Monday, August 5, 2013

Wanafunzi 5,000 washindwa kuingia vyuo vikuu

057 23c5b
Siku chache baada ya kufungwa kwa pazia la udahili kwa wanafunzi wa kidato cha sita walioomba kujiunga na vyuo vikuu nchini, imebainika kuwa zaidi ya wanafunzi 5,000 wameshindwa kujiunga na vyuo hivyo kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo matumizi ya mtandao wa kuomba udahili. (HM)
 
Pazia la udahili huo kwa wanafunzi waliomaliza kidato cha sita mwaka huu, lilifungwa rasmi Julai 5, mwaka huu. Hadi wakati unafika tarehe hiyo, wanafunzi waliokuwa wameomba nafasi hiyo ni 39,140.


Matokeo ya kidato cha sita mwaka huu, yanaonyesha kuwa watahiniwa 50,611 walifanya mtihani huo na kati yao 44,366 sawa na watahiniwa wa shule waliofaulu ni 40,242 sawa na asilimia 93.92 ya waliofanya mtihani huo.
 

Watahiniwa wa kujitegemea waliofanya mtihani huo walikuwa ni 7,659 na waliofaulu ni 4,124 sawa na asilimia 53.87. Kutokana na matokeo hayo, watahiniwa wote waliofaulu ni 44,366, hivyo kufanya wanafunzi walioshindwa kujiunga na vyuo vikuu kuwa 5,226.
 

Akizungumza na Mwananchi Jumamosi, Mkurugenzi wa Ithibati na Ubora wa Elimu ya Juu wa Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU), Dk Savinus Maronga alisema, wanafunzi waliomaliza kidato cha sita na kuomba kujiunga na vyuo vikuu ni 39,140 na kwamba vyuo vikuu nchini vina uwezo kwa kuchukua wanafunzi 60,000.
 

Dk Maronga alisema hali hiyo inatokana na baadhi yao kutokuwa na sifa zinazotakiwa kuweza kuomba udahili wa kumwezesha kusoma elimu ya juu.
 

“Kuna baadhi hawana sifa ‘Eligibility’ za kuweza kuchaguliwa kuingia Chuo Kikuu. Hivyo ili uweze kudahiliwa kuendelea na elimu ya juu ni lazima uwe na vigezo. Kuhusu mfumo sidhani kama ulikuwa na matatizo yeyote,” alisema Dk Maronga
 

Kauli za Wanafunzi
Wanafunzi waliozungumza na gazeti hili kuhusu mfumo huo wa udahili wa mtandao, walisema una usumbufu kutokana na wengi kutokujua kuutumia.
 

Frank Mabagala aliyehitimu Shule ya Sekondari Pugu Jijini Dar es Salaam, alisema wanafunzi walio wengi wameshindwa kuutumia mfumo huo kwani una mambo mengi ya kufanya.
 

“Nilijaza fomu vizuri tu, lakini sikuwa najua kama kuna wakati nilitakiwa kwenda kuangalia ‘Eligibility’ hadi nilipoambiwa na rafiki yangu kwenda kuangalia ‘Eligibility’ na kukuta kuna nafasi imeandikwa ‘NO’ hapana vyuo vyote nilivyochagua,” alisema Mabagala.
 

Alisema hata upatikanaji wa vocha za TCU bado zilikuwa tatizo, kutokana na kupatikana sehemu moja tu ya Benki ya NBC. Hivyo kwa watu wanaoishi pembezoni mwa benki hiyo kuwawia vigumu kupata huduma hiyo kwa haraka.
 

“Mfano mimi ninaishi Tegeta lakini nilikwenda benki pale Tegeta nikakuta zimekwisha,.Nikaenda Mliman City nako nikakuta vivyo hivyo hadi nilipokwenda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ndipo nikazikuta nako kulikuwa na foleni,” alisema Mabagala na kuongeza:
 

“Kama Dar es Salaam upatikanaji wa vocha inakuwa hivi, je, kwa wanaoishi pembezoni mwa mkoa ambako benki kuifikia ni kazi, watu wa aina hii watakuwa wamepata usumbufu mfano ni rafiki zangu watatu wa mkoa walinitumia fedha huku ili niwanunulie vocha na kuwatumia.”
 

Naye Zahora Miraji aliyehitimu kidato cha sita Shule ya Seminari ya Ridwaa jijini humo, alisema alijaza fomu kulingana na maelekezo yalivyokuwa, lakini katika hali ya kushangaza amekuta kile alichokijaza kimebadilishwa.
 

Miraji alisema, katika chaguo la vyuo, chaguo la kwanza na pili aliomba Chuo cha Mkwawa, la tatu na nne aliomba Chuo cha Dodoma na chaguo lake la tano aliomba Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, lakini alipokwenda kuangalia kwa mara ya mwisho akakuta amebadilishiwa.
 

“Nilijaza vizuri na nilipokuwa nikifungua kuona kinachoendelea ninakuta bado iko katoka ‘mchakato’ lakini nilipokwenda tena kuangalia nikakuta vyuo nilivyoomba vya Mkwawa, Dodoma na Dar es Salaam vyote vimebadilishwa sasa sikujua tatizo ni nini,” alisema Miraji na kuongeza:
 

“Nilikuta chagua la kwanza na la pili nimeandikiwa chuo cha Jordan na hata sijui kipo wapi na chaguo la tatu hadi la tano Chuo cha Usafirishaji Marrine. Nilikwenda TCU kuwaeleza kilichotokea wakanipa fomu nikaijaza kuonyesha tatizo langu sasa sijui kama watalishughulikia au la.”
 

Kauli ya Chuo
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekeza Mukandala, alisema mfumo huu ni mzuri kutokana na kuepusha usumbufu uliokuwepo awali.
 

Alisema kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ni lazima nchi ibadilike, kwa kuwa mfumo wa kujaza kwenye makaratasi ilikuwa inaongeza ufanisi.
 

“Kama kuna matatizo hakuna budi kuufanyia marekebisho ili uweze kutoa huduma kwa ufanisi lakini kweli ni mzuri na siyo mwisho, kwani TCU wataufungua tena na wanafunzi wataweza kuomba tena,” alisema Profesa Mukandala. Chanzo: mwananchi
 ....................................................................
LEO WILAYANI RUNGWE KATIKA MJI WA TTKUYU MVUA YAENDELEA KWA SIKU YA SITA BILA YA KUONA JUA
LEO MVUA NA BARIDI NA UKUNGU IMEZIDI
 
WENGINE WAMEKWAMA

IMEHARIBIKA....


BIASHARA IKO PALEPALE ILA ELIMU YA KUJIKINGA NA BARIDI NA MVUA INAHITAJIKA

MATENGENEZO YA BARABARA YA LAMI KUTOKA TUKUYU KWENDA BUSOKELO  YAMESIMAMA KUTOKANA NA MVUA ZINAZOENDELEA KUNYESHA

USAFIRI WA LEO KUTOKA LWANGWA  HADI TUKUYU
ANGEJUA ANAKWENDA WAPI...




No comments: