Friday, June 28, 2013

Serikali yatoa tamko polisi kuua raia

 

silima 06919
Serikali imetoa tamko bungeni kuhusu mauaji ya raia mikononi mwa polisi ikieleza kuwa sheria ya kanuni ya adhabu inaruhusu kutumia nguvu za kadiri hata kiasi cha kusababisha madhara au kifo.

Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kunukuliwa bungeni akiwataka polisi kuwashughulikia kwa kuwapiga watu wote wanaokaidi kutii sheria.
“…Nasema wapigwe tu, maana tumechoka sasa,” alisema Pinda alipojibu maswali ya papo hapo Alhamisi iliyopita.

Akisoma tamko hilo bungeni jana, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Pereira Ame Silima alisema kuwa kifungu cha 18(B) na 18(C) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu kinatoa uwezo kisheria wa kutumia nguvu za kadiri hata ikibidi kiasi cha kusababisha madhara au kifo katika mazingira ya kisheria.

Aliyataja mazingira hayo kuwa ni pamoja na kuokoa uhai wa mtu mwingine, kuzuia madhara makubwa ya mwili yasitokee kwake au kwa mtu mwingine na kumzuia mtu anayetenda tendo ovu la kubaka au kunajisi mtoto au kufanya vitendo kinyume na maumbile.
Pia kumzuia mtu anayevunja nyumba usiku au unyang’anyi wa kutumia silaha au kuchoma nyumba moto au kufanya kitendo chochote kinachohatarisha uhai wa mtu au mali.
Alieleza kuwa Kifungu cha 18 na 18(A) cha Sheria ya Adhabu Sura namba16 iliyofanyiwa mapitio mwaka 2002, kinampa haki mtu yeyote akiwemo askari kujilinda, kumlinda mtu mwingine, kulinda mali yake au mali ya mtu mwingine ikiwemo ya Serikali na taasisi zake, ambayo iko chini ya uangalizi wake kisheria.

Kauli hiyo ya Serikali kuhusu mauaji ya raia mikononi mwa polisi, ilitolewa ikiwa ni ufafanuzi wa jibu la swali la nyongeza lililoulizwa bungeni Mei 28,2013 na Rashir Ally Abdalah (Tumbe-CUF), ambapo Silima alisema mauaji yanayofanywa na askari polisi ni mauaji ya kisheria. Kutokana na kauli hiyo, Mbunge wa Wawi, Hamad Rashi Mohammed aliomba mwongozo wa spika kupata ufafanuzi wa kauli hiyo, na jana Silima kutoa kauli ya Serikali kujibu mwongozo huo.

“Ikumbukwe pia kuwa, kifungu cha 29 cha Sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi wasaidizi Sura322, pamoja na Kanuni za Kudumu za Utendaji za Jeshi la Polisi Na274, vinampa haki ya kisheria askari polisi kubeba na kutumia silaha za moto ikiwamo bunduki na mabomu katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku..,”alisema Silima.
Alifafanua kwamba katika kutafsiri sheria, kanuni na taratibu mbalimbali ikiwamo alizozitaja, mahakama katika nyakati tofauti imetoa msimamo wa kisheria juu ya suala hilo.
Akitoa mfano alisema: “Mathalan katika kesi ya Seif Mohamed Senzagala dhidi ya Jamhuri ya mwaka 1994 kama ilivyonukuliwa na Tanzania Law Report ukurasa wa 122, ambapo mshitakiwa (mwomba rufaa) alimjeruhi kwa panga mlalamikaji ambaye alimfuata nyumbani kwake na kuanza kumshambulia.”

Alisema katika kesi hiyo,mahakama ya rufaa pamoja na kuridhia uamuzi wa mahakama ya awali wa kumtia hatiani kwa kutumia nguvu kupita kiasi, ilibainisha kuwa mshtakiwa hakustahili adhabu kwani alitenda kosa lile wakati akijihami dhidi ya mashambulizi toka kwa mlalamikaji.
“Kwa msingi huo, tarehe 28 Mei, 2013 wakati nikijibu swali Na 290, nilitumia maneno ‘mauaji yanayofanywa kisheria’ nikimaanisha mauaji yanayotokea katika mazingira niliyoeleza..,”alisema Silima.

Hata hivyo alisema siyo nia ya Serikali kuhalalisha vitendo vya matumizi mabaya ya silaha ambavyo vinaweza kufanywa na askari wasio waadilifu.
Alibainisha kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria, kuheshimu haki za raia na kutumia busara kutatua migogoro.
Hata hivyo, Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni imelaani kauli ya Serikali kuhusu mauaji ya raia mikononi mwa polisi iliyoitoa jana na kueleza kuwa haikubaliani nayo kwa kuwa inatoa baraka kwa polisi kuendeleza mauaji ya raia.
Akizungumza na gazeti hili baada ya kikao cha bunge kuahirishwa, Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani wa kambi hiyo rasmi, Vicent Nyerere alisema kauli hiyo ingekuwa na uthabiti kama askari polisi wangekuwa waadilifu.

“Kauli ingekuwa thabiti kama polisi wangekuwa waadilifu. kabla ya kutoa kauli hiyo, Serikali ilitakiwa kuchuja miongoni mwa askari wa jeshi la polisi, wa ngazi zote na kuwaondoa wasio waaadilifu ndipo wakatoa kauli hiyo wananchi wataielewa Serikali,”alisema Nyerere ambaye pia ni Mbunge wa Musoma Mjini(Chadema).
Kwa upande wake, Mbunge wa Ole, (CUF) Rajab Mbarouk Mohammed akizungumzia kauli hiyo ya Serikali alisema kuwa majibu ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Pereira Ame Silima ni ya kisiasa.
Alisema kwamba kauli hiyo ni mwendelezo wa kauli iliyotolewa Alhamisi iliyopita na Waziri Mkuu,Mizengo Pinda akiwataka pilisi kuwashughulikia kwa kuwapiga watu wote watakaokaidi kutii sheria.
“Hakuna mwenye haki ya kuua, kuua ni kuua tu. Mahakama pekee ndiyo ina haki ya kuhukumu kifo baada ya kumtia hatiani mshtakiwa husika. Lakini kuwa polisi wanafundishwa utii, siyo kuua,”alisema Rajab.
Alifafanua kuwa kazi ya polisi ni kulinda raia na mali zao na kwamba kuruhusiwa kujihami haimaanishi kuua raia.

Nao Wabunge Aeshi Hilaly na Aly Keissy walisema ni vizuri raia wakatii mamlaka iliyopo na kutekeleza utii wa sheria bila shuruti.
Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu alisema: “Maoni yangu haki za watuhumiwa lazima ziheshimiwe.”

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, (TLS), Francis Stola alisema hakuna sheria inayompa mamlaka askari polisi kutumia nguvu za ziada ikiwemo kupiga raia pindi anapotekeleza majukumu yake,isipokuwa tu anaweza kutumia nguvu kiasi iwapo raia anayekabiliana naye anaonyesha vitendo vya kukaidi amri ama kuhatarisha usalama.
Stola ambaye alikuwa akitoa ufafanuzi wa kisheria kuhusiana na kauli bungeni alisema kuwa kwa kufuata sheria polisi haruhusiwi kupiga raia. “ Ukisoma sheria hakuna mahala utakuta kuna neno limeandika piga…. Askari polisi anachoweza kufanya ni arrest(kamata) na siyo vinginevyo, hana mamlaka kabisa ya kupiga raia”

Alisema sheria imetamka wazi kuwa kunapojitokeza hali yoyote inayopaswa kdhibitiwa na vikosi vya ulinzi, nguvu inayopaswa kutumika ni ile ya kawaida na kwamba kitendo cha kutumia risasi za moto ama kupiga raia ni ukiukwaji wa sheria za nchi.
Alisema polisi anapaswa kutoa mwongozo kwa raia kumwelekeza jambo la kufanya iwapo kunajitokeza hali ya sintofahamu,lakini hapaswi kutumia nguvu kupita kiasi ikiwemo kuwapiga raia

“ Sheria inasema wazi kwamba panapojitokeza hali yoyote korofi, polisi wanatakiwa kutumia nguvu ya kawaida tu kukabiliana na hali hiyo na wala siyo kutumia silaha za moto… silaha za moto zinaweza kutumika tu iwapo kunajitokeza tukio ambalo linaweza kuhatarisha usalama wa maisha ama mali isipotee” alisema

Kuhusu wananchi kufanya maandamano, rais huyo alisema maandamano ni haki ya msingi ya kila raia,lakini yanafanyika katika utaratibu maalumu. “ maandamano ni haki ya kila raia lakini panapaswa kuwa na utaratibu maalumu…. Kama kunajitokeza maandamano ambayo hayana utaratibu polisi wanapaswa kutumia reasonable force (nguvu ya kawaida) kudhibiti maandamano hayo na wala siyo kutumia nguvu za ziada. Chanzo: mwananchi

...............................................................................................................................

Leo

DSC 0064 13dba

 DSC 0066 8089a

 .................................................................................

  "Likilipuka moto hapo utasikia oooo Serikali....."

Gari la kubebea mafuta laanguka Kibaha, watu "kama kawaida" na vidumu vyao...2093648 orig 8c4d3
7076096 orig aa465Lori moja la kubebea  mafuta ya vyombo vya moto likiwa limeanguka eneo la Kongowe, Kibaha kama lilivyokutwa na mpiga picha jioni ya leo. Wananchi wanaonekana wamelizungukaa   hawanahofu ya hatari inayoweza kutokea kama zilivyotokea nyingine siku zilizopita

 .............................................................................................................................

Ajali mbaya yatokea katika eneo la maji masafi Kawetere Nje kidogo ya Jiji la Mbeya barabara ya Mbeya- Tabora Kichanga afariki dunia wengine wajeruhiwa.

Mtambo wa Wachina ukinyenyua gari la Kampuni ya Sabena baada ya kupata ajali eneo la maji mazuri Kawetere barabara ya Chunya likiwa linaelekea Tabora leo Asubuhi.


Baadhi  ya abiria walionusurika  wakihamisha mizigo yao kutoka katika gari lililopata ajali ya Kampuni ya Sabena baada ya kupata ajali eneo la maji mazuri Kawetere barabara ya Chunya likiwa linaelekea Tabora leo Asubuhi.

Wachina wanaojenga barabara ya Chunya wakishangaa gari la Kampuni ya Sabena baada ya kupata ajali eneo la maji mazuri Kawetere barabara ya Chunya likiwa linaelekea Tabora leo Asubuhi.
Majeruhi wa ajali hiyo Ramadhani Kipese (45) akiwa na majeraha kichwani.

Kondakta wa gari la Kampuni ya Sabena Seif Salum (34) akisaidia kuokoa mizigo ya abiria baada ya kupata ajali eneo la maji mazuri Kawetere barabara ya Chunya likiwa linaelekea Tabora leo Asubuhi.

Gari la Polisi likiwa eneo la tukio kuokoa mizigo ya majeruhi walolazwa katika Hospital ya Rufaa ya Mbeya.
                             ********************************************
KICHANGA cha Miezi 6 kimefariki dinia papo hapo na wengine zaidi ya 60 wamenusurika kufa  katika ajali mbaya iliyohusisha Basi kampuni ya Sabena baada ya kuacha njia na kutumbukia katika Mtaro  pembezoni mwa Barabara eneo la Maji mazuri Kawetere nje kidogo ya Jiji la Mbeya.
Kwa mujibu wa Wahanga wa ajali hiyo iliyotokea jana wamesema imetokana na mwendokasi ambapo Dereva alishindwa kulimudu basi hilo lililokuwa likitokea Mbeya kuelekea Mwanza.
Wamesema ajali hiyo imetokea majira ya Saa moja asubuhi  ambapo katika ajali hiyo watu kadhaa walijeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya huku wengine wakipatiwa huduma ya kwanza kisha kuendelea na safari baada ya kubadilishiwa gari.
Gari hilo lenye namba za usajili T 887 AYG liliharibika vibaya na kushindwa kuendelea na safari ndipo lilipoletwa basi lingine kampuni hiyo hiyo ya Sabena kwa ajili ya kuendelea na Safari.
Kondakta wa Basi hilo Seif Salum(34) amesema chanzo cha ajali hiyo ni ubovu wa gari uliosababisha kupasuka kwa mpira wa Breki hivyo gari kushindwa kusimama na kutumbukia mtaroni.
Amemtaja Dereva wa basi hilo kuwa ni Suddy Hussein ambaye inasadikika kuwa alikimbia baada ya ajali hiyo ingawa kondakta alitoa taarifa kuwa kafuata matibabu Hospitalini.
 Picha na Mbeya yetu.
Post a Comment