Sunday, December 8, 2013

Madiba na maisha ya kifamilia

Mandela+Familia+ClipWajukuu wa Mandela wakimshangilia babu yao alipokuwa akitimiza miaka 89, mwaka 2008.
………………………………………………………………
Wakati Nelson Mandela anaongoza Afrika Kusini dhidi ya ubaguzi wa rangi na baadaye kuwa kiongozi maarufu duniani baada ya kutoka jela, inabidi tujiulize ni watu gani ambao walikuwa karibu naye kifamilia, kiroho na kuumia naye na waliomfahamu zaidi ya wote?

Baba yake Mandela alimwacha akiwa na miaka tisa baada ya kufariki mwaka 1927, baadaye alilelewa na Chifu Jongintaba kabla ya kutoroka baada ya kutaka kuozwa akiwa bado mdogo.
Wakati anaanzisha mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi na kupigania usawa, ilikuwa dhahiri Mandela alihitaji kuwa na mwanamke mkakamavu na jasiri.

Mandela ameishi na wake watatu katika maisha yake – EvelynMase, Winnie Madikizela na wa mwisho, Graca Machel alimuoa akiwa anatimiza miaka 80.
Mandela amekuwa kipenzi kwa watoto na masuala ya elimu na kwa kudhihirisha hilo aliaanzisha Mfuko maalumu wa elimu kwa ajili ya watoto, ukiwa ni sehemu ya mafanikio katika maisha yake.

Nelson Mandela ni baba wa watoto sita, wanne akiwazaa kwenye ndoa ya kwanza na Evelynna wengine wawili kwa mkewe wa pili, Winnie.
Watoto wa Mandela wamepitia katika kipindi kigumu na wana kitu cha kipekee katika maisha yao, kwani kuna wengine ambao hawakupata kuonana na baba yao maisha yao yote, kwani alikuwa jela katika kipindi cha uhai wao.
Mabinti wa Mandela waliozaliwa kwa mke wa kwanza waliitwa Makazawie.  Mkubwa alikufa miezi tisa baada ya kuzaliwa na mwingine aliyemfuata ilibidi apewe heshima ya jina hilo kwa ajili ya dada yake.

Mwingine, Madiba Thembikile (Thembi) alikufa kwa ajali ya gari mwaka 1969 akiwa na miaka 25. Mandela alikuwa jela kipindi hicho na hakuruhusiwa kuhudhuria mazishi ya mwanawe.
Makgatho alikufa mwaka 2005 baada ya kuugua ugonjwa wa Ukimwi.
Ndio maana Nelson Mandela amekuwa mwanaharakati mkubwa wa mapambano dhidi ya ugonjwa huo na alianzisha kampeni dhidi ya ugonjwa huo aliyoiita 46664 AIDS Campaign, jina likitokana na namba yake akiwa jela.

Mandela na Evelyn walidumu katika ndoa kwa miaka 13 na kuachana mwaka 1957. 
Waliachana kwa sababu mwanamke huyo alikuwa Shahidi wa Yehova na imani yao iliwataka wasishabikie masuala ya siasa. Mwanamke huyo alifariki dunia mwaka 2004.
Mwaka 1958 Mandela alimuoa Winnie Madikizela.  Ingawa sehemu kubwa ya muda wa ndoa yao aliutumia akiwa jela.
Winnie alikuwa mwanamke shupavu kwani naye alikuwa mwanasiasa machachari.
Walifanikiwa kuzaa mabinti wawili Zenani (Zeni) –aliyezaliwa mwaka 1958, na Zindziswa (Zindzi) – aliyezaliwa 1960.

Zeni aliolewa na mtoto wa mfalme, Prince Thumbumuzi Dlamini. Zindzi alijiandikia historia mwaka 1985 pale alipotoa hotuba ya kupinga baba yake kutolewa jela kwa masharti.
Kutokana na tofauti za kisiasa na za kibinafsi, Mandela na Winnie walilazimika kuachana mwaka 1994.  

Mwaka 1988 alipotimiza miaka 80 ya kuzaliwa, Mandela alimuoa Graca Machel (Mjane wa Rais wa Msumbiji, Marehemu Samora Machel ambaye aliyekufa kwenye ajali ya ndege inayodhaniwa ilitunguliwa na Makaburu mwaka 1989.

Nelson Mandela alikuwa akiishi katika nyumba yake iliyoko Qunu. Pamoja na kwamba ana nyumba nyingi sehemu mbalimbali duniani, lakini sehemu aliyoipenda ni kijijini kwao katika jimbo la Transkei.
CHANZO: MWANANCHI

 .................................

India, Ufaransa, Marekani, Canada zaomboleza kipekee

Madiba+Maombolezo+Clip 
Bendera za mataifa mbalimbali zikipepea nusu mlingoti jijini Dar es Salaam kuomboleza kifo cha Madiba. PICHA | FIDELIS FELIX
Pamoja na kutuma salamu za rambirambi kwa familia ya Mandela na wananchi wa Afrika Kusini, viongozi wa mataifa makubwa duniani wameonyesha kuguswa na msiba huo kiasi cha kuomboleza kwa namna tofauti tofauti.
India
Hii inaweza kuwa ni nchi mojawapo ambayo imetangaza siku nyingi zaidi za maombolezo kwa ajili ya kifo cha Nelson Mandela kutoka nje ya Bara la Afrika.
Baada ya kupata taarifa za kifo cha Mandela, Serikali ya India kupitia Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Manmohan Singh aliwatangazia siku tano za maombelezo na kuamuru bendera zipeperushwe nusu mlingoti katika kipindi hicho cha maombolezo.
Sambamba na hilo, Singh  alimwelezea  namna kiongozi huyo wa Afrika alivyokuwa shujaa katika kupinga mfumo wa kibaguzi.
Ufaransa
Kuonyesha kuwa taifa hili pia limeguswa kwa kiasi kikubwa na msiba huu, jengo refu zaidi mjini Paris la Eiffel Tower liliwashwa taa zenye rangi zilizopo kwenye Bendera ya Afrika Kusini.
Picha zilizopigwa katika jengo hilo mpaka siku ya jana, linaionyesha likiwa limenakshiwa na taa zenye rangi tano  za bendera hiyo zikiwemo nyekundu, kijani, nyeusi, njano na nyeupe.
Marekani
Taifa hili lenye nguvu duniani limeonyesha heshima kubwa kwa Nelson Mandela kwa kupeperusha bendera zake nusu mlingoti nchi nzima na kuweka siku tatu za maombolezo.
Kana kwamba hiyo haitoshi taa zenye rangi ya Bendera ya Afrika Kusini zilionekana kung’arisha jengo la Empire state lililopo NewYork na Hoteli ya Omni iliyopo Dallas.
Mjini Washington jengo la Ubalozi wa Afrika Kusini lilitawaliwa na taa hizo pamoja na bendera za nchi hiyo hali iliyosababisha mwonekano wa eneo hilo kubadilika kabisa.
Pia  kiongozi wa taifa hilo Rais Barack Obama alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Graca Machel ambaye ni mjane wa Mandela.
Taarifa kutoka Ikulu ya Marekani ilisema kuwa Obama alimpigia simu mama Machel kwa lengo la kumtumia salama za rambirambi.
Canada
Kwa mujibu wa taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari nchini Canada, Waziri Mkuu Stephen Harper amewaalika mawaziri wakuu wengine wastaafu wa nchi hiyo kuungana naye kuelekea Afrika Kusini kwa ajili ya mazishi ya Nelson Mandela.
Australia na Uingereza
Kama ilivyo kwa nchi nyingine, mataifa haya pia yalitangaza siku za maombolezo sanjari na kupeperusha bendera zake nusu mlingoti kuashiria maombolezo ya kifo cha kiongozi shujaa na mahiri barani Afrika, hayati Nelson Mandela.

No comments: