Friday, December 6, 2013

Siku Mandela Alipofika Nyumbani Kwa Nyerere Msasani..! (Simulizi Za Mzee Madiba:)

mandelaa_a5117.jpg

Mandela alikuwa njiani kuelekea Addis Ababa kwenye mkutano ambao ANCC walialikwa rasmi. Ni mkutano wa PAFMESCA ambao ungeshirikisha nchi na viongozi wengi wa nchi za Afrika zilizokuwa huru wakati huo. Ilikuwa ni fursa kwa Mandela kufungua milango ya mawasiliano na viongozi mbali mbali kwa manufaa ya ANC na mapambano yao ya ukombozi kutoka ubaguzi wa rangi.

Mandeka aliingia Tanganyika kwa mara ya kwanza kwa kupitia Mbeya. Na tuone kwanza ni jinsi gani Mandela alivyoitafakari nchi yake ya kwanza ya Kiafrika aliyoiona tangu azaliwe. Ikumbukwe,
kwenye safari yake ya Tanganyika, Mandela aliongozana na Bw. Joe Matthews, Mzungu mwanaharakati wa kupinga ubaguzi na mwanachama wa ANC.

Mandela alishangazwa sana na aliyoyaona pale Mbeya, na hususan pale kwenye hoteli waliyofikia. Na hapa Mbeya inaingia katika historia kuwa ni mji wa kwanza wa nchi huru ya Kiafrika uliopatwa kutembelewa na shujaa wa Afrika, Nelson Mandela.

Na kuna Mtanzania anayeingia pia kwenye historia, ni Bw. John Mwakangale, huyu ni Mtanzania wa kwanza, akiwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na kiongozi wa TANU , ambaye ndiye aliyempokea na kuongea rasmi na Nelson Mandela alipofika Mbeya.


Na pale hotelini Mbeya Mandela alishangazwa kuona kuwa hakukuwa na ubaguzi wa rangi kama ilivyo kwao Afrika Kusini. Mandela alibaini mara moja, kuwa amefika katika nchi inayotawaliwa na Waafrika weusi. Kwamba mzungu hakuwa mtu wa kuogopewa. Na hilo linathibitishwa pale bwana mmoja Mtanganyika mweusi, alipoona Mandela na mwenzake wanashangaa shangaa, ndipo Mtanganyika yule alipokwenda sehemu ya mapokezi ya hoteli na kumwuliza mhusika, dada wa Kizungu;

" Madam, did Mr Mwakangale inquire after these two gentlemen" Aliuliza huku akiwaonyesha Mandela na Joe Matthews. Anasimulia Mandela.
Bwana yule Mtanganyika alimwuliza dada yule mhusika kwa vile alimwona Mwakangale akifika hapo kuwaulizia wageni wake hao.

" I am sorry, sir,' – Samahani bwana, alisema dada yule na kisha akaendelea kusema;
" He did, but I forgot to tell them"- kwamba ni kweli Mwakangale amewaulizia, lakini nilisahau kuwaambia. Alisema dada yule mhudumu wa kizungu.

Bwana yule Mtanganyika akamalizia kwa kumwambia mhudumu;
" Please, be careful, madam"- Kwamba , tafadhali dada, uwe mwangalifu.
Ndipo hapo kwa maneno yake, Mandela anasimulia juu ya tukio hilo;
" I then truly realized that, I was in a country ruled by Africans"- Kwamba ndipo kwa ukweli alipobaini, kuwa yuko kwenye nchi inayotawaliwa na Waafrika.
Na Mandela alijiona, kwa mara ya kwanza maishani mwake, kuwa yuko huru, mbali ya kwamba nyumbani kwao Afrika Kusini ni mtu anayesakwa kwa udi na uvumba na watawala.
Hatimaye safari ya kutoka Mbeya kwenda Dar es Salaam ikawadia. Mandela akawasili Dar es Salaam siku ya pili yake.

Alipofika Dar es Salaam, Mandela akakutana na Julius Nyerere nyumbani kwake Msasani. Ndio, ni Julius Nyerere, Rais kijana kwenye nchi ambayo ilikuwa na mwaka mmoja tu tangu ipate uhuru. Mandela alishangaa kuona Rais anakaa kwenye nyumba isiyo ya kifahari. Alishangaa pia kumwona Rais anayeendesha mwenyewe gari yake. Mandela anasema;

" I recall that he drove himself in a simple car, a little Austin"- Nakumbuka aliendesha mwenyewe gari ndogo ya kawaida aina ya Austin. ( Nelson Mandela, Long Walk To Freedom, pg. 345- 346)
Naam,

 Ni yepi mengine yalimshangaza Mandela juu ya Nyerere alipokutana naye pale Msasani? Na je, waliongea nini?
Hii ni simulizi endelevu...

 Na Maggid Mjengwa, 

No comments: