Friday, July 5, 2013

Uholanzi yadhamini mafunzo ya gesi kwa watanzania

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akisikiliza jambo toka kwa balozi wa Uholanzi anayemaliza muda wake Mheshimiwa Ad Koekkek  aliyefika ofisini  kwake kwa lengo la kumuaga

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akipeana mkono na  balozi wa Uholanzi anayemaliza muda wake Mheshimiwa Ad Koekkek ofisini kwake Dar es Salaam.


Balozi wa Uholanzi hapa nchini aliyemaliza muda wake Mhe. Ad Koekkek amesema serikali yake imeandaa mpango wa mafunzo kwa vitendo kwa watanzania yanayohusu upimaji thamani ya gesi.

Aliyasema hayo hivi karibuni alipomtembelea Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ofisini kwake jijini Dar es Salaam kwa nia ya kumuaga rasmi.

Kwa mujibu wa Balozi Koekkek, mafunzo hayo yatakayotolewa nchini Uholanzi yatahusisha wataalamu kumi wa sekta ya gesi kutoka Wizara ya Nishati na Madini na kwamba serikali ya Uholanzi itagharamia gharama zote.

Kwa upande wake Prof. Muhongo pamoja na kushukuru kwa niaba ya serikali ya Tanzania, alisema kuwa mafunzo hayo ni muhimu sana. Aidha, alishauri wataalamu kutoka Uholanzi kuja nchini na kuelimisha watu wengi zaidi kwani watanzania wanaopata nafasi kusoma nje ya nchi ni wachache.

Alifafanua kuwa wataalamu wanaohitajika zaidi ni wanaoweza kufundisha masuala ya gesi na petroli katika vyuo vikuu, ambapo kwa hapa nchini watafundisha katika vyuo vikuu vya Dodoma, Dar es Salaam, pamoja na Chuo cha Madini Dodoma. 
.......................................................................................................

No comments: