Thursday, May 9, 2013

UTAFITI WA CHANJO YA UKIMWI MBEYA WAENDELEA HUKU UTAFITI HUO UKIONYESHA MATUMAINI YA MAFANIKIO

mwinyi2 a0a18
Dkt. Hussein Mwinyi

Matokeo ya awali ya chanjo ya dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi yaliyofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) yameonyesha kuwa chanjo hiyo ni salama na ina uwezo wa kusisimua mwili na kuzalisha viini kinga katika dozi ndogo.

Akiwasilisha hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa Mwaka wa Fedha wa 20013/2014, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi alisema chanjo hiyo aina ya TAMOVAC-01 imeshirikisha watu 60 katika Mkoa wa Mbeya.
Hii ni mara ya pili kwa Serikali kufanya utafiti kama huo. Mara ya kwanza ulihusisha wanajeshi, askari polisi na magereza wapatao 60 wa Dar es Salaam ambao walipewa dawa na kuachwa waendelee na maisha yao ya kawaida kwa muda wa miaka mitano.
Hata hivyo, alipoulizwa jana jioni kuhusu utafiti huo wa awali ulipoishia Dk Mwinyi alisema: “Huu ni utafiti mwingine ule wa awali ulikatizwa.” Alisema utafiti wa awamu ya pili unaendelea na umeonyesha mafanikio makubwa.
Alisema taasisi hiyo pia iliendelea na utafiti wa awamu ya tatu wa chanjo ya malaria iitwayo RTS, S/AS01E na matokeo yake kwa watoto wa rika la wiki sita hadi 12 yalionyesha kuwa ina ubora sawa na chanjo zitolewazo kwa watoto na inazalisha viini kinga.
“Chanjo hii ilipunguza watoto kuugua malaria mara kwa mara kwa kiwango cha asilimia 30 kwa mwaka mmoja wa ufuatiliaji,” alisema.
Alisema utafiti huo ulihusisha vijiji 34 vya Wilaya za Handeni na Korogwe na jumla ya watoto 1,505 chini ya miezi 17 walipata chanjo ya malaria au chanjo ya kilinganishi na walikamilisha kupatiwa dozi ya nyongeza ilipofikia robo ya nne ya mwaka 2012 na ufuatiliaji unaendelea.
Alisema Serikali imepata mafanikio katika juhudi za kudhibiti magonjwa ya Ukimwi na malaria kutokana na utafiti uliofanywa mwaka 2011/12 kuhusu viashiria vya magonjwa hayo kuonyesha kuwa malaria imepungua kutoka asilimia 18 mwaka 2007/08 hadi asilimia 10 mwaka 2011/12.
Alisema taasisi hiyo itaendelea na utafiti wa chanjo dhidi ya Ukimwi na awamu hii itahusisha washiriki 80 katika Mkoa wa Mbeya lakini pia itaendelea na hatua ya kwanza ya utafiti ujulikanao kama R 262 utakaochunguza aina nyingine ya chanjo ya DA na MVA dhidi ya Ukimwi kwa lengo la kubaini ubora na usalama wa chanjo hiyo mpya kwa kuchanja washiriki 20 mkoani Mbeya.
Waziri Mwinyi alisema wizara imeomba cha Sh47,282,941,000 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambao kati ya fedha hizo Sh36,1000,000 ni fedha za ndani na Sh435,182,941,000 zinatoka kwa asasi za kimataifa na wadau wa maendeleo.
Alipoulizwa baadaye sababu za bajeti hiyo kuwa tegemezi kwa zaidi ya asilimia 80, alisema Serikali imeamua kupeleka fedha nyingine katika matumizi mengine ya msingi baada ya kuhakikishiwa kupatiwa fedha na wahisani.
Alisema wizara pia imepanga kuajiri wataalamu 612 wa kada mbalimbali na kuwapandisha vyeo watumishi 707.
Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Antony Mbassa alizungumzia tatizo la dawa bandia za kupunguza makali ya Ukimwi (ARV) na kuitaka Serikali kutoa taarifa juu ya makopo 4,000 kama yameondolewa sokoni ili watumiaji wasiathirike.
Mwaka jana gazeti hili lilifichua taarifa za kuwapo ARV bandia sokoni baadhi zikiwa zimeanza kutumiwa.
Taarifa hizo ambazo zilithibitishwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), ziliibua mjadala ambao uliilazimu Serikali kuwasimamisha maofisa kadhaa wa Bohari ya Dawa (MSD).
Dk Mbassa alizungumzia dawa ya ‘Kikombe cha Babu wa Samunge’ inayotolewa na Mchungaji Ambilikile Mwaisapile akitaka ifanyiwe utafiti na kushauri kuanzishwa kwa taasisi ya kitaifa ya takwimu za dawa za asili na kuibua mipango itakayohamasisha wananchi kutumia tiba asili. Chanzo: www.mwananchi.co.tz
.................................................................................................................................................................

