Wednesday, August 7, 2013

TAARIFA YA SIKU KUU YA EID KUTOKA JESHI LA POLISI


3 c9818
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI
JESHI LA POLISI TANZANIA

Anuani ya Simu “ MKUUPOLISI”                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                   Ofisi ya  Inspekta  Jenerali wa Polisi,
Simu : (022) 2110734                                                                                    Makao Makuu ya Polisi,
Fax Na. (022) 2135556                                                                                                         S.L.P. 9141,
Unapojibu tafadhali taja:                                                                                    DAR ES SALAAM.

          



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Dar Es Salaam Agosti 06, 2013.

Ndugu Wanahabari,
Jeshi la Polisi Nchini linatoa shukrani kwa wananchi wote wakiwemo waandishi wa habari, viongozi wa dini, wanasiasa, makampuni binafsi ya ulinzi kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa kwa njia mbalimbali katika kuhakikisha kwamba nchi yetu ya Tanzania inakuwa salama na raia wote wanaishi kwa amani na utulivu bila hofu ya uhalifu na wahalifu.

Katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu ya Eid-El-Fitr, Jeshi la Polisi linatoa tahadhari kwa wananchi wote kuwa makini na kuchukua hatua stahiki na za haraka kwa kutoa taarifa pindi wanapoona viashiria vyovyote vya uhalifu katika maeneo wanamoishi na sehemu mbalimbali zikiwemo maeneo ya biashara.

Ikumbukwe kuwa, wananchi wenye imani ya kiislam na hata madhehebu mengine hutumia muda huo kwenda kuabudu pamoja na muendelezo wa sherehe hizo kwenye maeneo mbalimbali ya starehe. Uzoefu unaonyesha kuwa baadhi ya watu hutumia kipindi hicho cha sikukuu kama mwanya wa kufanya matukio ya uhalifu kutokana na mikusanyiko hiyo ya watu. Jeshi la Polisi limejipanga vizuri kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama katika kuhakikisha kwamba, wananchi wote wanasherekea sikukuu hiyo kwa amani na utulivu, pasipo vitendo ama viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani.

Ulinzi umeimarishwa kwenye maeneo yote ya kuabudia, fukwe za bahari, sehemu za starehe na maeneo mengine yote ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu.

Aidha, wale wote ambao watakuwa wakitumia barabara, wanatakiwa kuwa makini kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani na hasa kwa madereva wa magari na pikipiki kuepuka kwenda mwendo kasi na kutumia vilevi wawapo kazini.

Katika kuhakikisha usalama kwenye kumbi za starehe, wamiliki wa kumbi hizo wazingatie uhalali na matumizi ya kumbi zao katika uingizaji wa watu kulingana na uwezo wa kumbi hizo, badala ya kuendekeza tamaa ya fedha kwa kujaza watu kupita kiasi. Vilevile, wazazi wawe makini na watoto wao na hasa disko toto, ili kuepuka ajali na matukio mengine yanayoweza kusababisha madhara juu yao.

Wananchi wanatakiwa kuwa makini hususani watokapo kwenye makazi yao, wasiache nyumba wazi ama bila mtu na pale inapobidi watoe taarifa kwa majirani zao. Wanapowatilia mashaka watu wasiowafahamu wasikae kimya bali watoe taarifa haraka kwenye vituo vya Polisi vilivyo karibu nao ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa haraka.

Vilevile, Jeshi la Polisi linawatahadhalisha wananchi kuwa makini na matapeli yanayotumia majina ya viongozi, watu maarufu na wafanyabiashara wakubwa ili kujipatia pesa na vitu mbalimbali. Matapeli hao wamekuwa wakitumia ujumbe mfupi wa simu za mkononi kupata taarifa za mtu binafsi hatimae mtu huyo kuibiwa.

Ndugu wanahabari,
Kufuatia agizo la Mhe. Rais la kuwataka watu wote wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kusalimisha silaha hizo, pamoja na watu wote wanaoingia ama kuishi na kufanya shughuli hapa nchini bila kufuata utaratibu (wahamiaji haramu) kutakiwa kuondoka au kuharalisha ukaazi wao, Jeshi la Polisi linawataka watu hao kuendelea kutekeleza agizo hilo la Serikali kabla ya Operesheni kabambe kuanza itakayoendeshwa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Vyombo Vingine vya Ulinzi na Usalama.

Aidha, baadhi ya watu hao tayari wamekwishasalimisha silaha wanazozimiliki kinyume cha sheria na pia baadhi ya wahamiaji haramu wameanza kuondoka hususani katika mikoa ya Kagera na Kigoma. Hiyo ni hatua nzuri, tunawataka wale wote ambao bado hawajatekeleza agizo hilo, waendelee kufanya hivyo haraka kabla ya muda wa msamaha kumalizika.

Mwisho, napenda kuwahakikishia wananchi kwamba, Jeshi la Polisi linatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria za nchi na hivyo halitawajibika kumwonea huruma ama upendeleo mtu yeyote atakayeenda kinyume na sheria.


NAWATAKIENI WATANZANIA WOTE SIKUKUU NJEMA YA
EID –EL-FITR

Imetolewa na:-
Advera Senso- SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.

 

 .................................................................

WALIOUA PUNDA NA KUMTUPA MTONI MOMBA MBEYA WAKAMATWA NA KUADHIBIWA KWA KUCHARAZWA VIBOKO KISHA KUACHIWA HURU

 Wakicharazwa viboko na mgambo baada ya kukamatwa.
 Fimbo hizo ni silaha walizokuwa wakizitumia kukaidi sheria bila shuruti na kujeruhi kila aliyewakaribia huko Chilulumo wilaya ya Momba mkoani Mbeya.

Hapa wakiwa mikononi mwa wanafunzi wa wanamgambo waliofanikiwa kuwakamata vijana hao ambao ni kabila la Wasukuma.

* Baada ya viboko, watakiwa kuhudumia mashamba ya mtu waliyemjeruhi kwa fimbo.

* Walitupa mzoga kwenye mto unaotumiwa na wanakijiji.

* Wanafunzi wa mafunzo ya Mgambo wafanikisha kuwanasa.

No comments: