Saturday, May 20, 2017

CAG mstaafu amsifu Rais Magufuli


ALIYEKUWA Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, ameisifu serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli kwa kufanyia kazi ripoti za ukaguzi zinazofanywa na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu (NAOT).Amesema katika ripoti nyingi za ukaguzi, ilikuwa ikiripotiwa kuwapo kwa watumishi hewa lakini hakuna hatua zilizokuwa zikichukuliwa. Amesema iwapo taarifa hizo zingekuwa zinafanyiwa kazi, kusingekuwa na watumishi hewa.


Utouh ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Wajibu Institute of Public Accountability,  aliyasema haya jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa kuchambua ripoti ya CAG.


“Mara nyingi tulitoa mapendekezo halafu hayatekelezwi na nadhani ndiyo maana tunaona miaka mingi sana kulikuwa na kelele za watumishi hewa, mishahara hewa serikali haikushughulika na maoni yetu.

“Sasa afadhali awamu hii ya tano imeliona tatizo hilo na imeanza kulishughulikia na sasa unaweza kuona ni mabilioni mangapi ya fedha ambayo yameokolewa,”alisema.

Alisema  hata katika ukusanyaji wa kodi, misamaha ya kodi  na deni la taifa hayo yote yana mwingiliano na ukuzaji wa uchumi na maendeleo ya nchi, hivyo mapendekezo yote ya CAG yaangaliwe kwa umakini na kufanyiwa kazi.

“Sisi tunaamini kuwa ripoti za CAG zimekuwa zikiangaliwa juu juu tu lakini kiukweli zina taarifa muhimu sana kwa ajili ya kukuza na kuimarisha uchumi na zaidi katika kuimarisha uwajibikaji na utawala bora nchini,” alisema

Mkutano wa jana uliandaliwa na  taasisi yake kwa kushirikiana na  Foundation for Civil Society kwa ajili ya kuelimisha umma kuhusiana na mapendekezo ya ripoti za CAG ili kuzitumia vizuri katika kujenga uwajibikaji na utawala bora Zaidi.

Utouh alisema kwenye uchambuzi wa ripoti za CAG, matatizo mengi ambayo wameyaona ni utekelezwaji mdogo wa mapendekezo kwa kuwa ripoti ya mwaka 2015/2016 kwa serikali za mitaa, kati ya mapendekezo 79 ni matatu tu yamefanyiwa kazi, sawa na asilimia nne.

“Unapokuwa na utekelezaji mdogo wa mapendekezo ambayo yanalenga kuimarisha yakaachwa, tunaona mambo mengi yanajirudia. Mambo yanazungumzwa na mapendekezo yanatolewa lakini kwa sababu ya utekelezaji mdogo hakuna kinachofanyika,” alisema.

Aidha, alisema kutokutekeleza mapendekezo kwa mujibu wa Katiba, CAG ana jukumu kubwa la kushauri serikali kuhusiana na ujenzi na uimarishaji wa uchumi wa nchi, hivyo yasipotekelezwa serikali inajikuta inapata hasara kubwa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation for Civil Socity, Francis Kiwanga, alisema wamekuwa wakifanya kazi ya kusukuma ajenda ya utawala bora nchini na kwamba wameungana na taasisi ya Wajibu kusaidia kufanyia kazi taarifa za ripoti za CAG kuwa kwenye lugha ambayo inayofahamika kwa kila mwananchi.

Alisema lengo ni kuwawezesha wananchi ambao wako vijijini  kuona  viongozi wetu na kuwauliza maswali ambayo yameibuliwa na mojawapo ya maswali ni kwani ni kumekuwa na utekelezaji mdogo wa mapendekezo yanayotolewa na ripoti ya CAG licha ya kutumia fedha nyingi katika kufanya kazi hiyo.

Naye  Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Nagy Kaboyoka, alishangaa kuona serikali haifanyii kazi mapendekezo ambayo yamekuwa yakitolewa katika taarifa za CAG.

Alisema bajeti ya CAG imekuwa ikipunguzwa kila wakati na kwamba hali hiyo imekuwa ikimfanya ashindwe kutekeleza majukumu yake licha ya kwamba PAC imekuwa ikimtegemea.
Post a Comment