Frank Mvungi-Maelezo
Wabunge
wanaowakilisha Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki wamempongeza
Rais Jakaya Kikwete kufuatia hotuba yake aliyoitoa Bungeni Dodoma tarehe
07/11/2013 kuhusu Mustakabali wa Jumuiya Hiyo.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa wabunge hao Mh. Adam Kimbisa wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.
Mh.
Kimbisa amesema wabunge hao wanampongeza Mh. Rais kwa kuchukua fursa ya
kuongea na Watanzania kupitia Bunge na kueleza masuala kadhaa baina ya
Nchi wanachama na hali ya hivi sasa ndani ya Jumuiya.
Akifafanua
zaidi Mh. Kimbisa amesemaMh. Rais amefanya uchambuzi wa kina kuhusu
matatizo yaliyoikumba jumuiya ya Afrika Mashariki kufuatia mikutano
mitatu iliyofanywa na nchi tatu za Kenya,Uganda na Rwanda ikiwatenga
Tanzania na Burundi.
Alieleza
zaidi kuwa wabunge wa bunge hilo wanaungana na Watanzania wengi kuhusu
kuwepo kwa shirikisho la Afrika Mashariki lakini wanataka hatua hiyo
isifanywe haraka bali kwa umakini mkubwa,sera ambayo pia Serikali ya
Tanzania imeipa kipaumbele.
Pia
alisema jambo la msingi ambalo mkataba wa uanzishwaji wa jumuiya umesema
ni kuwa Jumuiya lazima iwe ni ya wananchi kwa manufaa ya wananchi na
isiwe ya viongozi ambapo wananchi watashirikishwa katika kila hatua na
kila ngazi ili waweze kushiriki kikamilifu kwa ajili ya maslahi yao.
Katika
hatua nyingine wabunge hao waliipongeza Serikali kwa hatua iliyochukua
kwa kuwarejesha makwao wahamiaji haramu kutoka Burundi,Rwanda,Uganda,DRC
nchi nyingine ambao walitishia na kuharibu hali ya usalama na
mazingira katika maeneo ya Mikoa ya Kagera,Geita na Kigoma.
Aidha
wabunge hao wameiomba Serikali iendelee kusimamia suala hilo kwani
baadhi ya wahamiaji haramu wameanza kurejea katika maeneo husika na
wananchi wameanza kutoa malalamiko dhidi ya wahamiaji haramu.
No comments:
Post a Comment