Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini, Dk Edward Hosea.
Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imekiri kuwapo kwa baadhi ya
watumishi wake wanaojihusisha na vitendo vya kupokea rushwa, hivyo
kuchafua sifa ya taasisi hiyo.
Akizungumza
na waandishi wa habari mjini Kigoma jana, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru,
Dk Edward Hoseah alisema tuhuma zilizotolewa hivi karibuni na taasisi
zilizofanya utafiti juu ya masuala ya rushwa nchini, baadhi yake zina
ukweli.
Dk Hoseah
alisema wanapokea utafiti huo kama changamoto na watatumia sheria,
kanuni na taratibu kuwapa adhabu watumishi watakaobainika kujihusisha na
vitendo vya rushwa.
"Takukuru
siyo malaika, iwapo nitasema hakuna kabisa rushwa ndani ya taasisi hii
nitakuwa ninajidanganya kwani hili tatizo lipo sehemu zote, inawezekana
maofisa wasio waadilifu wanapokea rushwa lakini ninawahakikishia kwamba
tutachukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayebainika," alisema Dk Hoseah
na kuongeza:
"Serikali
imefanya jitihada kubwa kuhakikisha Takukuru inaboreshwa, ndiyo maana
bado sielewi kwanini kuna baadhi ya watumishi wanalalamikiwa kujihusisha
na ulaji rushwa, wanalipwa vizuri na kuna mazingira mazuri ya kufanya
kazi. Nitafanya jitihada kuondoa changamoto hizi."
Pia,
alitoa tahadhari kwa wananchi kuwa makini na matapeli wanaojitangaza
kwamba wao ni maofisa wa Takukuru, hivyo kuomba rushwa kwa baadhi ya
maofisa wa Serikali na watu wengine ambao wanabainika kufanya makosa
yanayohusiana na ubadhirifu mbalimbali.
Dk Hoseah
alisema ili kupambana na rushwa lazima Serikali iwe na uongozi bora na
imara, ambao utasaidia kuweka mipango thabiti kwa maendeleo ya wananchi,
kufanya mambo kwa uwazi, kuwajibika kwa umma, kuwashirikisha watu
katika mipango mbalimbali na kusimamia utawala wa kisheria.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment