Saturday, December 7, 2013

Mazishi ya Mandela kuvunja rekodi

mandela 
Afrika na dunia inatarajiwa kushuhudia kitu kipya katika maziko ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela (95) aliyefariki dunia juzi, baada ya kuugua kwa zaidi ya miezi sita.
 
Serikali ya Afrika Kusini imesema kiongozi huyo ambaye atazikwa Desemba 15, imeandaa mazishi ya kihistoria yanayosemekana yatazidi yale ya Papa John 11.
Matukio ya shughuli mbalimbali zinazohusu mipango ya maziko ya kiongozi huyo maarufu yanatarajiwa kushuhudiwa sehemu mbalimbali duniani, tofauti na tukio jingine lililowahi kutokea barani Afrika mbali na kombe la dunia.

Rais Jacob Zuma alisema jana kwamba “Mpendwa wetu Madiba atazikwa kwa heshima zote za Serikali. Nimeagiza bendera zote za Afrika Kusini zipepee nusu mlingoti na hiyo itaendelea hivyo hadi tutakapokamilisha mazishi yake.

Mazishi ya Mandela yanalinganishwa na yale ya Papa John Paul II mwaka 2005, ambayo yalihudhuriwa na wafalme watano, malkia sita wa falme mbalimbali na marais wapatao 70 na mawaziri kadhaa, wakiwamo wafuasi wake zaidi ya milioni mbili. Yanakadiriwa pia kulingana na maziko ya Winston Churchil aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza mwaka 1965.
Marais wote wa Marekani walio hai wanatarajiwa kuhudhuria mazishi hayo iwapo afya zao zitawaruhusu kusafiri, pamoja na Prince Charles wa Uingereza na hata Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe. Pia watu maarufu wenye urafiki wa karibu na Mandela akiwamo msanii Oprah Winfrey wameshathibitisha kuhudhuria.

Changamoto la kiusalama
Kutokana na idadi kubwa ya wakuu wa nchi na watu maarufu duniani wanaotarajiwa kufika Afrika Kusini, suala la usalama limeelezewa kuwa changamoto mpya kwa vyombo vya usalama nchini humo.
Afrika Kusini imekuwa moja ya nchi zinazokabiliwa na matukio ya uporaji na mauaji yanayotokana na idadi kubwa ya wahalifu, wengi wao wakidaiwa kuwa wahamiaji haramu.
“Huyu ni shujaa wa dunia. Tutafanya mipango ya mazishi makubwa ambayo hayajawahi kushuhudiwa. Nadhani kila nchi itakuwa imeandaa utaratibu wake wa namna ya kushiriki,” alisema mmoja wa wanadiplomasia wa Afrika Kusini ambaye hakutaka kutajwa jina lake.
Siku 11 za maombolezo
Serikali ya Afrika Kusini, kwa mujibu wa gazeti la The Guardian tayari imeweka wazi ratiba ya siku 11 za maombolezo tangu alipofariki dunia juzi jioni. Japokuwa ratiba hiyo ilishaandaliwa karibu mwaka mmoja uliopita na kupitiwa na kufanyiwa maboresho katika baadhi ya maeneo, inaonyesha namna maofisa wa Serikali ya Afrika Kusini walivyolipa uzito suala hilo na kulifanya kuwa tukio la kukumbukwa katika historia.
“Mwili wake ulipelekwa kwenye nyumba ya kuhifadhia maiti kwa ulinzi wa polisi jana, na tayari mipango yote ya kurusha moja kwa moja kupitia shughuli hii kupitia televisheni imekamilika,” inasomeka taarifa ya Serikali.

Taarifa ya Serikali iliyotolewa jana pia ilieleza kwamba tayari vitabu kwa ajili ya rambirambi vimeshaandaliwa katika ofisi zote za ubalozi, kwenye ofisi za Nelson Mandela Foundation, majengo yote ya Serikali na kwenye sehemu ya kumbukumbu ya Mandela huko Soweto.
Katika siku ya tatu, yaani leo wanadiplomasia wa nchi mbalimbali waliopo nchini humo watapewa taarifa mjini Pretoria kuhusu utaratibu wa mazishi ya Mandela na katika siku ya nne, yaani kesho watu mbalimbali mashuhuri wataruhusiwa kuitembelea familia ya Mandela.
Katika siku ya tano na ya sita kutakuwa na sala maalumu ya kumbukumbu ya Mandela itakayohudhuriwa na watu mbalimbali na viongozi wa makundi yote ya kijamii ambapo mwili wa kiongozi huyo mwenye historia ya kipekee duniani pia utawekwa mbele ya hadhira.
Tukio hilo litahudhuriwa pia na Rais Jacob Zuma na zitawekwa ‘skrini’ za televisheni katika baadhi ya kumbi za manispaa na viwanja vya wazi huko Soweto, Cape Town na maeneo mengine kwa ajili ya kuwezesha watu wengi kushuhudia shughuli zote za mazishi.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, siku ya nane mwili wa Mandela utawekwa kwenye jengo la Serikali mjini Pretoria kwa siku tatu mfululizo, ili kutoa fursa kwa wananchi kuuaga.
“Mwili huo utawekwa katika eneo hilo kuanzia asubuhi hadi jioni kwa siku zote tatu ukiwa ndani ya jeneza la kioo ili kuruhusu watu kuuona, kisha utaondolewa kwa ajili ya kuandaliwa kwa siku inayofuata…

Katika siku ya tisa, Jeshi la Afrika Kusini litaendelea kusimamia na kutoa heshima za mwisho na kufanya maandalizi ya mazishi rasmi ya kitaifa kwenye jengo la Union Buildings ambapo Mandela aliapishwa rasmi kuwa rais wa kwanza mweusi aliyechaguliwa kidemokrasia mwaka 1994.
Pia shughuli ya kuwapokea wakuu wa nchi mbalimbali watakaoshiriki katika maziko hayo itakuwa ikiendelea.

Katika siku ya 10 baadhi ya mitaa itafungwa ikiwa ni hatua ya kuimarisha zaidi ulinzi na maandalizi ya mwisho ya eneo la kuuaga mwili huo kwenye Union Building, ambapo jeshi litakuwa likikamilisha kuandaa vifaa vyote vitakavyotumika wakati wa maziko yake, kisha mwili wake utachukuliwa na kwenda kuandaliwa rasmi kwa ajili ya kuhitimisha maziko.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mwili huo utawekwa rasmi kwenye eneo hilo siku ya 11 na kuwaruhusu wakuu wa nchi na wageni mbalimbali wa kimataifa watakaokuwa wamefika kumuaga hayati Madiba na baadaye kuhudhuria mazishi hayo.

Taarifa hiyo imeeleza kwamba baada ya kutoa fursa kwa wakuu wa nchi kutoa heshima zao za mwisho safari ya kuelekea kijijini Qunu ambako ndiko alikozaliwa itaanza siku ya 11 kwa ajili ya kuupumzisha kwa amani, kazi ambayo itasimamiwa na jeshi.

Taarifa hiyo inaeleza kwamba katika siku ya mwisho, asubuhi mwili huo utapitishwa katika baadhi ya mitaa kwenye Kijiji cha Qunu kisha kupelekwa katika eneo la nyumbani kwa Mandela na siyo katika makaburi ya familia ya Mandela.

Wageni wanaotarajiwa kuhudhuria mazishi ya Mandela ni pamoja na Rais Barack Obama wa Marekani na mkewe Michelle ambaye aliwahi kumtembelea Mandela nchini Afrika Kusini mwaka 2011 pamoja na binti zake, Sasha na Malia.

Pia rais wa zamani, Bill Clinton na mkewe Hillary ambao wamekuwa marafiki wa karibu wa Mandela wanatajwa kuwa miongoni mwa watakaohudhuria maziko yake, pamoja na marais wengine wastaafu wa Marekani.

Chanzo kutoka Ubalozi wa Uingereza nchini Afrika Kusini kilisema Prince Charles na Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron, wamethibitisha kwamba watahudhuria.
Mgogoro wa familia

Moja ya mambo yanayotarajiwa kuibua utata katika mpango huo wa karibu wiki mbili za maandalizi ya mazishi ni mvutano katika familia ya marehemu Mandela.
Mjukuu wake ambaye ndiye kiongozi wa familia, Mandla amekuwa akituhumiwa kufanya mkakati wa kumzika Mandela kwenye Kijiji cha Mvezo ambako anatambulika kama chifu wa eneo hilo.

Wanafamilia wengine pamoja na serikali ya nchi hiyo wamekuwa wakidai kwamba eneo linalostahili kuzikwa Mandela ni Kijiji cha Qunu ambako amekuwa akiishi tangu alipostaafu.
CHANZO: MWANANCHI

No comments: