Monday, November 4, 2013

MAKAMU WA RAIS DKT. BILAL AMJULIA HALI DKT. SENGONDO MVUNGI ALIYELAZWA MUHIMBILI


Mvungi 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akimsikiliza Dkt. Mugisha Clement, aliyekuwa akimpa maelezo kuhusu alivyompokea Mjumbe wa Tume ya Katiba, Dkt. Sengondo Mvungi, aliyelazwa  katika Kitengo cha Uangalizi Maalum (ICU) MOI katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, wakati alipokwenda kumjulia hali, kufuatia kujeruhiwa na majambazi usiku wa kuamkia jumapili huko nyumbani kwake maeneo ya Kibamba.
 .......................................................................

Bobby Williamson kocha mpya Simba SC

Bobby_3286b.jpg

Maofisa wa ngazi ya juu wa Simba wameanza mazungumzo na kocha Bobby Williamson wa Gor Mahia ya Kenya ili achukue mikoba ya Abdalla Kibadeni.

SIMBA itaanza mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara, Januari 26 mwakani dhidi ya Rhino Rangers kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ikiwa na kocha mpya, Mwanaspoti linaweza kuthibitisha.
Maofisa wa ngazi ya juu wa Simba wameanza mazungumzo na kocha Bobby Williamson wa Gor Mahia ya Kenya ili achukue mikoba ya Abdalla Kibadeni.
Williamson (52), ni straika wa zamani wa West Bromwich Albion na katika mechi 53 aliyoichezea timu hiyo alifunga mabao 11.

Williamson, ambaye ni raia wa Scotland alijiunga na Gor Mahia msimu huu na tayari ameipa ubingwa wa Ligi Kuu Kenya ikiwa ni miaka 18 tangu timu hiyo itwae ubingwa wa Kenya mwaka 1995.
Williamson, ambaye alikuwa kocha wa timu ya taifa ya Uganda na kuipa ubingwa wa Kombe la Chalenji mara nne, ni kocha anayesifika kutokana na kufundisha soka la kisasa kwa timu kushambulia na kukaba kwa pamoja.

Habari kutoka makao makuu ya Simba, barabara ya Msimbazi jijini Dar es Salaam zinasema kuwa maofisa kadhaa wa klabu hiyo wameanza mazungumzo na kocha huyo.
Habari hizo zinasema kuwa Simba ina asilimia kubwa ya kumnasa kocha huyo kwa sababu alikuwa na mkataba wa mwaka mmoja tu Gor Mahia na kwamba analipwa kidogo.

Simba imeamua kuingiza nguvu zake kwa kocha huyo baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa timu hiyo ambayo inashika nafasi ya nne katika ligi, lakini kubwa zaidi ni kutokana na benchi la ufundi kushindwa kudhibiti nidhamu kwa wachezaji na kucheza mpira wa hovyo uwanjani.
Hakuna kiongozi wa Simba aliyekuwa tayari kulizungumzia hilo, licha ya karibu wote kukiri kuwa hawaridhishwi na jinsi timu hiyo inavyocheza.

Williamson aliteuliwa na Shirikisho la Soka Uganda (Fufa) kuwa kocha wa timu ya taifa ya nchi hiyo 'The Cranes' Agosti 19, 2008 akichukua nafasi ya Csaba Laszlo, aliyekuwa amejiuzulu Julai 2008 baada ya kuteuliwa kuwa kocha wa klabu ya Hearts inayoshiriki Ligi Kuu Scotland.
Akiwa na kikosi cha Uganda, Williamson ameshinda mataji manne ya Kombe la Chalenji mwaka 2008, 2009, 2011 na 2012.

Uganda nusura itinge katika fainali za Mataifa ya Afrika 2013, lakini ilipoteza mchezo wake wa mwisho wa kufuzu baada ya kupigiana penalti na Zambia.
Hata hivyo, Fufa ilimtimua kazi Williamson Aprili 8, mwaka huu na nafasi yake ikachukuliwa na Kocha wa Serbia Sredojevic Milutin 'Micho', ambaye alikuwa ametimuliwa timu ya taifa ya Rwanda.
Julai 5, mwaka huu, Williamson alijiunga na Gor Mahia ya Kenya akichukua nafasi ya Zdravko Logarusic wa Croatia, ambaye alikuwa amefukuzwa siku tisa za nyuma yaani Juni 25 mwaka huu.

No comments: