WAZIRI wa
Nishati na Madini, George Simbachawene ameomba aombewe afanye vizuri
asipeleke aibu nyumbani, kwa kile alichoeleza wizara anayoongoza ni
ngumu.
Alisema ugumu wake unatokana na wizara hiyo kubeba rasilimali za nchi.
“Niombeeni
kwa Mungu, wizara hii inahusika na rasilimali za nchi, ni wizara nzito,
kazi ni kubwa tunalinda mafuta, madini, gesi na umeme, sioni sababu ya
kujisifu wala kustahili kuliko wengine. Mnisaidie kwenye maombi ili
nifanye vizuri nisilete aibu nyumbani,” alisema.
Simbachawene
ambaye ni Mbunge wa Kibakwe mkoani Dodoma, alitoa kauli hiyo juzi
wakati akizungumza na wananchi wa Mpwapwa na wapiga kura wake,
waliojitokeza kumlaki na kumpongeza kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo.
Alisema
kuteuliwa kushika wadhifa huo ni jambo moja na anahitaji maombi aweze
kutekeleza wajibu, kutokana na wizara hiyo kubadilishwa mawaziri na
manaibu waziri kila mara.
Alisema
kwenye wizara hiyo kuna watu wanaotaka vitalu, kuna watu wanaopora
maeneo na wanaotaka kupora mali za Watanzania, licha ya wao pia kuwa
watanzania.
“Pamoja
na kulinda mali za Watanzania nina wajibu wa kuhakikisha nishati
inapatikana kwa watu wote na sasa serikali iko katika mpango kamambe wa
kusambaza umeme vijijini,” alisema.
Alisema dhamira ya serikali ni kuhakikisha vijiji vyote vinakuwa na umeme kwa lengo la kuwafanya Watanzania kuwa na maisha bora.
Licha ya
kukabidhiwa zawadi mbalimbali wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika
Kibakwe, pia wazee walimkabidhi Sh 100,000 kwa ajili ya kuchukua fomu
kwa ajili ya kugombea tena ubunge jimboni humo.Aidha, viongozi wa dini
walimfanyia maombi.
“Nashukuru kwa mapokezi makubwa na ukarimu mkubwa mliouonesha na nawaahidi sitawaangusha,” alisema.
Awali, kabla ya kufika Kibakwe, waziri huyo alisimamishwa mara kwa mara njiani na wananchi waliokuwa wamebeba mabango.
Katika
vijiji vya Lukole na Kilolo, wananchi walisema wanahitaji umeme kwani
maisha yao yamekuwa magumu kutokana na kutembea umbali mrefu kutafuta
mashine za kusaga.
“…Tunaomba
utusaidie tupate umeme. Sisi akina mama tunatembea umbali mrefu kwenda
kusaga tunaporudi tumechelewa ugomvi moja kwa moja ndani ya nyumba,”
alisikika mama mmoja akilalamika.
Waziri
alimtaka Meneja wa Shirika la Umeme (Tanesco) Mkoa wa Dodoma, Zakayo
Temu kuhakikisha kijiji hicho kinapatiwa transfoma umeme uanze
kusambazwa.
“Nimeshatoa
maagizo na meneja kanihakikishia hadi Juni mwaka huu, zoezi hilo
litakuwa limekamilika,” alisema na kuwataka wananchi kufanya haraka
kufunga nyaya za umeme na taa kwenye nyumba zao.
Pia,
wananchi wa Kijiji cha Kingiti waliziba njia kwa mabango kuomba kupatiwa
zahanati. Aidha, katika Kijiji cha Idunda wananchi hao waliomba
kupatiwa umeme kutokana na kuchoka kutumia koroboi.
Wananchi hao waliahidiwa kupatiwa umeme haraka iwezekanavyo. Aliahidi kutoa mabati kwa ajili ya kuezeka zahanati ya Kingiti.
“Upatikanaji
wa umeme vijijini utaimarisha uchumi, kwani wananchi watakuwa na uwezo
wa kuanzisha viwanda vya usindikaji,” alisema. Alisema licha ya serikali
kutumia fedha nyingi kusambaza umeme vijijini, changamoto kubwa iliyopo
ni wananchi kushindwa kuunganisha umeme unapofika kwenye maeneo yao.
“Tumieni nishati kuboresha maisha yenu, jipangeni ili muweke umeme,
umeme umefika kwenye vijiji vingi lakini watu bado hawaunganishi kwenye
nyumba zao,” alisema.CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment