Viongozi wa Serikali walio madarakani na wastaafu wakiongozwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan wamejumuika na waombolezaji wengine kuaga mwili wa mwanasiasa mkongwe nchini, marehemu Kingunge Ngombale Mwiru.
Shughuli ya kuaga mwili wa Kingunge imefanyika leo Jumatatu Februari 5,2018 katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam.
Viongozi wengine walioaga mwili wa Kingunge ni marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa aliyeambatana na mkewe Anna; Makamu wa Rais mstaafu, Dk Mohamed Gharib Bilal; mawaziri wakuu wastaafu Dk Salim Ahmed Salim, Frederick Sumaye, Edward Lowassa na mkewe Regina; na Jaji mstaafu Joseph Warioba.
Wengine ni Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula na mtangulizi wake Pius Msekwa; Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Othman Chande; Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad na mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.
Pia, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole; Mama Maria Nyerere; Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye; na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba.
Wengine ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva; Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais –Tamisemi, Selemani Jafo; Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita; na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ali Hapi.
Kabla ya kuanza kutoa heshima za mwisho mwenyekiti wa kamati ya mazishi, Omary Kimbau aliwashukuru viongozi na wananchi waliojitokeza.
Akisoma wasifu wa marehemu, Balozi Ally Mchumo amesema mwanasiasa huyo alizaliwa Mei 30, 1932 wilayani Kilwa mkoani Lindi lakini alikulia Dar es Salaam.
Amesema Kingunge amesoma vyuo vya ndani na nje ya nchi na alifanya kazi serikalini na ndani ya CCM.
Amesema Oktoba 2015, Kingunge alijitoa CCM kutokana na kutokubaliana na mchakato wa chama tawala kumpata mgombea wa urais.
Rafiki wa siku nyingi wa Kingunge, Ally Mtopa amesema waliishi pamoja tangu wakiwa wadogo na hata mwanasiasa huyo mkongwe alipofiwa na mkewe, Pares viongozi mbalimbali walimtafuta ili akamueleze juu ya kifo hicho.
Katika salamu za rambirambi, Jafo amesema Kingunge ameacha historia kubwa katika nyaraka za Taifa.
“Katika ofisi yetu ya Tamisemi mzee Kingunge amefanya kazi kwa kiwango kikubwa mwaka 1985 hadi 1987 na 1998 hadi 2000,” amesema.



No comments:
Post a Comment