Tuesday, November 5, 2013

‘Kuumizwa Dk Mvungi pigo kubwa kwa Tume ya Katiba’

ibada_d6125.jpg
Wajumbe wa Tume ya Katiba, Dk Salim Ahmed Salim (kushoto), Joseph Warioba, Joseph Butiku (kulia) na Profesa Paramagamba Kubudi (nyuma kushoto) wakiwa katika ibada ya kumwombea afya njema Dk Sengondo Mvungi katika Kanisa la Mtakatifu Joseph Dar es Salaam jana. Picha na Venance Nestory

Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Agustino Ramadhan alisema kuwa kuumizwa kwa Dk Sengondo Mvungi ni pigo kubwa kwa tume yao wakati huu wa maandalizi ya rasimu ya pili ya Katiba.
Jaji Ramadhan alisema kuwa, Dk Mvungi amekumbwa na matatizo katika kipindi ambacho wanajiandaa kuandika rasimu ya pili.

Alisema kwa sasa wamekamilisha kazi ya kuandaa majumuisho ya maoni kutoka katika mabaraza ya katiba ya nchi nzima na kazi iliyobaki ni kuandika rasimu ya pili.
Alisema Dk Mvungi ni mtu muhimu kwenye kazi yao, kwani amebobea katika masuala ya katiba.
"Tulikuwa tunamtegemea atusaidie sana katika kuandaa rasimu ile ya pili, kwa kweli kuumizwa kwake ni pigo kwa Tume," aliongeza Jaji Ramadhan.

Katika hatua nyingine, hali ya Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Mvungi aliyeruhiwa na majambazi nyumbani kwake Jumamosi iliyopita, inaendelea vizuri.
Akizungumza na gazeti hili, mtoto wa mjumbe huyo, Deogratias Mwarabu alisema hali ya Dk Mvungi inaendelea vizuri na madaktari wamefanikiwa kudhibiti matatizo hayo mawili.
Madaktari wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu (Moi) wamezuia watu kumuona mjumbe huyo.

Aidha, jana kulikuwa kuna Sala Maalumu ya kumwombea iliyofanyika katika Kanisa la St Joseph jijini Dar es Salaam.
Chanzo:Mwananchi

No comments: