Mgeni
rasmi Mkuu wa Ofisi na Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Zulmira
Rodrigues (wa pili kushoto) akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja
wa Vilabu vya Waandishi wa Habari (UTPC), Abubakar Karsan mara baada ya
kuwasili kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Nyanza jijini Mwanza
kushiriki maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Amani duniani ambapo
kitaifa yamefanyika jijini Mwanza. Kushoto ni Msajili wa Vyama vya Siasa
nchini, Jaji Francis Mutungi na wa pili kulia ni Afisa Mfawidhi Ofisi
ya Msajili wa vyama vya siasa kanda ya ziwa Mwanza, Bw. Ludovick Ringia.
………………………………………………
Na Modewjiblog team
WAKATI
viongozi wa dini wametakiwa kuacha kufanya siasa na badala yake
wahubiri upendo na si upinde, waandishi wa habari wameelezwa kununuliwa
na wanasiasa kulainisha maneno yao.
Hayo
yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa
Habari (UTPC), Abubakar Karsan wakati akizungumza kwenye kilele cha
maadhimisho Siku ya Amani Duniani iliyofanyika Mwanza.
Alisema
katika mazungumzo yake hayo kukengeuka kwa wanahabari na viongozi wa
dini ambao ni wadau muhimu wa amani hasa kipindi hiki kuelekea uchaguzi
ni kasoro inayotakiwa kufutwa mara moja.
Akikazia
kwa viongozi wa kidini alisema kwamba amani ya nchi inahitaji kulindwa
na wote lakini viongozi wa dini wana wajibu mkubwa katika hilo.
Alisema
kutokana na wadhifa wake amekuwa akipata habari nyingi ambazo
zinakengeuka na zenye mwelekeo hatarishi na nyingi zinakuwa ni za
viongozi wa dini.
“Habari zinapoandikwa Tanzania, inapofika saa saba, saa nane ya usiku,
mimi huletewa habari nyingi sana, kuziangalia na miongoni mwa habari
tulizozizuia ni mbaya kweli kweli zinatoka kwa baadhi ya viongozi wa
madhehebu ya dini.” alisema Karsan
Mkurugenzi
Mtendaji wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari (UTPC), Abubakar
Karsan akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho Siku ya Amani Duniani
iliyofanyika kitaifa jijini Mwanza.
“Sasa nawaomba sana kwa unyenyekevu mkubwa kwa viongozi wa dini nchini,
nawaomba muhubiri upendo na msihubiri upinde!..” alisisitiza Karsan.
Kiongozi
huyo wa UTPC yenye wanachama zaidi ya elfu nne alisema kwamba
anashangaa viongozi hao wa dini kugeuka wanasiasa kwani anaamini kwamba
Kwa Msajili wa Vyama hakuna chama cha dini kilichosajiliwa.
Alisema
pamoja na kwamba hakuna chama cha siasa cha kidini kusajiliwa
anashuhudia anashuhudia baadhi ya viongozi wa dini wakihubiri siasa.
Pamoja
na kuhimiza viongozi wa dini wasitoke katika mstari wao wa kuhubiri
amani, alisema kuna kasoro kubwa miongoni mwa wanahabari kwa kuwa wengi
wao tayari wamenunuliwa.
“Wanahabari
wengi baadhi yao wameshanunuliwa hasa kwa habari zao wanazoandika
nyingi wanawachagulia wananchi kwa habari zao za kununuliwa. Andikeni
habari na sio kuandika hatari.” alisema Karsan.
Na
kuongeza kuwa: “Magazeti yanapiga kura, radio inapiga kura, Televisheni
inapiga kura, tena inapiga kura sasa wakati siku ya kura ni Oktoba 25.
Acheni kabisa michezo hiyo kwani tunawaomba muwe waandishi wa habari na
sio waandishi wa hatari…Andikeni habari na sio hatari!!” alisisitiza
Karsan.
Kwa
kuzingatia miiko ya taaluma ya habari nchini, alipigilia msumari kwa
wamiliki wa vyombo vya habari, wanasiasa kuacha kuwahonga waandishi hasa
kwa kutumia fedha ili kulainisha habari huku wakionekana kuunadi Uhuru
wakati mioyoni mwao hawana utu.
“Nawaomba
wananchi wa Tanzania, msiwachague viongozi wa nchi hii kupitia
magazeti, radio na Televisheni. Puuzeni habari zote nendeni kwenye
mkutano wa wanasiasa na msikilize kila mgombea anasema nini na kila
chama kinasema nini hao wanaoandika kwenye magazeti yao ni yao wenyewe
na mengi hayana ukweli.” Alisema.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari (UTPC), Abubakar
Karsan akisisitiza jambo kwenye maadhimisho ya siku ya kimataifa ya
Amani duniani jijini Mwanza.
UTPC ina zaidi ya waandishi wa habari 4600 nchini kote ambapo makao yake makuu yapo Mkoani Mwanza.
Pia
aliwawaomba wamiliki wa vyombo vya habari nchini kuhakikisha wanawalipa
mishahara waandishi wao kwani hadi sasa baadhi yao wanahabari wanadai
mishahara zaidi ya miezi mitatu.
“Nawaomba
wamiliki wa vyombo vya habari, ili waandishi waweze kufanya vizuri,
basi walipeni mishahara yao. Wapo ambao hadi leo baadhi yao wanawadai
mishahara zaidi ya miezi mitatu” alifafanua Karsan.
Karsan
aliwataka wamiliki hao kuacha kusimama majukwaani na kujinadi mambo
mazuri wakati wanashindwa hata kuwalipa wafanyakazi wao mishahara mizuri
na hapo hapo wanataka waandike habari za haki.
Aidha alikemea tabia ya wamiliki wa vyombo vya habari ya kuwachagulia habari wahariri.
Naye
mwakilishi Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia
Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Zulmira Rodrigues ambaye alikuwa
mgeni rasmi katika hafa hiyo aliwataka watanzania katika umoja wao
kuhakikisha kwamba amani inaendelea kuwapo nchini ikizingatiwa kwamba
taifa hili lilipata uhuru kwa njia ya amani.
Alisema
Tanzania tangu zamani imeweka mbele mazungumzo katika kutatua mambo
mbalimbali na kusema hatua hiyo ya mazungumzo ni hatua kubwa ya
kidekrasia ambayo imefanikisha amani na kusema ni tumaini lake kwamba
itaendelea kuwapo.
Naye
Naibu kamishina wa Polisi Charles Mkumbo ambaye ni kamanda wa polisi wa
mkoa wa Mwanza akizungumza katika hafla hiyo aliwataka wananchi kutii
sheria bila shuruti na kwamba jeshi la polisi limejipanga kuzuia uhalifu
na vitendo vinavyotia hofu kuelekea na siku ya uchaguzi.
Alisema
jeshi lake limejipanga vyema pamoja na kutumia weledi na busara
kuelekea uchaguzi, siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi.
Aliwatahadharisha wananchi umuhimu wa kulinda amani kwani gharama ya kuipoteza na kutaka kuirudisha ni kubwa.
Pichani
ni viongozi mbalimbali wa madhehebu ya dini nchini waliohudhuria
maadhimisho ya siku ya kimataifa ya Amani Duniani ambayo kitaifa
yamefanyika jijini Mwanza.
No comments:
Post a Comment