ZAHANATI YAGEUZWA OFISI YA AFISA MTENDAJI MBARALI MBEYA

JENGO LA LA OFISI YA AFISA MTENDAJI LILILOBOMOKA SASA WAMEHAMIA KATIKA ZAHANATI


HII NDIYO ZAHANATI ILIYOVAMIWA NA MTENDAJI NA KUFANYWA OFISI YA MTENDAJI 

JENGO LA ZAHANATI HIYO SASA NI OFISI YA MTENDAJI 



KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, Uongozi wa Serikali ya Kijiji cha Mpolo kata ya Utengule Wilaya ya Mbarali Mkoa wa Mbeya imegeuza matumizi ya Zahanati ya Kijiji kuwa Ofisi.
             
Hilo limebainika baada ya Waandishi wa Habari kutembelea eneo hilo na kukuta majengo ya Zahanati hiyo yakitumika kama Ofisa ya Mtendaji wa Kijiji, Ofisi ya Mwenyekiti na Ofisi kwa ajili ya Baraza la Usuluhishi la Kijiji.
Mwenyekiti wa Kijiji hicho Andres Mlongosi,  alipohojiwa kuhusiana na tuhuma za kugeuza matumizi ya Jengo ambalo lilitakiwa litumike kwa ajili ya Zahanati lakini wao wanalitumia kama ofisi alikiri kufanya kinyume kwa kile alichodai Serikali ya Kijiji haina ofisi kutokana na jengo lilikuwa likitumika awali kubomoka.
Aliongeza kuwa wako kwenye mpango wa kujenga upya ofisi yao ambapo baada ya kukamilika Jengo hilo litaachwa litumike kama ilivyokuwa imekusudiwa kwa matumizi ya Zahanati ambapo hadi sasa Wananchi hupata matibabu katika Kituo cha Afya cha Utengule, Igurusi au Hospitali ya Misheni ya Chimala sehemu ambazo ni mbali.
Aidha wananchi hao wameendelea kupata adha ya matibabu hasa Wanawake wajawazito ambao hutumia muda mrefu kusafiri kufuata matibabu pamoja na Wazee wasiojiweza ambapo hutembea kwa zaidi ya Kilomita 15.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Utengule, Benyanga Zuberi amethibitisha uwepo wa hali hiyo na kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali  ndiyo iliyosababisha hali hiyo kutokana na kutotuma fedha za kumalizia maeneo yaliyobaki kama Choo.
Alisema suala la kuweka Ofisi kwenye majengo ya Zahanati ni suala la Mpito ambapo baada ya kukamilika kwa ujenzi kwa asilimia zote Zahanati itaendelea kama kawaida hivyo Wananchi wasiwe na wasiwasi kuhusu hali hiyo.
Nao Wananchi wa Kijiji hicho walisema wanasikitishwa na kitendo kilichofanywa na uongozi wa Kijiji cha kugeuza majengo ya Zahanati kuwa ofisi licha ya kutumia nguvu nyingi kuchangia ujenzi huo.
Walisema kitendo hicho si cha uungwana na kinakatisha tamaa wananchi kuendelea kujitolea nguvu na michango katika kufanikisha ujenzi na shughuli mbalimbali za maendeleo kama wataendelea kugeuza matumizi tofauti na inavyokuwa imekusudiwa.
Diwani wa kata ya Utengule Juntwa Mwalyaje alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kwamba Baraza la dharula lililoketi Mei 6, Mwaka huu lilikutana kujadili mustakabali wa zahanati hiyo ambapo walimwomba mganga Mkuu wa Wilaya kuandika barua ya maombi ya fedha za kumalizia ujenzi wa zahanati hiyo ikiwemu ujenzi wa Choo na Nyumba ya Mganga.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Venance Gwaza Mwashala amesema Halamashauri ilishapitisha Shilingi Milioni Tano kwa ajili ya ujenzi wa awamu ya Kwanza ambazo zitaingizwa katika akaunti ya Kijiji wakati wowote kuanzia sasa
Aidha ameutaka uongozi wa kijiji kuongeza nguvu zao ili waweze kukamilisha mapema ujenzi huo na kuletewa waganga na huduma zote ili kupunguza adha kwa wananchi ya kufuata matibabu mbali.
Picha na E.Kamanga 
 .....................................................................................................................................................

WABUNGE WATAKA UMOJA KULINDA AMANI, WACHOCHEZI KUDHIBITIWA

wabunge
NA  MAGRETH KINABO – MAELEZO, DODOMA
 BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania   limeazimia kuitaka Serikali kuchukua mara moja dhidi ya viashara  vya aina yoyote ya uvunjifu wa amani unaojitokeza  ilikuwapa wananchi  matumaini ya kujumuika na kubudu kwa uhuru bila kuwa na hofu ya usalama wao.
 Azimio hilo limepitishwa leo Bungeni kufuatia Mwenyekiti wa  Kamati ya  Bunge ya Ulinzi na Usalama, Anna Abdallah  alipowasilisha Azimio la Bunge la Kulaani Tukio la Kulipuliwa kwa Bomu katika Kanisa la Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi Parokia ya Olasiti, jijini Arusha , Mei 5,mwaka huu.
 “Pamoja na kazi nzuri iliyokwishafanywa na Serikali ya kuwakamata baadhi ya watuhumiwa, Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama kwa kuzingatia majukumu yake ya msingi kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Aprili, mwaka 2013, Kanuni ya 118 ikisomwa  pamoja na nyongeza na Nane, Kifungu cha 6(3),.
  “Inaomba kuleta azimio la kuitka Serikali na vyombo vyote vya ulinzi na usalama kuhakikisha kuwa inatumia uwezo wake wote kuendeleza uchunguzi wa kina na kuwatia nguvuni wale wote waliohusika na tukio hili kubwa na la kinyama na kuwafikisha katika vyombo vya sheria haraka iwezakanavyo ili hatua kali zichukuliwe dhidi yao,” alisisitiza.
  Akichangia azimio hilo, Mbunge wa  Jimbo la Kigoma Kaskazini-CHADEMA Kabwe Zitto alisema  tunaweza kuwa na sheria ya kupiga marufuku lugha za uchochezi kwa Watanzania zinazoweza kuligawa Taifa.
“Mikanda inauzwa hadharani inawagawa Watanzania tunaomba kipengele hiki kamati iingize katika azimio  wanasheria watatusaidia,” alisema Zitto.
 Mbunge wa Jimbo  la  Kibakwe – CCM George Simbachawene alisema; “inaweza  kuwa  ni fursa na kauli zetu tunazotoa kama viongozi wa dini au kisiasa kwa wengine tunawapelekea ujumbe inakuwa ni mapambano”, .
  Kwa upande wake   James Mbatia – NCCR Mageuzi aliiomba Serikali isimamie sheria zilizopo.
 “Wanasiasa   tuna mkono wetu mkubwa kwa yeyote ni wajibu wetu sote usitake kupata maradaka kwa kumwaga damu ya Watanzania. Nawaomba Watanzania tuwe kitu kimoja,” alisema Mbatia .
 Naye Mbunge  Jimbo la Vunjo –TPL Agustino Mrema alitaka jamabo linapotokea hatua zichukuliwe mara moja.
 Aliongeza kuwa wahubiri wanaopewa kibali cha kuhubiri  na wanatukana na kutoa lugha za uchochezi, vikundi au madhehebu vichukuliwe hatau, ambapo alitoa siku saba.
 Mbunge wa Viti Maalum – CCM Getrude Rwakatare aliomba viongozi wa dini kuhuri upendo.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mahusiano na Utaratibu ,  Stephen Wassira, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bunda – CCM ,aliwashauri wabunge kuungana pamoja ili kushinda tatizo hilo.
 “ Waliopatikana watatusaidia Serikali , hakuna atakayepona Serikali itachukua hatua.  Tunaendelea na kazi hiyo hadi nchi inakuwa na amani,” alisema Waziri Wassira.
 Mwenyekiti  wa kamati hiyo  alisema suala la kupitia sheria ni la msingi na kamati hiyo italiangalia. Pia aliongeza hata lugha ya uchochezi hata Bungeni hairuhusiwi kwa pande zote.
 “Jambo hili halifai tumeanzisha sisi humu ndani wimbo watu wanaitikia. Lazima  tuilinde nchi kwa udi na uvumba.
 ”Hakuna  kiongozi atakayechaguliwa kwa udini nchi hii lazima achaguliwe na Wakristo na Waislamu,” alisema.
 Spika wa Bunge hilo, Anne Makinda aliwataka  wabunge kuchunga kauli zao.
 Katika hatua nyingine spika huyo aliondoka kwenda Arusha kwa safari ya siku moja na baadhi wa wabunge ili kutoa pole kwa wananchi wa Arusha.
...........................................................................................................................................

RAIS JAKAYA KIKWETE AIAGA BATALIONI ITAYOJIUNGA NA MAJESHI YA UMOJA WA MATAIFA YA KULINDA AMANI DRC LEO


Amiri Jeshi Mkuu Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimtakia kila la heri  kiongozi wa batalioni ya  wanajeshi wa JWTZ wanaokwenda  kujiunga na  jeshi la Umoja wa Mataifa  kulinda amani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,  katika sherehe za kuwaaga zilizofanyika Msangani, Kibaha, Mkoa wa Pwani leo Mei 8, 2013.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Shamsi Vuai Nahodha na Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange wanashuhudia.
Picha na IKULU


Wanajeshi wa Tanzania wanaokwenda kulinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wametakiwa kudumisha utamaduni wa askari wa kulinda amani wa Tanzania katika maeneo mbali mbali duniani kwa kuifanya kazi hiyo kwa heshima, nidhamu na utii ili kulinda heshima yao wenyewe na ile ya Tanzania.
 
Askari hao wamekumbushwa utamaduni huo wa askari wa kulinda amani wa Tanzania katika maeneo mbali mbali duniani na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete.
 
Rais na Amiri Jeshi Mkuu alikuwa akiwaaga wanajeshi wa Tanzania wanaokwenda kulinda amani chini ya Umoja wa Mataifa katika DRC katika hafla iliyofanyika leo, Jumatano, Mei 8, 2012, kwenye Makao Makuu ya Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu la Tanzania yaliyoko Msangani, Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani.
 
Akizungumza na askari hao, Rais Kikwete amewaambia kuwa hana wasiwasi kuhusu uwezo wao wa kutelekeza majukumu yao yanayowapeleka DRC isipokuwa tu kwamba waifanye kazi hiyo vizuri na kulingana na utamaduni wa majeshi ya kulinda amani ya Tanzania katika sehemu mbali mbali duniani.
 
“Tunakwenda kutelekeza majukumu ya Umoja wa Mataifa, sina shaka kuwa majukumu yenu mnayaelewa vizuri.
 
 Kazi yetu ni kulinda amani na wala hatuendi kupigana na yoyote. Kazi ya kijeshi mnaijua vizuri vile vile na kwa hili pia sina wasiwasi hata kidogo,” amesema Amiri Jeshi Mkuu na kuongeza:
 
“Kubwa ambalo lazima tulikumbuke ni kwamba nchi yetu kila ilikopeleka majeshi ya kulinda amani imejenga utamaduni wa pekee. Imejenga utamaduni wa askari wetu kuifanya kazi ya kulinda amani kwa heshima, kwa nidhamu na kwa utii wa kiwango cha juu. Hii ni heshima kwetu binafsi na heshima kwa taifa letu. Nawashukuruni na nawatakie kila la heri”
 
Kama ishara ya kuagana na askari hao, Rais na Amiri Jeshi Mkuu amemkabidhi Bendera ya Taifa Luteni Kanali Orestess Cassian Komba, Kamanda wa Kikosi cha Tanzania katika DRC ambacho kitajulikana kwa jina la TANZBATT 1-DRC, akimwambia “Bendera na Ikapepee”.
 
Katika jukumu la kulinda amani Mashariki mwa DRC, Kikosi cha Tanzania chenye askari 1281, kitajiunga na vikosi vya Malawi na Afrika Kusini ambavyo vyote vitakuwa chini ya Kamanda wa Brigedi hiyo, Brigedia Jenerali James Mwakibolwa wa Tanzania pia.
 
 Kundi la kwanza la askari hao Tanzania linaondoka nchini kesho.
 
Majeshi hayo ya Tanzania yatalinda amani katika DRC chini ya Azimio Nambari 2098 (2013) la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
 
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
....................................................................................................

No comments: