Wednesday, February 18, 2015

KIZAAZAA SINZA MAKABURIN


Timbwili lililotokea juzi, ndiyo lile hasa linaloitwa nguo kuchanika. Maana zilianza ngumi za pande tatu. Maana ikawa hata haieleweki nani anamtandika nani, na kutokana na mkasa mzima, sisi wananchi wema ililazimika tukae pembeni tumekodoa macho, huku hatuelewi kitu gani tufanye. Sababu ya timbwili hili mimi kama raia mwema nasema lilianzishwa na ubovu wa barabara, najua wengine mtakuja kusema barabara haihusiki lakini ki ukweli barabara ingekuwa nzuri kusingekuwa na tatizo lililotokea.
Katika kukwepa mashimo makubwa kadhaa yaliyokuwa barabarani ghafla gari mbili zenye vioo vyeusi tii wala humuoni mtu ndani zikajikuta zimegongana katikati ya barabara. Magari husika yalikuwa Kivitz kidogodogo kilichokuwa kimeanza kuchoka na Land-Cruiser moja jipya la bei mbaya. Madereva wa gari zote wakafungua milango na kutoka kumbe wote wanawake.
Huyu mama dreva wa Kivitz alionekana kuwa na umri mkubwa kuliko mwenzie na hata nguo zake zilikuwa za staha , alionekana kama vile ni mama mwenye hadhi kidogo anayejiheshimu ambaye ana familia na mambo yake si mabaya. Huyu mwingine mwenye Land Cruiser kubwa kama la waziri, alitoka kwenye gari na kikaptura kidogo ambacho hata mtoto mdogo kingembana, na ndiye aliyeanza kelele akionekana kuwa ni wazi atamlamba makofi Mama Kivitz wakati wowote, ubishi wa kosa la nani ulipamba moto, japo kuwa wote tulijua kosa ni la Kikaptura, ila yeye ndiye aliyekuwa mkali na kudai kagongwa.
Mama Kivitz akanyanyua simu na kumpigia mumewe, "Baba John nina tatizo nimegongwa hapa Sinza naomba uje tafadhali."
Baba John alijibu kwa mkato, "Jamani niko bize katikati ya kikao, hebu lisovu mwenyewe".
Wakati huohuo binti Kikaptura naye si akapiga simu, "Bebi kuna mjinga mmoja kanigonga hapa Sinza, come please."
Haikuchukua muda Bebi akafika pale, hapo ndipo picha likaanza, kumbe Bebi ndiye Baba John, mume halali wa Mama Kivitz!!!!
Kimsingi mwisho wa picha, Baba John akamnyang'anya kikaptura funguo za gari na kumkabidhi mkewe mbele yetu jasho jingi likiwa linamtoka!.CHANZO:.Globalpublishers
Post a Comment