Monday, February 5, 2018

Meneja wa TRA Mkoa wa Mara asimamishwa kazi

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Charles Kichere amemsimamisha kazi Meneja wa TRA Mkoa wa Mara Ndg. Nicodemus Mwakilembe kutokana na uzembe wa kutosimamia vizuri matumizi ya Mashine za Kielektroniki za Kutolea Risiti (EFDs) kwa wafanyabiashara wa mkoani kwake.

Uamuzi huo umetokana na ziara ya kushtukiza ya kukagua matumizi ya EFD aliyoifanya Kamshina Mkuu wa TRA kwenye baadhi ya maduka ya biashara Wilayani Bunda Mkoa wa Mara. Akizungumza mara baada ya ziara yake, Kamishna Mkuu Kichere alisema Meneja huyo ameonyesha uzembe wa hali ya juu kwani kuna wafanyabishara wengi mkoani kwake ambao walishalipa fedha kwa ajili ya kupata mashine za EFD lakini mpaka sasa hawajapatiwa mashine hizo.

"Katika ziara yangu nimegundua kwamba, wapo wafanyabiashara ambao walikwisha kulipia mashine tangu mwaka 2013, 2014 na 2015 lakini mpaka sasa bado hawajapatiwa mashine za EFD na wamekuwa wakitumia mwanya huo kama kinga ya kutochukuliwa adhabu na TRA wakati Meneja wa Mkoa yupo na hachukui hatua zozote. Huu ni uzembe uliopitiliza na kamwe siwezi kuuvumilia," alisema Kichere.

Kutokana na uzembe huo, Kamishna Mkuu Kichere amewaagiza Mameneja wote wa TRA nchi nzima pamoja na majukumu mengine, kuhakikisha wanasimamia kikamilifu matumizi ya mashine za EFD katika mikoa yao na amesema hatasita kumuwajibisha Meneja yeyote atakayeshindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

No comments: