Sunday, November 10, 2013

Kenya yaiunga mkono Tanzania Afrika Mashariki

131110120158_amina_mohamed_304x171_bbc_nocredit_860b3.jpg
Amina Mohamed,waziri wa mambo ya nje wa Kenya

Kenya imekuwa nchi ya kwanza kutoka Jumuia ya Afrika Mashariki kuipongeza Tanzania kwa hatua yake ya kutangaza bayana kwamba haiko tayari kutoka katika jumuiya hiyo kama ilivyodhaniwa.
Wasiwasi kuwa Tanzania ingejitoa kutoka jumuia ya Afrika Mashariki ulitokana na hali iliyojitokeza kwa baadhi ya nchi za jumuia hiyo kuendesha mikutano yao bila kuishirikisha Tanzania na Burundi.
Baadhi ya wanasiasa na wananchi nchini Tanzania walitaka nchi yao iachane na jumuia hiyo wakizishutumu Kenya, Rwanda na Uganda kuitenga Tanzania hata katika mikutano ya masuala yaliyohitaji maamuzi ya jumuia.

Kufuatia mfarakano huo, ulionekana kutishia uhai wa Jumuia ya Afrika Mashariki, Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, wiki hii alilihutubia bunge la Muungano wa Tanzania mjini Dodoma, katikati ya nchi na kutangaza bayana kuwa Tanzania haitatoka katika jumuiya ya Afrika Mashariki, kwani imefanya kazi kubwa kuifufua na kuiunda upya baada ya kusambaratika mwaka 1977.
Kwa upande wake, Kenya moja ya nchi waanzilishi wa Jumuia ya Afrika Mashariki na ambayo ilishutumiwa kushiriki kuibagua Tanzania, imemtuma waziri wake wa mambo ya nje, Amina Mohammed kwenda Tanzania na kuwa na mazungumzo na waziri mwenzie wa mambo ya nje Bernard Membe kuhusu mfarakano huo na nia ya kuimarisha zaidi uhusiano wa nchi mbili hizo.
Katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Jumapili, waziri Amina Mohammed, amesema Kenya inaunga mkono hotuba ya Rais Jakaya Kikwete, kuhusu uamuzi wake wa kutojitoa katika Jumuia ya Afrika Mashariki, huku akisisitiza kuwa bila Tanzania hakuna Afrika Mashariki na bila Afrika Mashariki hakuna Tanzania.

"Kama unavyojua Kenya na Tanzania tumekuwa tukiijenga jumuiya ya Afrika Mashariki kwa muda mrefu sana, tuko na mafanikio mengi sana, kuna mambo mengi tumeyafanya, kuna njia ndefu imebakia kuna mambo mengi yasiyoweza kupimwa kati ya nchi hizi. Na tuna tumaini kwamba tutaendelea kuijenga Afrika Mashriki kwa nguvu zote na tutawasiliana na watu wetu kwa sababu tunataka watu wetu waishi vema na wawe majirani wazuri na waendelee . Kwa Tunataka uchumi wetu uende vizuri. Kwa hiyo tutaendelea kushirikiana, sisi ni wale wa kwanza tuliokuwa pale kwa hiyo tunataka tufanye kile tunachoweza kuendeleza Afrika Mashariki..... Lakini tumefurahia sana sana hotuba ya Rais aliyotoa pale bungeni na tunawashukuru pia Watanzania kumuunga mkono."
Uhusiano wa Kenya na Tanzania ni wa kindugu

Pia waziri Amina amesisitiza kuwa hakuna namna ambavyo Tanzania na Kenya zitatenganishwa, kwa namna ambavyo zimejenga maingiliano makubwa ya kijamii na kiuchumi, huku akiomba Tanzania kusaidia kusukuma ombi la Kenya la kutaka kesi ianyomkabili Rais wake, Uhuru Kenyatta iahirishwe kwa mwaka mmoja zaidi ili kumpa fursa ya kutekeleza majukumu yake ya kitaifa.
Kwa upande wake waziri wa mambo ya nje wa Tanzania, Benard Membe amesema serikali yake imefurahi kuona Kenya imekuwa nchi ya kwanza kuipongeza Tanzania kwa kuinusuru jumuia ya Afrika Mashariki kama ilivyokuwa mwanzoni na kujenga jumuiya ya watu na si ya viongozi, na kuahidi kushirikiana na Kenya katika masuala mbalimbali likiwemo la kutaka kesi inayomkabili Rais Uhuru Kenyatta katika mahakama ya ICC iahirishwe kwa mwaka mmoja zaidi.

Waziri Membe amesema waziri mwenzake Amina kutoka Kenya amesema hotuba ya Rais Kikwete imewazindua kwani hawakujua kuwa baadhi ya yale waliyokuwa wakiyafanya yalikuwa ni kukiuka taratibu za Jumuia ya Afrika Mashariki na kuahidi kuwa Kenya itashirikiana kikamilifu na nchi waanzilishi halisi wa Jumuia ya Afrika Mashariki.

Katika kuonyesha nia thabiti ya kutotoka katika Jumuia ya Afrika Mashariki, Rais Kikwete katika hotuba yake aliyoitoa bungeni, alisema "Tanzania ni mwanachama mvumilivu, mtiifu na mwaminifu na tunatimiza wajibu wetu kwa jumuia na kuhusika kikamilifu katika ujenzi wake."alisema.
Rais Kikwete alitumia muda mrefu katika hotuba hiyo kuchambua masuala mbalimbali ya msingi ya uhai wa jumuia hiyo huku akisema ameshangazwa na nchi za Kenya, Uganda na Rwanda kuzitenga Tanzania na Burundi.
...........................................................

TANZANIA HORTICULTURE ASSOCIATION (TAHA) YATOA SOMO KWA VIONGOZI WA KANDA YA NYANDA ZA JUU KUSINI.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbasi Kandoro  ambaye alikuwa mwenyekiti katika mkutano huo aliwataka viongozi wenzie kuacha porojo na kutekeleza Agizo la Raisi Kikwete kwa vitendo kuhusu kutumia fursa ya Uwanja wa Ndege wa Songwe katika kilimo cha mazao ya m,atunda, maua na mboga mboga.
 Mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya TAHA, Jackline Mkindi wakati akizungumza katika Mkutano wa wadau wa kilimo cha mazao ya mboga mboga, maua na matunda kilichofanyika  katika ukumbi wa jengo la ukaguzi jijini Mbeya.
Wakuu wa mikoa  wakiwa makini kumsikiliza  Mkurugenzi mtendaji wa taasisiya TAHA 
Makatibu tawala, Wakuu wa Wilaya na wataalamu wa Kilimo wakimsikiliza Mkurugenzi mtendaji wa TAHA katika mkutano huo




Watanzania wametakiwa kubadilika kutoka kulima kilimo cha mazoea na kujikita katika uzalishaji unaolenga mahitaji ya soko la nje ili kuboresha vipato na maisha yao kutokana na uwepo wa fursa.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya TAHA, Jackline Mkindi wakati akizungumza katika Mkutano wa wadau wa kilimo cha mazao ya mboga mboga, maua na matunda kilichofanyika  katika ukumbi wa jengo la ukaguzi jijini Mbeya.
Mkindi amesema wananchi wengi hawajui kuwa kilimo hicho ni rahisi na kinaweza kubadilisha maisha yao kwa muda mfupi tofauti na mazao mengine ambayo yanachukua muda mrefu hadi kuvunwa kwake.
Amesema ni bora wakajikita katika uzalishaji wa mazao hayo wakilenga mahitaji ya soko la nje kwa kuzingatia uwepo wa fursa ya uwanja wa kimataifa wa Songwe kwa ajili ya kusafirisha mazao hayo hadi Sokoni.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbasi Kandoro aliwataka viongozi wenzie kuacha porojo na kutekeleza Agizo la Raisi Kikwete kwa vitendo kuhusu kutumia fursa ya Uwanja wa Ndege wa Songwe katika kilimo cha mazao ya m,atunda, maua na mboga mboga.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Wakuu wa Mikoa wa Mbeya, Njombe na Iringa pamoja na makatibu tawala, Wakuu wa Wilaya na wataalamu wa Kilimo cha mazao hayo kutokana na kuwa na mpango wa pamoja katika kilimo hicho.

Na Mbeya yetu

No comments: