwelekeo uliopo ni kuhakikisha
usafirishaji unaongezeka kwa tani za mizigo na abiria njia zote za reli
nchini.
"Kabla ya
mwekezaji tulikuwa na uwezo wa kubeba tani milioni 1.5 na tulikuwa
tunafikiria kwenda hadi tani milioni 5, lakini mwekezaji huyo alipoingia
uzalishaji ukaanza kushuka tani 900,000 mara 500,000," alisema.
"Kinachosikitisha
zaidi, mpaka tulifikia usafirishaji wa tani 190,000 kwa mwaka, tukaona
hapana wacha atupishe ili tuanzishe harakati zetu wenyewe."
Dk Mwakyembe aliwaonya watumishi wabadhirifu, akisema hawatakuwa na nafasi ya kuendelea na ubadhirifu wao.
"Kwa
mfano, udhaifu uliojitokeza kwenye ununuzi mabehewa, nasubiri uchunguzi
wa kamati, hatuwezi kuwatuma watu kazi, halafu wanakwenda kupima suti
India," alisema.
Kuhusu
viwanja vya ndege, alisema kwa sasa wizara yake iko kwenye mpango wa
kukarabati viwanja vikubwa vya ndege mikoani kabla ya kununua ndege za
Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment