Friday, April 5, 2013

SHIRIKA LA WITHOUT MOTHER NA BEZ MAMY WATOA MISAADA YA VITABU VYA KIADA, UJENZI WA DARASA NA MADAWATI KWA SHULE ZA WILAYA YA CHUNYA, RUNGWE NA MBARALI MKOANI MBEYA


Ujenzi wa darasa la awali katika Shule ya Msingi Galula ukiendelea

Waalimu wa shule ya Msingi Mahango wakipanga vitabu walivyopewa msaada na Shrika la Without Mother na Občanské sdružení Bez Mámy
Wilaya ya Mbarali nayo haikusahaulika baada ya shule za Msingi Mahango na Simike kupata msaada wa vitabu vya kiada vyenye thamani ya shilingi 1, 282, 000
Mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi Simike Bw Vituko Issa Akipitia vitabu vilivyotolewa msaada kwa shule yake

Bw Chris Zacharia akiwa na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kisa Bw Usaje Kasitu wakikagua maendeleo ya utengenezaji wa Madawati 32 yaliyofadhiliwa na Without Mother Organization (Tanzania) na Občanské sdružení Bez Mámy (Czech Republic)
Pia Shule ya Msingi Kisa ya Wilaya ya Rungwe imepewa msaada wa madawati 32
Shirika lisilo la kiserikali la Jijini Mbeya WITHOUT MOTHER kwa kushirikiana na shirika mwenza na Jamhuri ya Czech Občanské sdružení Bez Mámy wametoa misaada mbalimbali kwa shule za wilaya ya Chunya, Rungwe na Mbarali ili kuboresha elimu mkoani Mbeya

Akiongea na Mbeya yetu Mwenyekiti wa Without Mother NGO na Mratibu wa miradi ya Africa ya shirika la Občanské sdružení Bez Mámy  Bw Chris Zacharia amesema wametoa TZS  1,170,000 kwa shule ya Msingi Galula kwa ajili ya Ujenzi wa Darasa la awali
Picha zote kwa hisani ya WMO|Občanské sdružení Bez Mámy
..................................................................................................................................................................................................................

WAZIRI MEMBE AITAKA MALAWI IACHE KUTAPATAPA IRUDI KWENYE USULUHISHI

CIMG3067 
Na Benedict Liwenga , Johary kachwamba na Magreth Kinabo – MAELEZO.

  SERIKALI ya Tanzania imeomba  Malawi iache kutapatapa kuhusu mgogoro wa mipaka wa ziwa Nyasa kufuatia Rais  wa nchi hiyo, Joyce Banda kutangaza katika  baadhi ya vyombo vya  habari  kuwa atapeleka  suala hilo kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki(ICJ), badala yake isubiri uamuzi wa jopo la usuluhishi lifanye kazi na litoe maamuzi.

 Aidha serikali   imesema kuwa hata siku moja  haijapelekewa taarifa wala nyaraka za siri kutoka kwa Katibu wa jopo hilo, ambalo linahusisha marais wastaafu wa zamani wa Afrika na wanasheria  kama ilivyodaiwa  na  Rais  Banda katika vyombo hivyo , kuwa kuna Mtanzania anayeitwa Dk. John Tesha ambaye wanaamini ametoa  habari na kuiba nyaraka za siri.
 Akilitolea ufafanuzi   jambo hili, Waziri Membe amesema kuwa   Tanzania na jopo hilo   limestushwa juu ya madai hayo na hatua ya Rais Banda kupoteza imani.
 Kauli hiyo ilitolewa leo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard  Membe, wakati akizungumzia na waandishi wa habari juu ya mgogoro huu  kwenye ukumbi wa mikutano wa wizara jijini Dares Salaam. 

 Kwa kuwa baada ya kuwasilisha barua na nyaraka zake Dk. Tesha hatahusika katika suala hilo ili kuondoa uwezekano wa nchi  hiyo (wenzetu)  kulalamika. Pia   hata marais wastaaafu kutoka katika nchi zenye migogoro ya mipaka   hawatahusika  kwa sababu ya  kuzuia ‘confilict of interest’.       
  “ Serikali ya Tanzania ina imani  na jopo linaloongizwa na Rais mstaafu wa Msumbiji , Joachim Chissano na marais wengine ambao ni  Festus Mogae na Thabo Mbeki ,  kwa kuwa lina watu wenye uzoefu, wataalamu na wachapakazi.  Pia kuna jopo la   wanasheria   na wataalamu wa masuala ya   migogoro limeundwa na ni la watu saba,” alisisitiza Waziri Membe.
  Aliwataja   wanasheria hao kuwa ni Jaji Raymond Ranjeva, ambaye ni Jaji mstaafu wa ICJ, Profesa George Kanyeihamba(Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu ya Uganda, Jaji Baney Afako (Mshauri wa masuala ya sheria kwenye Umoja wa Afrika kuhusu mgogoro wa mpaka wa Sudan), Dk. Gbanga Oduntun(Profesa  wa  Sheria na Mjumbe wa Kamisheni ya mgogoro wa mpaka kati ya Nigeria na Cameroon).
 Wengine ni Profesa Martin   Pratt, (ambaye ni Mkurugenzi wa Utafiti wa Geografia na Mipaka), Dk. Dire David Tladi (Mjumbe wa Kamisheni  ya Sheria ya Umoja wa Mataifa) na Miguel Chisano(Kiongozi wa Chuo kinachoshughulikia mipaka ya Baharini na Nchi Kavu. 
 “   Ni watu wenye heshima ya dunia tusingetegemea— kusema hana imani na jopo hili,” alisema.
  Akirejea mazungumzo ya makubaliano yaliyofanyika Novemba 17, mwaka jana(2012) kuwa walikubaliana  hapo walipo katika jopo hilo ndipo sehemu ya mwisho. Hivyo wataenda ICJ iwapo watashauriwa na jopo la mzee Chissano.
 ‘’Wakati   tunasubiri jopo kufanya kazi na kutoa majibu serikali inaiomba Malawi pale katikati ya Ziwa Nyasa pasiguswe mpaka jibu litakapotolewa na jopo la usuluhishi. Tunaiomba serikali ya Malawi irudi katika jopo la usuluhishi na tutashangaa  ikiwa  Malawi itakwenda  kushtaki ICJ   kwa kuwa  ili Malawi iende ICJ ni lazima sisi  tukubali. Hata pale tutakaposhauriwa   ni lazima sisi tukubaliane na Malawi,” alisisitiza  Waziri Membe.
  Hivyo aliiomba  serikali ya  Malawi iache kutapatapa mara Uingereza, Marekani ,Jumuia ya Madola na Umoja wa Afrika(AU) na kuona viongozi mbalimbali wa dunia, bali iamini jopo la Mzee Chissano. Matokeo ya utafiti wao  upo uwezekano wa kuyakubali au kuyakataa.
  Akizungumzia kuhusu utoaji wa ripoti ya jopo hilo utakuwa ni lini,Waziri Membe alisema Tanzania haina haraka juu ya jambo hilo.
 Waziri Membe  alisema  Tanzania , ilipeleka wataalamu Uingereza na Ujerumani ili kupata uelewa wa kutosha  juu ya jambo hilo, hivyo ina ushahidi wa kutosha.
...................................................................................................................................................................

Malawi Imekurupuka Kususia Mazungumzo


Katika hatua isiyotegemewa, Malawi imetangaza kujitoa katika mazungumzo ya mgogoro wa mpaka kati yake na Tanzania kwenye Ziwa Nyasa. Rais Joyce Banda wa nchi hiyo alisema mwanzoni mwa wiki aliporejea nchini mwake akitokea katika ziara ya Marekani na Uingereza kuwa, sasa mgogoro huo utapelekwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), kwa madai kwamba juhudi za usuluhishi wa kidiplomasia umeshindwa.

Hatua hiyo ya Rais Banda ambayo tunaweza kuiita ya kukurupuka siyo tu imeishtua Tanzania, bali pia Afrika na dunia nzima kutokana na ukweli kwamba mazungumzo kuhusu mgogoro huo yalikuwa yakiendelea vizuri chini ya usuluhishi wa jopo la marais wa zamani barani Afrika chini ya uenyekiti wa Rais mstaafu wa Msumbiji, Joachim Chissano.

Lakini waliokuwa wakifuatilia mgogoro huo kwa karibu watakubaliana nasi kwamba nchi hiyo tangu mwanzo haikuwa na dhamira ya kumaliza mgogoro huo kwa mazungumzo au usuluhishi. Mara zote zilisikika kauli na sauti za viongozi katika serikali hiyo zikibeza juhudi hizo kwamba ni kupoteza muda tu. Tangu mwanzo mkakati wa serikali hiyo ulikuwa kupeleka mgogoro huo katika mahakama za kimataifa.

Ni jambo la kushangaza Rais Banda anaposema hatua ya nchi yake kujitoa katika mazungumzo ya usuluhishi imetokana na kuhujumiwa na katibu wa jopo la usuluhishi ambaye ni raia wa Tanzania, ambaye nchi hiyo inadai alivujisha taarifa muhimu za Malawi kwa Tanzania kabla ya Tanzania haijawasilisha taarifa zake kwa jopo hilo. Kama kweli Malawi ilikuwa na ushahidi wa hujuma hizo kwa nini haikulifikisha suala hilo kwa mamlaka husika, ikiwamo kutaka hatua zichukuliwe dhidi ya katibu huyo?

Mgogoro huo wa mpaka ni wa muda mrefu na unatokana na mikataba yenye utata iliyoachwa na wakoloni. Kwa kutambua hilo marais waliotangulia, hasa Bakili Muluzi na Bingu wa Mutharika wa Malawi na wenzao Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa wa Tanzania, waliendeleza mazungumzo, kwani walitambua kwamba Ziwa Nyasa ni urithi wa wananchi wote wanaoishi katika nchi tatu za Msumbiji, Tanzania na Malawi na kwamba mazungumzo ndio suluhisho pekee la tatizo la mpaka.

Lakini kujitokeza kwa dalili za kuwapo mafuta katika Ziwa Nyasa na baadaye Rais Joyce Banda akaingia madarakani ndiko kulikosababisha Malawi isione tena umuhimu wa kuendelea na mazungumzo. Kwa maneno mengine, suala la mafuta ghafla liliichanganya na kuipofusha Serikali ya Malawi ambayo haikuona tena umuhimu wa kutoa kipaumbele kwa masuala ya ujirani mwema.

Serikali ya Rais Joyce Banda bila kushauriana na Tanzania ilitoa leseni kwa makampuni mawili ya kigeni kutafuta mafuta katika eneo la Ziwa ambalo linamilikiwa na Tanzania.
Hilo ndilo chimbuko la mgogoro uliopo hivi sasa ambao umechukua sura mpya baada ya upande mmoja wa mgogoro huo kupata ndoto za kuneemeka na mafuta.
...............................................................................................................................................................................................................

Lissu: Tutampigania Lwakatare Dhidi ya Kesi ya Ugaidi


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema kwa gharama yoyote kipo tayari kumtetea Mkurugenzi wake wa Ulinzi na Usalama, Wilfred Lwakatare dhidi ya kesi ya ugaidi inayomkabili.

Lwakatare na mwenzake, Joseph Rwezaura, wanakabiliwa na kesi ya ugaidi katika Mahakama ya Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka manne ya kula njama na kufanya mipango ya kumteka, kisha kumdhuru kwa sumu, Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi, Dennis Msacky.

Majalada hayo namba 37 na namba 6 yote ya mwaka 2013, yalishawasilishwa Mahakama Kuu, kwa awamu mbili. Jalada la kwanza, namba 37 liliwasilishwa Mahakama Kuu, Jumatatu na jalada la pili namba 6 liliwasilishwa Jumanne wiki hii iliyopita.

Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa Chadema, Tundu Lissu alisema kuna wanaohoji nguvu ya kisheria wanayoitumia kuweka jopo la mawakili watano kumtetea Lwakatare, akisisitiza kuwa wapo tayari kuhakikisha sheria inatumika ipasavyo kubainisha ukweli wa tuhuma hizo.

Lissu aliyasema hayo jana alipokuwa akieleza msimamo wa baadhi ya mambo yaliyojadiliwa na Kamati Kuu kwenye kikao chake kilichofanyika Dar es Salaam.

Pia, alisema wanamwamini Jaji Lawrence Kaduri aliyepangwa kusikiliza maombi ya kupinga utaratibu wa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP). “Jaji Kaduri aliyepangwa kusikiliza kesi hii aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) miaka kadhaa iliyopita, hivyo tunaamini kwa uzoefu wake alionao kwenye masuala ya sheria ataamua kwa kuzingatia sheria,” alisema.
.................................................................................................................................................................

No comments: