Tuesday, February 24, 2015

WAZIRI MKUU AZINDUA UANDIKISHAJI WAPIGA KURA KITAIFA

images 
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amezindua zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa kutumia mfumo wa Biometric Voter Registration (BVR) na kuwataka viongozi wa siasa wawahimize wanachama wao wajitokeze kwa wingi bila kujali tofauti za kiitikadi.
Ametoa wito huo wakati akizungumza na viongozi mbalimbali na wananchi waliofika kushuhudia uzinduzi huo uliofanyika kwenye kata ya Lumumba, Halmashauri ya Mji wa Makambako, mkoani Njombe.

“Ninawasihi viongozi wa siasa tuwahimize wanachama wetu waende kujiandikisha kwa wingi. Tuache kauli za kukatisha tamaa, tuache kauli za kejeli sababu zoezi hili ni jema na lina nia ya kuwawezesha Watanzania wote kutumia haki yao ya kupiga kura,” alisema.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaomba Watanzania wenye vitambulisho vya uchaguzi vya zamani na wale wasio na vitambulisho wajitokeze kwa wingi kushiriki zoezi hilo.

“Wale waliokwishafikisha miaka 18, na wale ambao watatimiza miaka 18 ifikapo Oktoba, mwaka huu wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwa sababu wasipofanya hivyo hawataweza kupiga kura kama hawatajiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,” aliongeza.
Akiwa uwanjani hapo, Waziri Mkuu alishuhudia uandikishaji wa wakazi watatu wa kata hiyo ambapo zoezi zima lilidumu kati ya dakika tatu na dakika tano. Kisha alikabidhi kadi kwa mpigakura wa kwanza kuandikishwa ambaye alitumia dakika tatu kamili.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema amefurahishwa na taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Damian Lubuva kwamba zoezi la uandikishaji lililoanza jana katika mji wa Makambako lilizidi matarajio ya Tume ya kuandikisha wapigakura 1,850.
“Nimefarijika sana na taarifa ya Mwenyekiti… Mlianza na kata tisa zenye vituo 54 na mlitarajia kuandikisha watu 1,850 lakini badala yake mmepata watu 3,014. Hili limenipa faraja sana. Ninawapongeza sana kwa hatua hiyo,” alisema.
Mapema, akitoa taarifa kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu kufanya uzinduzi huo, Jaji Lubuva alisema ana imani wadau mbalimbali wataendelea kuhamasisha wananchi washiriki zoezi la uboreshaji daftari la wapiga kura.

Alisema uboreshaji wa daftari hilo utafanyika kikanda na kwamba wamepanga kutumia siku saba kwa kila kituo huku akisisitiza kwamba hakuna mtu atakayebakizwa bila kuandikishwa wakati ameshafika kituoni.
Aliwataka watu wanaokwenda kujiandikisha wawe na vitambulisho vyao vya zamani vilivyotolewa na Tume ya taifa ya Uchaguzi kwani tayari vina taarifa zao kwa hiyo vitapunguza muda wa mtu kuandikishwa. “Kadi za Tume (NEC) au za NIDA kwa wale wachache ambao wanazo, wakija nazo zitapunguza muda wa uandikishai sababu zina taarifa kwenye kanzidata,” alisema.

Akitoa ufafanuzi kuhusu mfumo wa uandikishaji wa BVR, Jaji Lubuva alisema mfumo huo siyo sawa na mfumo wa upigaji kura wa kielektroniki (e-voting) kama ambavyo wengi wanadai bali mfumo huo unafanya kazi kwa kutumia alama muhimu za mpigakura.
“Mfumo huu unatumia alama zaidi kwanza ikiwa ni picha na zaidi ni macho ya mhusika, pili ni alama za vidole na tatu ni saini ya mhusika. Mfumo huu unaweza pia kuchukua alama za mtu mwenye ulemavu wa kuona ama ulemavu wa mikono,” alisema.

Alisema uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura ni hatua ya kisheria na kwamba Tume itajitahidi kuhakikisha inafuata hatua zote wakati wa zoezi hilo.
Waziri Mkuu ameondoka Makambako na anaelekea Mbeya kuanza ziara ya kikazi ya siku sita kukagua shughuli za maendeleo katika mkoa huo.

No comments: