Wednesday, September 25, 2013

WAENDESHA BODA BODA 300 WILAYANI RUNGWE WATUNUKIWA VYETI VYA UDEREVA PAMOJA NA LESENI.

Baadhi ya Pikipiki zinazoendeshwa na vijana Wilayani Rungwe waliotunukiwa vyeti na Leseni na Mkuu wa Wilaya hiyo Crispin Meela baada ya kumaliza mafunzo.
Afisa Biashara wa Wilaya ya Rungwe, Prince Mwakibete akisoma majina ya madereva wanaostahili kutunukiwa vyeti na mkuu wa Wilaya ya Rungwe Crispin Meela.  
Dereva wa Bodaboda Baraka Mwasile akisoma risala kwa niaba ya madereva wenzie kabla ya kuanza kwa zoezi la kuwatunuku Vyeti na Leseni zao.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe Noel Mahyenga akizungumza na Madereva wa bodaboda na kumkaribisha Mkuu wa Wilaya ili akabidhi vyeti na Leseni.
Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Crispini Meela akizungumza na Madereva wa bodaboda kabla ya kuanza kwa zoezi la kuwatunuku vyeti na leseni za kuendeshea pikipiki kwa vijana 300 wa Wilaya hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Rungwe akimkabidhi cheti dereva wa bodaboda kwa niaba ya wenzie 300 katika hafla iliyofanyika nje ya jengo la ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe Tukuyu mjini.
Baadhi ya madereva wa Bodaboda wakifuatilia kwa makini zoezi la kutunuku vyeti lililokuwa likifanywa na Mkuu wa Wilaya ya Rungwe.


IMEELEZWA kuwa mafanikio ya jambo lolote duniani  linatokana na kuwaelewesha vijana kwa kuwa ndilo kundi kubwa ambalo likisahaulika ni rahisi kupata matokeo tofauti na matarajio.
Hayo yalibainishwa jana na Mkuu wa Wilaya Rungwe Crispin Meela wakati wa Zoezi la kuwatunuku Vyeti na Leseni za kuendeshea pikipiki maarufu kwa jina la Bodaboda vijana 300 wa Wilaya ya Rungwe katika Hafla iliyofanyika katika Jengo la Halmashauri Tukuyu Mjini.
Meela alisema baada ya kugundua kuwa vurugu nyingi hutokea kutokana na vijana wengi kutokua kwenye makundi na shughuli maalumu za kufanya akaamua kuandaa mafunzo kwa Madereva wa Bodaboda ili wapate Leseni na vyeti ili wajue sheria za barabarani.
Alisema  baada ya kupatiwa mafunzo vijana hao tayari ni kundi maalumu ambalo limeshatambuliwa na ni rahisi kulisaidia kwa kuwaanzishia miradi mbali mbali itakayowasaidia kuepukana na vitendo viovu hasa vurugu zinazotokana na Siasa.
Alisema  kwa kuanzia atahakikisha Asilimia tano za Makusanyo ya mapato ya Halmashauri kwa ajili ya Mfuko wa Vijana zitasaidia kuanzisha Sacoss ambayo  kabla ya hapo watapatiwa elimu juu ya uendeshaji wake ikiwa ni pamoja na kuchagua viongozi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe,Noel Mahyenga alisema mradi wa Boda boda ni kichocheo kikubwa cha Wilaya hiyo baada ya vijana wengi kujishughulisha na kuwa tayari kuchangia shughuli za maendeleo ndani ya Wilaya.
Aliongeza kuwa tayari Halmashauri imeshapata kundi la Vijana ambalo limejikusanya pamoja hivyo itarahisisha kuwawezesha na kuwapatia msaada kutokana na kuachana na kazi zisizo rasmi.

 

 ..........................................

MASHINDANO YA NGOMA ZA ASILI NA SAFARI LAGER YAFANA MBEYA.

Mkuu wa Matukio wa kampuni ya bia (TBL) kanda ya Mbeya, Geophery Mwangungulu akimkaribisha mgeni rasmi wa mashindano ya ngoma za asili ambaye ni Kaimu Katibu Tawala wa mkoa wa Mbeya, Leonard Magacha katika kinyanyang'anyiro hicho.
Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Mbeya Leonard Magacha akisaini katika kitabu cha wageni baada ya kuwasili katika viwanja vya TIA kushiriki mashindano ya ngoma za asili. 
Baadhi ya viongozi pamoja na waendesha sherehe ambao ni watangazaji wa redio ya bomba fm wakiandaa utaratibu kabla ya kuanza kwa kinyanyang'anyiro.
Mkuu wa matukio Geophrey Mwangunguru akizungumza na wananchi waliofurika kushuhudia mashindano hayo.
Mgeni rasmi Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya akizungumza na mamia ya Wananchi na washiriki wa Mashindano ya ngoma za asili. 
Baadhi ya Watumishi wa TBL pamoja na viongozi mbali mbali wakifuatilia kwa makini burudani zilizokuwa zikiendelea kutoka kwa washiriki.
Majaji wakifuatilia kwa makini Washiriki kama wanafuata vigezo na masharti ya mashindano na kuchukua alama.
Mkuu wa matukio akiwa ameshika kikombe atakachojishindia mshindi wa kwanza katika kucheza na kuimba ngoma za asili.
Mmoja wa Majaji Nimwindael Mjema akisoma washindi wa shindano la ngoma za asili kuanzia nafasi ya 20 hadi ya 4 ambao waliambulia kifuta jasho cha shilingi 50000 kila kundi.

Baadhi ya vikundi vya ngoma za asili wakiwa wamekaa wakipewa maelekezo mbali mbali kabla ya kuanza kwa mashindano
Ngoma ya Mbeta kabila la Wasafwa wakiwajibika uwanjani.
Wananchi mbali mbali wakifuatilia mashindano hayo
Mzee wa mila ambaye pia ni kiongozi wa kikundi cha ngoma cha Kasanga kutoka Tukuyu Wilayani Rungwe akiwa ameshikilia kombe na fedha taslimu shilingi Milion Moja baada ya kuibuka washindi wa kwanza wakicheza ngoma yao aina ya Ling'oma.


WANANCHI wameaswa kupenda utamaduni wa Asili hususani ngoma za Makabila ili kuenzi mila na desturi zilizoachwa na mababu  tangu zamani na siyo kuegemea katika nyimbo za kizazi kipya.
Mwito huo ume na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya, Leonard Magacha wakati akifungua mashindano ya Ngoma za Asili yaliyofanyika katika Viwanja vya Chuo cha Uhasibu(TIA) Jijini hapa.
Magacha amesema mashindano ya ngoma za asili yatasaidia kuamsha ari ya kupenda utamaduni wa Mtanzania kwa kuenzi Mila na Desturi zilizoachwa na waliotanguliatangu zamani kabla ya sayansi na teknolojia ambapo vifaa vya asili vilitumika.
Ameongeza kuwa kupitia mashindano hayo itakuwa chachu ya kufufua utamaduni vijijini ikiwa ni pamoja na kupima utendaji kazi wa Maafisa utamaduni wa Wilaya kwa kuhamasisha na kuwafundisha wananchi kuzipenda ngoma za asili.
Kwa upande wake Afisa Michezo na Utamaduni wa Mkoa wa Mbeya, George Mbigima, amesema kama Mkoa utandaa mashindano makubwa mwakani ambayo yataanzia kwenye ngazi ya Kijiji, kata, Wilaya na hatimaye kumpata mshindi wa Mkoa.
Naye Mkuu wa Matukio wa kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kanda ya Mbeya, Geophrey Mwangungulu ambao ndiyo waandaaji wa Mashindano hayo amesema lengo la kuandaa tukio hilo ni kuhamasisha wananchi kupenda ngoma za asili pamoja na utamaduni.
Amesema jumla ya vikundi 26 vilijitokeza kushiriki mashindano hayo kutoka katika Wilaya za Mbeya, Rungwe, Kyela,Mbozi Njombe na Iringa ambapo katika Mashindano hayo Mshindi wa Kwanza aliibuka na kitita cha fedha taslimu Milion moja na Kikombe.
Mshindi wa pili aliibuka na shilingi laki tano huku mshindi wa Tatu akiondoka na shilingi laki mbili na washiriki wengine wakiambulia kifuta jasho cha shilingi 50,000/= kwa kila kundi.
Katika mashindano hayo yaliyokuwa kivutio kwa mamia ya Wakazi wa Mbeya kikundi cha ngoma cha Kasanga maarufu kwa Ing’oma kutoka Wilayani Rungwe ndiyo walioibuka kidedea katika kinyang’anyiro hicho.
Nafasi ya pili ilienda kwa kikundi cha ngoma za asili cha Lipango kutoka Isansa Wilayani Mbozi na Nafasi ya Tatu ikinyakuliwa na Kikundi cha Mbeta kutoka Isyesye Jijini Mbeya.
 
picha na Jem
Post a Comment