Monday, December 9, 2013

Polisi wamshauri Dk Slaa asifike Kigoma

 dkslaa 75659
Polisi mkoani Kigoma, imemshauri, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Wilbrod Slaa kusitisha ziara zake mkoani Kigoma kwa sababu za kiusalama.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Zedekia Makunja alisema jana: "Ni ushauri tu tunatoa kwa Dk Slaa kwamba anaweza kuahirisha kutokana na hali ilivyo hapa." Hata hivyo, Kamanda Makunja alisema pamoja na yote hayo bado Polisi mkoani, Kigoma imejipanga imara kukabiliana na vurugu zozote zinazoweza kutokea katika ziara hiyo.


Lakini Dk Slaa alipoulizwa kuhusu ushauri huo alisema hawezi kufuta ziara hiyo na kusema hahofii chochote. Alisema na alishafahamu siku nyingi kuwa hayo yanayotokea. Juzi, vijana mbalimbali waliandamana kwa pikipiki na wengine wakitembea kwa mguu huku wakiwa na mabango kupinga ziara ya Dk Slaa Kigoma. Anatarajiwa kuwasili Kigoma Kaskazini keshokutwa.

Hatua hiyo ya kupinga ziara hiyo, imetokana na Kamati Kuu ya Chadema kumvua madaraka aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe ambaye ni mbunge wa Kigoma Kaskazini.

Wakizungumza baada ya maandamano yao yaliyoanzia Kijiji cha Mwandiga kilichopo Kigoma Kaskazini hadi Uwanja wa Mwanga Center, Kigoma, vijana hao walisema kundi hilo halimuungi mkono Dk Slaa.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chadema katika Kijiji cha Mwandiga, Mtoro Mvunye alisema: "Tumetoa wito kwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Issa Machibya na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma (RPC) Fraser Kashai kusitisha ziara hiyo mara moja."
Akizungumza baada ya kupokea maandamano hayo juzi, Mvunye alisema hawataki kumwona Dk Slaa akifika katika Kijiji cha Mwandiga, Ujiji na Mwanga.

"Kwanza nampongeza Mkuu wa Mkoa na RPC kwa kusimamia vizuri maendeleo ya Kigoma, lakini nataka niwaeleze kwamba endapo hawatachukua hatua ya kumzuia Dk Slaa kuja hapa Kigoma, hawa watu wanatudharau sana sisi wa Kaskazini," alisema Mvunye.
Alitoa wito kwa wanachama wa Chadema kutowapigia kura kuwachagua viongozi wote wa mikoa na majimbo walioonyesha kutomuunga mkono Zitto katika sakata hilo ambalo limesababisha mgawanyiko kwa baadhi ya mikoa.

Mjini Singida, Baraza la Uongozi mkoani Singida, limemtaka aliyekuwa Mwenyekiti Chadema Mkoa huo, Wilfred Kitundu kuomba radhi ndani ya siku 14 kutokana na kutoa taarifa ya uongo, uzushi na upotoshaji mkubwa wakati akitangaza kujiuzulu nafasi yake hiyo. Taarifa ya Baraza la Uongozi ilisema asipotekeleza agizo hilo, atavuliwa uanachama. Akisoma taarifa hiyo, Kaimu Mwenyekiti, Shaaban Limu alisema tuhuma zilizotolewa na Kitundu kuwa uamuzi uliotolewa na Kamati Kuu ya kuwavua uongozi kina Zitto na wenzake ni za kipuuzi ni zake binafsi na si za Chadema.
Vurugu zavunja mkutano wa Dk Slaa

Vurugu kubwa zilizuka jana na kusababisha mkutano wa Dk Wilbrod Slaa uliokuwa ukifanyika kwenye Uwanja wa Kigalamo, Kasulu kuvunjika.Mkutano huo ulivunjika baada ya polisi kufyatua mabomu ya kutoa machozi kwa kundi la vijana waliokuwa wakifanya vurugu kwa kuwarushia mawe wanachama na wapenzi wa chama hicho waliokuwa wakimsikiliza Dk Slaa.

Vurugu hizo zilianza baada ya Dk Slaa kumaliza kuhutubia na kuruhusu watu kuuliza maswali.

Polisi walichukua hatua hiyo baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya. Walifyatua mabomu kutawanya kundi hilo na kumteremsha Dk Slaa harakaharaka jukwaani na kuingizwa kwenye gari na kuondoka chini ya ulinzi vijana wa chama hicho, Red Brigade.

Imeandikwa na
 Frederick Katulanda, Thomas Kayanda na Gasper Andrew.
Kigoma

No comments: