Wednesday, July 26, 2017

China kubaini watukanaji WhatsApp, Facebook Bongo

WATU wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii kama WhatsApp na Facebook, huenda wakaanza kubainika kirahisi katika siku za karibuni na kufikishwa mbele ya vyombo vya dola kwa msaada wa China, imeelezwa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Edwin Ngonyani, alisema watu wanaotumia lugha za matusi, kutuma picha zisizokuwa na maadili katika mitandao ya kijamii watabainika kwa urahisi kwa kutumia mfumo wa China.

Ngonyani alisema China imefanikiwa kudhibiti suala hilo kwani kitu kibaya kinapoingizwa nchini mwao kupitia mtandao, hukizuia kabla hakijaleta madhara kwa jamii.

Sheria ya Makosa ya Mtandao ilipitishwa na Bunge Aprili Mosi, 2015 lakini ujio wa sheria hiyo haujaleta matokeo chanya kwa kuwa kumekuwa na matukio ya matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii ikiwemo Instagram pia.

Sheria hiyo ambayo tayari imeshaanza kutekelezwa ilipelekwa bungeni kwa hati ya dharura.

Ngonyani aliyekuwa akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa vyombo vya habari na matumizi ya mtandao uliofanyika jijini Dar es Salaam, alisema kuna idadi kubwa ya wananchi wanaotumia mitandao ya kijamii.

"Lakini baadhi yao huitumia kwa kuwatukana watu na hata kuweka vitu visivyotakiwa kwa maadili ya Kitanzania," alisema.

"Kama mtu amekutumia ujumbe mbaya, tunataka tuwe na uwezo wa kumkamata na kumchukulia hatua.

"Au (mtu) amekutumia barua pepe, au ametuma picha mbaya kwenye WhatsApp, wenzetu China wameweza kuwanasa kwa urahisi.

"Sasa na sisi tunataka kujifunza hilo ili tuanze kuwabaini."

Ngonyani alisema mgeni yoyote anayeingia China hawezi kutumia mtandao wowote wa kijamii isipokuwa wa Kichina, tofauti na hapa nchini ambako mgeni anaweza kutumia mitandao ya nje.

AANDAA MFUMO
Mhandisi Ngonyani alisema serikali inaandaa mfumo huo wa kuwabaini moja kwa moja watumiaji wabaya wa mitandao na kwamba pindi utakapokamilika utapelekwa katika Baraza la Mawaziri; kisha kupelekwa bungeni na kupitishwa kuwa sheria.

"Mfumo huo ukikamilika tutaweza kujua ujumbe huu umetoka kwa nani, kwa sababu kwa sasa hivi mtu anaweza kutumia simu ya mtu mwingine kutuma ujumbe mbaya," alisema zaidi.

"Sasa ni lazima tutafute teknolojia mpya ambayo hata mtu akitumia simu (namba) ya mtu na kuitumia vibaya tunamkamata.

"Kule (ujumbe) ulikotoka lazima ujulikane."

Alisema kwa sasa serikali imefikia hatua nzuri ya udhibiti wa wezi wa fedha wa mitandao lakini bado inatatizwa na mitandao ya kimajii kutoka nje ya nchi. WhatsApp, Facebook na Instagram yote ina kanzidata Marekani.

Pamekuwa na hukumu zinazotokana na Sheria ya Makosa ya Mtandao hata hivyo.

Isaack Emily wa Arusha alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu au kulipa faini ya Sh. milioni saba na Mahakama ya Hakimu Mkazi

Arusha katikati ya mwaka 2016, baada ya kumuona na hatia ya kumtukana Rais John Magufuli kupitia ukurasa wake wa Facebook.

Aidha, Februari 21, mwaka huu wanafunzi wanne wa Chuo Kikuu cha Kampala (KIU) kampasi ya Dar es Salaam, walifikishwa katika

Mahakama ya Wilaya ya Ilala, kujibu shitaka la kusambaza picha za kumkashifu Rais Magufuli kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp.

Washitakiwa hao ni Amenitha Kongo (19), Maria Tweve (20), Agnes Gabriel(21) na Anne Mwansasu(21).

Kwa pamoja walidaiwa kuchapisha picha ambazo zinaonyesha Rais Magufuli akiwa amevaa hijabu kama mwanamke wa Kiislamu na kuzisambaza kwenye mtandao huo wa WhatsApp, huku wakijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.
Post a Comment