Tuesday, May 9, 2017

Waziri Mwakyembe kuanza na BMT, TFF

 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amesema tangu achukuwe nafasi ya kuongoza wizara hiyo amegundua mambo yanayorudisha nyuma mchezo wa soka hapa nchini na kuahidi kuanza kuyachukulia hatua kwa kuanzia Baraza la Michezo Tanzania (BMT) na Shirikisho la Soka nchini (TFF).

Mbali na hilo, Mwakyembe amewarushia lawama wanachama kwa kuchagua viongozi wa kuongoza klabu na TFF kwa masilahi binafsi pasipo kuangalia faida ya mchezo husika.

"Unajua wanachama wa klabu na TFF wale wanachagua viongozi wa kuwaongoza ndiyo huvipelekea vyombo hivi kuwa na migogoro mikubwa ambayo haiana manufaa yoyote kwenye soka. Nimeingia na nimegundua madudu mengi, nikiwa kama Waziri ambaye najua sheria nitalishughulikia hilo haraka.

"Hata ukiangalia pale BMT na TFF kote kuna matatizo ya kisheria ambayo yanaharibu kabisa soka, nawatahadhalisha pia wanachama ambao ndiyo wenye kuanzisha hii migogoro kuwa makini katika kuchagua viongozi wao, tunahitaji viongozi bora wa michezo, ukiangalia zaidi hata huu mfumo wa kiongozi wa juu kushika nafasi nyingi za kuongoza si sahihi.

"Nitakachokifanya kabla ya kutoa uamuzi wangu, nitawashirikisha wadau mbalimbali wa michezo ili kuwapata somo na kujadili kwa pamoja huu mfumo ambao unaturidisha nyuma, ukiwa kiongozi hutakiwi kuhodhi madaraka mengi, ama kama uliwahi kuwa kiongozi wa klabu basi kila jambo ama uamuzi yako yataonekana hayako sahihi, tutajuwa cha kufanya hapo hivi karibuni tu," alisema Mwakyembe.

No comments: