Tuesday, June 18, 2013

MKUU WA MOKOA WA MBEYA KANDORO AWAKABIDHI HATI MILIKI ZA MASHAMBA WAKULIMA WA CHAI RUNGWE MKOANI MBEYA


Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro akihutubia wananchi wa kijiji cha Ntandabala kata  ya Masoko Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya wakati wa  hafla ya kugawa Hati Miliki kwa wakulima wa Chai iliyofanyika katika viwanja vya Tarafa ya Pakati.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya AbbaS Kandoro akiwa na baadhi ya Viongozi wa Wilaya ya Rungwe wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo Crispin Meela wa nne kutoka kushoto wakati wa  hafla ya kugawa Hati Miliki kwa wakulima wa Chai iliyofanyika katika viwanja vya Tarafa ya Pakati.Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro akimkabidhi  mwananchi wa kijiji cha Ntandabala kata  ya Masoko Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya wakati wa  hafla ya kugawa Hati Miliki kwa wakulima wa Chai iliyofanyika katika viwanja vya Tarafa ya Pakati.
Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro akisalimiana na mwananchi wa kijiji cha Ntandabala kata  ya Masoko Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya wakati wa  hafla ya kugawa Hati Miliki kwa wakulima wa Chai iliyofanyika katika viwanja vya Tarafa ya Pakati.
                
Baadhi ya wananchi wakifuatilia kwa makini zoezi la ugawaji hati miliki za mashamba
Halmashauri za Wilaya kutengeneza mipango mizuri ya matumizi bora ya Ardhi vijijini ili kuepusha  migogoro ya mara kwa mara ikiwa ni pamoja na kutenga bajeti kwa ajili ya kusaidia zoezi la upimaji
 
Hayo aliyasema juzi katika hafla ya kugawa Hati ya Haki miliki za Ardhi za kimila kwa wakulima wa Chai iliyofanyika katika viwanja vya makao makuu ya Tarafa ya Pakati iliyopo  katika Kijiji cha Ntandabala kata ya Masoko Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya.
 
Kandoro alisema ili kuepusha migogoro inayotokana na ardhi ni vema Halmashauri ikatengeneza mpango wa matumizi bora ya ardhi kama kutenga eneo lawazi, shule, zahanati na maeneo ya kupitisha miundombinu mapema kabla ya kuanza kuwagawia wananchi.
 
Aidha amewasihi Wakulima kuhakikisha wanazitunza vizuri Hati miliki walizopewa kwa kuogopa kutapeliwa na watu wengine ambao wanaweza kuwanyang’anya hadi mashamba yao na wao kuishia kuwa maskini kutokana na kutokuwa na haki na ardhi yake.
 
“ Hakikisheni mnazitunza vizuri kuepuka matapeli, pia chukueni Hati hiyo kama kielelezo kinachokuhakikishia kuwa wewe ndiye mmiliki halali wa ardhi hiyo popote utakapokuwepo pia yatunzeni na kuyaendeleza maeneo hayo” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
 
Aliongeza kuwa Hati Miliki pia husaidia kuepusha migogoro ya mirathi na kunyanyaswa kwa wajane  kutokana na kuwepo kwa Hati inayoonesha mmiliki halali wa Ardhi hiyo.
 
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Crispin Meela akitoa taarifa kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya alisema Jumla ya wananchi 400 wameitikia wito wa kupimiwa ardhi na kukabidhiwa hati miliki zao hivyo kuwafanya kuishi maisha bora kama Ilani ya Chama cha Mapinduzi inavyotaka.
 
Meela alisema mradi wa upimaji wa mashamba kwa wakulima hao umefanywa na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania( Mkurabita)na kwamba jumla ya vijiji saba vimenufaika ambavyo ni Bujela, Nsongole, Njugilo, Kyambambembe, Nsyasya, Ntandabala na Bulongwe.
 
Naye Mratibu wa Mradi wa Mkutabita Gwabo Mwansasu alisema Mradi huo umeanza kutekelezwa Novemba Mwaka jana kwa awamu mbili ambapo mchakato wa awamu ya kwanza ulianza kufanyika mwaka 2004/2005 kwa ufadhili wa Abbott Axio ikiwa na lengo la kuwasaidia wajane na watoto yatima wa kata ya  Kinyala kumiliki ardhi yao.
 
Aliongeza kuwa awamu ya pili ilitekelezwa na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ufadhili wa European Union Mwaka 2007/2008 kwa vijiji 16, ambapo Vijiji 8 kutoka Rungwe Mashariki na Vijiji 8 kutoka Rungwe Magharibi.
 
Mwansasu alisema katika Mradi wa sasa wa awamu ya tatu umetekelezwa na Mkurabita kwa kushirikiana na Bodi ya Chai Tanzania pamoja na wakala wa maendeleo ya Wakulima wadogo wa Chain a lengo likiwa ni kupima mashamba ya Chai.
 
Alisema Mradi huu wa uwezeshaji wakulima wa Chai skimu ya Segera inayojumuisha vijiji 19 vya Masukulu, Kyambambembe, Segera, Mpombo, Ijigha, Ntandabala, Matwebe, Busisya, Bulongwe, Mpumbuli, Nsongola, Nsyasya, Bujela, Njugilo, Lufumbi, Kasyeto, Igembe, Kiloba na Ngaseke.
 
Mratibu huyo aliongeza kuwa Mradi huo ulianza Novemba 19, Mwaka  2012 na kukamilika Juni 15, Mwaka huu ambapo umegharimu Shilingi 64,078,440/= kwa awamu mbili fedha zilizotolewa na wafadhili.
 
Alisema Jumla ya mashamba ya wakulima 1891 yenye ukubwa wa Hekta 485.12 yamepimwa na kutolewa hati miliki za kimila 400 zenye ukubwa wa Hekta 160.45 kwa vijiji saba.

 Na Mbeya yetu.

 .................................................................................................................................

MABOMU YA MACHOZI YARINDIMA Arusha

rpc 8b91a
RPC Arusha, Liberaus Sabas
Hali si shwari katika uwanja wa Soweto  Arusha kufuatia mabomu ya machozi kupigwa ili kutawanya watu waliokusanyika katika viwanja hivyo kwa ajili ya kuuga miili ya marehemu waliokufa kwenye mlipuko wa bomu hivi juzi.

Habari kutoka mitandao mbalimbali zinaeleza kuwa wabunge wa CHADEMA wametanyika kila mmoja upande wake na kadhaa inadaiwa kuwa wamekamatwa na polisi. Mabomu ya machozi yanapigwa maeneo mbalimbali ya jiji hilo na watu wamejifungia majumbani mwao.

Awali Jeshi la polisi lilipiga marufuku CHADEMA kufanya shughuli zozote za kuaga miili ya marehemu kwenye viwanja vya Soweto kwani zoezi la uchunguzi bado linaendelea kwenye viwanja hivyo huku mabomu yakirindima uwanjani hapo.

Akizungumza ofisini kwake kamanda wa polisi mkoani hapa Liberatus Sabas alisema kutokana na uchunguzi unaoendelea wa tukio la bomu kwenye viwanja hivyo imeonelea kuwa si busara kuweka mkusanyiko wa watu kwani kutaharibu upelelezi.

Kamanda Sabas alisema kuwa kwa hiyo jeshi hilo limewataka viongozi wa chama hicho kuwaeleza wafuasi wao mahali sahihi watakapoweza kufanyia shughuli hiyo lakini si kwenye viwanja hivyo.
Hali kwenye viwanja hivyo imekuwa ya pilika pilika tangia juzi kwa wafuasi wa chama hicho kujikusanya tokea asubuhi hadi jioni kwa madai ya kuomboleza tukio la bomu la kurushwa kwa mkono lililotokea uwanjani hapo juzi.

Hata hivyo viongozi wa chama cha demokrasia na maendeleo walikuwa wamukusanyana kwenye uwanja huo hali iliyoendelea kuleta mvutano kati ya viongozi  wa jeshi la polisi na  wafuasi hao baada ya kukaidi amri ya jeshi hilo mabomu yalirindima uwanjani hapo.

Baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho walikuwepo uwanjani hapo akiwemo mbunge wa jimbo la ubungo John Mnyika,Ezekia Wenje na wabunge mbali mbali wa chama hicho walikuwa kwenye kikao cha bunge kinachoendelea hali hiyo imeliweka jiji hili kusimama shughuli zake kutokana na mabomu hayo. Chanzo: Fuullshangweblog na mitandao mingine.

 TUKIO SIKU YA MLIPUKO

MLIPUKO WATOKEA KATIKA MKUTANO WA CHADEMA, BOMU LAJERUHI NA KUUA JIJINI ARUSHA
 


Majeruhi. Mungu urehemu tz
ARUSHA.
MKUTANO wa Chadema wa kumaliza kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani mjini Arusha, jana ulivunjika baada ya bomu kulipuka na kuua watu wawili na wengine kujeruhiwa.

Bomu hilo lililipuka jana saa 11:50 dakika chache kabla ya Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe kumaliza kuhutubia mkutano huo uliofanyika katika Viwanja vya Soweto mjini Arusha na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi.
 
Hilo ni tukio la pili la bomu kulipuka katika mkusanyiko wa watu, Mei 5 mwaka huu bomu lililipuka katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasit mjini Arusha na kuua watu watatu na wengine kujeruhiwa.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mount Meru Frida Mokiti alisema katika hospitali yake kuna maiti moja ya mtoto na majeruhi 11.
 
Habari zingine zilisema katika hospitali ya Misheni ya Selian kuna maiti za watu wawili, waliokufa kutokana na shambulio hilo na majeruhi ambao idadi yao haijafahamika.
Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema katika tukio hilo watu wawili wamepoteza maisha, mwanamke na mwanamume na kwamba idadi ya majeruhi bado haijafahamika kwa kuwa wametawanywa katika hospitali mbalimbali mkoani humo.
Watu walioshuhudia tukio hilo waliliambia gazeti hili kuwa bomu hilo lililipuka karibu na jukwaa walilokuwa wamekaa viongozi wa Chadema, wakati Mbowe na Mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema wakiwa katika hatua za kumaliza kuhutubia.
 
Taarifa zilidai kuwa kuna mtu alionekana akirusha kitu kinachodaiwa bomu kwenye eneo la jukwaa karibu na gari la matangazo la chama hicho, lakini alipokuwa akifuatiliwa baada ya kutokea mlipuko huo, polisi nao walikuwa wameanza kudhibiti watu kwa kulipua mabomu ya kutoa machozi na kupiga risasi za moto hali iliyozidisha taharuki.
 
Baada ya tukio hilo watu waliokuwa katika mkutano huo walitawanyika wakikimbia kuokoa maisha yao huku wakimwacha Mbowe na Lema na viongozi wengine wakiwa bado wako jukwaani.
Hali hiyo ilifanya barabara zote za mji wa Arusha kujaa watu waliokuwa wakikimbia ovyo.
Hali hiyo ya watu kukimbia ovyo kuliwafanya askari polisi wengi kuingia mitaani kudhibiti watu na hivyo nao kulazimika kutumia mabomu ya machozi hali ambayo ilizidisha taharuki.
Baadhi ya watu waliojeruhiwa walikimbizwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru na wengine katika Hospitali ya Seliani na wafuasi wa Chadema na watu wengine waliokuwa katika eneo hilo.
...............................................................................................................................................................
Post a Comment