Monday, February 23, 2015

CUF yahofiwa kukwamisha uchimbaji Gesi na mafuta Zanzibar

seif-sharif-hamad66_a03ab.jpg
WAKATI Wazanzibari wakisubiri mchakato wa kupiga kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa kuruhusu kuanza uchimbaji mafuta na gesi, baadhi ya viongozi wakuu serikalili wameshutumiwa kupinga na kuhamasisha wafuasi kususa mchakato.

Makamu wa Kwanza wa Rais, Seif Sharif Hamad ametajwa kuhusika na matamshi ambayo yanayoweza kukwamisha visiwa hivyo kuchimba nishati hiyo.
Ametajwa kutotabirika kimisimamo kutokana na kutoa kauli zinazokinzana anapokuwa chini ya wadhifa wake serikalini wa makamu wa kwanza wa Rais na pale anapokuwa kwenye chama.
Imeelezwa kwamba, hivi karibuni akiwa nchini Qatar ambako alikutana na viongozi, wafanyabiashara na wawekezaji, aliwataka waje kuwekeza akisema mazingira yameimarika kutokana na amani na utulivu.

Aidha, alisema Zanzibar iko katika hatua za mwisho za kukaribisha kampuni mbali mbali za nje kuwekeza katika mafuta na gesi; hatua inayosubiri kukamilika kwa mchakato wa kura ya maoni ya katiba itakayoruhusu Zanzibar kuchimba mafuta.

Seif alitoa kauli hizo katika nyakati tofauti wakati alipokutana na Waziri wa Nishati na Viwanda wa Qatar, Dk Mohamed Saleh Al-Sada.
Hata hivyo, katika kile kilichoelezwa ni kubadilika ndani ya chama, katika hotuba yake mwishoni mwa wiki wakati akizindua kamati za uchaguzi wa chama chake, aliwataka Wazanzibari kususa mchakato wa kura ya maoni.

Alisema Zanzibar haiwezi kupata maendeleo ya kweli kwa mfumo wa serikali mbili uliopo sasa ambao ulipitishwa katika Katiba Inayopendekezwa. “Mimi napinga Muungano wa Serikali mbili”, alisema Seif.
Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Vuai Ali Vuai akizungumza na waandishi wa habari, alisema chama hakishangazwi na kauli alizoita za ‘ukigeugeu’ za kiongozi huyo wa CUF.

Vuai alisema mwaka 2010 wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka CCM na CUF kwa pamoja walikubaliana na kufikia azimio la kutaka kuona mafuta na gesi yanaondolewa katika orodha ya mambo ya muungano.

Alisema la kushangaza ni kuona kwamba, fursa waliyokuwa wanaitaka sasa imekuja ambayo itatoa nafasi ya Zanzibar kuchimba mafuta na gesi lakini sasa wanapinga na kukataa moja kwa moja.
Alimtaja Seif kwamba, yupo kuona kwamba kwa njia yoyote anaingia madarakani bila ya kujali maslahi ya Wazanzibari walio wengi.

“Mimi sishangazwi na kauli za Maalim Seif kwani akiwa Qatar alisema jambo jingine huku akihamasisha wawekezaji, lakini alipozungumza na wanachama wake ametoa kauli nyingine kabisa ya kutaka wafuasi wake na Wazanzibari kwa ujumla kususa mchakato huo,” alisema Vuai.
Akifafanua zaidi, alisema Seif hataki kuona Muungano wa Tanganyika na Zanzibar udumu na kwamba ndiyo sababu anatoa visingizio kwamba wananchi wanauchukia.

Alitoa mfano kwamba, ajira nyingi za vijana zinazotoka Tanzania Bara ambapo vijana kutoka Zanzibar wamenufaika na ajira Idara ya Uhamiaji na pia walimu wengi wamepata fursa kufanya kazi bara.
Vuai alisema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haina uwezo wa kuwapatia vijana wengi kwa wakati mmoja ajira . Alihimiza vijana kutokubali kurubuniwa na kusikiliza kauli za upotoshaji zinazotolewa na Maalim Seif.
CHANZO:HABARI LEO
Post a Comment