.Bunge
limepitisha azimio la kuwataka mawaziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kujipima iwapo
wanatosha kuendelea kuongoza wizara hiyo nyeti.
Azimio
hilo lilipitishwa jana na wabunge kwa kura ya ndiyo bila kupingwa, baada
ya kuhojiwa na Spika wa Bunge Anne Makinda iwapo wanaipokea taarifa ya
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (Laac) iliyowasilishwa na
Mwenyekiti wake Rajabu Mbaruku.
Soma zaidi...
Moja ya
mapendekezo yake ni Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia na manaibu wake,
Aggrey Mwanri na Kassim Majaliwa kujipima kama wanatosha kuendelea
kuongoza wizara hiyo kutokana na kugubikwa na vitendo vya ufisadi.
Kwa
mujibu wa taratibu za Bunge, taarifa ya kamati inapowasilishwa na
kupitishwa pamoja na mapendekezo yake, huwa ni azimio kamili ambapo
Serikali hutakiwa kutoa maelezo ya utekelezaji wake.
Kabla ya
azimio hilo kupitishwa, Mwenyekiti wa Laac, Rajabu Mbaruku alijibu
michango ya wabunge waliochangia katika taarifa ya kamati yake
iliyowasilishwa Ijumaa iliyopita, akiwemo Waziri Ghasia.
Akizungumza
baadaye, Mbaruku alisema hayo ndiyo mapendekezo na Serikali itatakiwa
kuyatolea maelezo ya jinsi yatakavyotekelezwa. "Hata waziri mkuu
nimemtaja kwa jina, na nimesisitiza kama ananisikia kuhusu ofisi yake,"
alisema.
Katika
mchango wake, Waziri Ghasia alijaribu kupangua tuhuma mbalimbali
zilizoelekezwa katika wizara yake ikiwamo kuwapo ufisadi, ubadhirifu na
mtandao wa wizi unaohusisha Hazina, Wizara na Halmashauri.
Ghasia alikiri Halmashauri ya Mbarali ilitumiwa fedha kuliko kiwango kilichoidhinishwa na Bunge na kwamba
suala la
halmashauri mbili za Tanga kupewa zaidi ya Sh2 bilioni haikuwa sahihi
bali yalikuwa ni makosa ya Mkaguzi Mkuu wa Mdhibiti wa Hesabu za
Serikali (CAG).
Kuhusu
ufisadi wa zaidi ya Sh600 milioni zilizotolewa na wafadhili kwa ajili ya
mpango wa maboresho ya Serikali za Mitaa, alisema haamini kama maneno
yaliyonukuliwa na vyombo vya habari kuhusu fedha hizo yalisemwa na
wafadhili.
Wafadhili
wa mradi huo walinukuliwa wakilalamikia ufisadi huo na kudai kwa sasa
hawana la kufanya na wanamwachia Rais, huku wakieleza kushangazwa na
Rais kuteua watu dhaifu kuendesha wizara nyeti kama Tamisemi.
Kuhusu
hilo, Ghasia alisema hadhani maneno hayo ni ya wafadhili akisema ni
majungu, ni maneno ya waandishi kwa sababu huwa wanatafuta mambo
yanayogusa jambo fulani ili kuuza magazeti.Hata hivyo, Ghasia alikiri
kwamba ulifanyika ukaguzi na yalibainika matumizi ambayo hayakufuata
taratibu na kusisitiza kuwa fedha zilizotumika bila kufuata taratibu
zilikuwa Sh444.8 milioni na siyo Sh600 milioni.
Alisema
kuwa tuhuma kwamba anawalinda watuhumiwa wa ufisadi na kuwahamisha wale
wanaotuhumiwa si za kweli kwani wizara imekuwa ikichukua hatua za
kinidhamu dhidi ya watumishi hao na hata kuwafikisha kortini.
Alitolea
mfano wa Halmashauri ya Kishapu ambayo watumishi 14 wamesimamishwa kazi
na masuala yao hivi sasa yanashughulikiwa na ofisi ya Mkurugenzi wa
Mashtaka (DPP) na Ofisi ya Takukuru.
Pamoja na maelezo ya Waziri Ghasia, bado Mwenyekiti wa Kamati alisisitiza kuwapo matatizo makubwa
Tamisemi na ndipo alipowataka Ghasia na Manaibu wake kujipima wenyewe kama bado wanafaa kuongoza wizara hiyo nyeti.
Mwenyekiti huyo alisema si kweli kama alivyosema Waziri Ghasia kuwa hakuna mtandao wa ufisadi na
kusisitiza kuwa fedha zilizopelekwa jijini Tanga hazikurudishwa Hazina na badala yake zilitumiwa na Halmashauri hiyo.
Alisema
kinachoonekana ni kwamba ulikuwapo mpango wa kuzipeleka fedha kwenye
baadhi ya Halmashauri nje ya fedha zilizoidhinishwa lakini baadaye fedha
hurudishwa kwa wanamtandao huo baada ya kutakatishwa.
Mwenyekiti
huyo alisema Halmashauri zinazopelekewa fedha hizo zilizo nje ya
bajeti, hupelekewa fedha hizo kwa malengo ya kuzitakatisha kisha
kuzirejesha Hazina ambapo wahusika hunufaika nazo.
Ijumaa
wakati akiwasilisha taarifa ya kamati, kamati hiyo iliilipua Wizara ya
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ikiituhumu kuwa sehemu
ya mtandao wa ufisadi serikalini.
Alisema
bado kuna ubadhirifu, ufisadi na utovu wa nidhamu wa hali ya juu wa
matumizi ya fedha za umma kutokana na Tamisemi kutosimamia au yenyewe
kuhusika moja kwa moja na ufisadi huo.
Mfano wa
mwaka 2011/2012 ambapo Sh1.6 bilioni zilitumika nje ya bajeti
iliyoidhinishwa katika halmashauri 38 na Sh2.6 bilioni zilihamishwa
kutoka akaunti moja kwenda nyingine bila kurudishwa.Kamati hiyo imebaini
kwamba upo mtindo wa Serikali kutuma kwa Halmashauri kiasi kikubwa cha
fedha kuliko kiasi cha fedha kilichoidhinishwa na Bunge katika fungu
husika wakati wa upitishaji wa bajeti.
Kamati
hiyo imetolea mfano wa Sh2 bilioni zilizotumwa Halmashauri ya Jiji la
Tanga na Sh500 milioni zilizotumwa Halmashauri ya Mji wa Korogwe zikiwa
zaidi ya kiasi kilichokuwa kimeidhinishwa na Bunge.
"Kitendo
hiki ambacho kinafanyika kwa ushirikiano wa hali ya juu wa
Hazina,Tamisemi na Halmashauri kinaashiria kuwapo mtandao wa kutisha wa
kifisadi baina ya mamlaka hizo," alisema.
Kamati
hiyo imeituhumu pia Tamisemi inayoongozwa na Waziri Hawa Ghasia,
kuwahamisha haraka watumishi wanaotuhumiwa kufanya ubadhirifu kutoka
halmashauri moja kwenda nyingine.
"Kamati
imebaini kwamba Tamisemi imekuwa ikitumia mtindo huu kuwalinda watumishi
mafisadi ndani ya halmashauri na kuifanya kamati iamini Tamisemi ni
sehemu ya mtandao huu," imesema.
Mwenyekiti
wa kamati hiyo alisema kwa makusudi mazima, Tamisemi imekuwa ikieneza
saratani hiyo ya ufisadi kwenye halmashauri nyingi iwezekanavyo na
kuitaka Serikali kuachana na mtindo huo.
Ubadhirifu Wakurugenzi 70
Itakumbukwa
Agosti 19 mwaka huu, Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC),
ilitoa taarifa yake baada ya kubaini kuwepo kwa mtandao wa ufisadi
unaoshirikisha Wakurugenzi 70 wa Halmashauri mbalimbali hapa nchini
ambao wanashirikiana na baadhi ya Watendaji wa Ofisi ya Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Kitengo cha Hazina.
Baadhi ya halmashauri hizo ni pamoja na Wilaya ya Monduli, Arusha, Mwanza, Mbeya na Ilala.
Ilielezwa kuwa Tanzania Bara ina halmashauri 134, kwa hiyo ina maana zaidi ya nusu ya wakurugenzi wanajihusisha na mambo hayo.
"Baadhi ya wakurugenzi hao walihamishwa kwenye vituo vyao vya kazi kutokana na kashfa ya matumizi mabaya
ya fedha
za Serikali, lakini bado wanajihusisha na mambo haya," alisema Mbarouk
alipokuwa akiwasilisha taarifa yake kwa waandishi wa habari."Kuna zaidi
ya Wakurugenzi 70 wako kwenye mtandao wa ufisadi kwa kushirikiana na
watendaji wa Hazina na Tamisemi, jambo ambalo limesababisha halmashauri
zao kupata hati chafu kwa miaka mitano mfululizo," alisema Mbarouk.
Aliongeza
wakurugenzi hao wamekuwa wakishirikiana na wahasibu wao katika kutumia
vibaya fedha za Serikali zinazotolewa kwa ajili ya kuendeleza miradi
mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri zao.
Akitolea
mfano wa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Wilson Kabwe ambaye halmashauri
yake ilifanya vibaya katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali (CAG), lakini hajachukuliwa hatua na badala yake
amehamishwa kuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam.
CHANZO MWANANCHI
No comments:
Post a Comment