Monday, July 6, 2015

MRAMBA NA DANIEL YONA WAHUKUMIWA MIAKA 3 KILA MMOJA, GREY MGONJA AACHIWA



Basili Mramba,Daniel Yona,Agrey Mgonja mwingine hakufahamika jina lake wakijadili jambo kabla ya kusomewa hukumu yao hivi karibuni katika mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu.
……………………………………………………………………………………………..
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo imewahukumu kwenda jela miaka mitatu na kulipa faini ya milioni tano aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona huku ikimuachia huru aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja baada ya kumuona hana hatia.
Vigogo hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka mawili ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya shilingi bilioni 11.7

Hukumu hiyo imetolewa chini ya jopo la mahakimu watatu ambao ni Hakimu Saul Kinemela, Jaji Sam Rumanyika na Jaji John Utamwa aliyekuwa mwenyekiti wa jopo hilo baada ya kupitia ushahidi pamoja na vielelezo vilivyowasilishwa na pande zote mbili katika kesi hiyo.
Kwa mara ya kwanza washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo mwaka 2008 wakikabiliwa na mashitaka ya kuisababishia serikali hasara ya kiasi hicho cha fedha kutokana na kutoa msamaha wa kodi kwa Kampuni ya kukagua madini ya dhahabu ya M/S Alex Stewart ya Uingereza.

Katika utetezi wake, Mramba alikiri kuisamehe kodi kampuni hiyo kwa kuwa kulikuwa na mkataba uliosainiwa Juni 2003 kati ya kampuni hiyo na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambao ulikuwa unaonesha malipo yafanyike bila ya kukatwa kodi.

Mgonja alidai kuwa yeye ndiye aliyemshauri Mramba kuisamehe kodi kampuni hiyo kutokana na mkataba huo. Hata hivyo, inadaiwa msamaha wa kodi ulitolewa wakati tayari Wizara ilikuwa imepokea barua za kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambazo zilikuwa zinakataza kampuni hiyo isisamehewe kodi.

No comments: