Saturday, January 4, 2014

CCM yamtolea uvivu Lowassa urais 2015

mangula1 bcabf
Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula
lowassa1 c95d3
Edward Lowassa (HM)
Unaweza kusema sasa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeamua kumfungia kazi Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa baada ya jana Makamu Mwenyekiti wake (Bara), Phillip Mangula kusema kuwa wanachama wake walioanza mbio za kuwania urais mwaka 2015 watachukuliwa hatua kali za kinidhamu.

Mangula alisema kama wanachama hao wasipochukuliwa hatua watakifanya chama hicho kupoteza mvuto katika medani ya kisiasa nchini;
"Wapo watu wanataka waichanechane CCM kwa sababu ya uroho wao wa madaraka, uroho wa udiwani, ubunge na hata urais. Kuna makundi ndani ya chama kazi yake ni kuwabomoa wenzao, kamwe hatuwezi kuyafumbia macho."

Akifafanua hilo Mangula alisema: "Tutawaita wote walioonyesha nia ya kuutaka urais 2015 na kuwahoji kwanini wanafanya hivyo wakati muda bado haujafika. Tumeshawachunguza
katika mikutano wanayoifanya, tumebaini kuwa wanatoa misaada na kusafirisha watu, tunajua dhamira yao ni nini."


Mangula ametoa kauli hiyo ikiwa imepita siku moja tangu Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye kusema mwanachama yeyote wa CCM anayetangaza nia ya kuwania urais kabla ya muda mwafaka kutangazwa atapoteza sifa za kugombea.
Nape alitoa kauli hiyo baada ya Lowassa siku mbili zilizopita, kutangaza nia 'kimtindo' akisema anaanza rasmi safari aliyoiita ya matumaini ya ndoto zake, ambayo pia itatimiza ndoto za Watanzania za kupata elimu bure, maji safi na maendeleo ya uhakika.

Lowassa ambaye amekuwa akitajwa kuwa mmoja wa wagombea wa nafasi ya urais kupitia CCM katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, alitoa kauli hiyo katika ibada ya shukrani ya kuupokea mwaka mpya, katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Monduli.
Mangula aliwashukia vigogo wa chama hicho wanaoutaka urais jana katika Kikao cha Halmashauri Kuu ya Kamati ya Siasa tawi la Ofisi ndogo za chama hicho Lumumba, wakati akitoa salamu za mwaka mpya kwa wanachama wote wa CCM nchini.

Ataja kanuni za uongozi

Katika mkutano huo Mangula alisaidiwa kusoma kanuni za uongozi na maadili ya chama hicho, kutolea ufafanuzi mambo mbalimbali na Katibu Tume ya Udhibiti wa Nidhamu ya Viongozi wa CCM na wanachama taifa, Masoud Mbengula.

Moja ya kanuni hizo inasema "Ni mwiko kwa kiongozi wa CCM kutumia dini yake au kabila au rangi au jinsia au eneo analotoka, kama sifa ya kushawishi wapiga kura wamchague ama yeye mwenyewe ama mgombea anayemuunga mkono."

Mangula alisema kwa mujibu wa kanuni za chama hicho, mwanachama anayefanya mambo kinyume na kanuni huitwa msaliti na hafai kuendelea kufumbiwa macho kwani anaweza kukiangamiza chama wakati wowote.

"Tutawachukulia hatua kali wale wote ambao wameanza kuonyesha dalili kama hizo za kutoa michango, misaada, zawadi. Lengo la mwanachama huyo ni kutaka kuungwa mkono, wanaotaka madaraka wasubiri muda ufike ndiyo wafanye hivyo."

Aliongeza "Hivi haya mapenzi ya kusaidia yameanza lini, fedha hizo zinatoka wapi, hawa wanaosadiwa wanatakiwa kutambua kuwa yote hayo ni kampeni kwa kuwekeza, hatuwezi kuwa na viongozi wa nchi wa namna hii wa uchu wa madaraka, CCM haitawafumbia macho lazima kanuni na miongozo ifuatwe."

"Kuna watu wameanza kudhani kuwa muda wa kampeni umeanza, muda wa kampeni haujafika na hakuna majina yaliyotangazwa ya kugombea udiwani, ubunge hata urais," alisema Mangula na kuongeza;

"Kuna makundi yanaifanya nchi ya Somalia isitawalike. Makundi ya aina hiyo naona yapo hata CCM; watu wanaibua vita ya maneno ndani ya chama, wanataka wakichanechane chama kwa sababu ya uroho wa madaraka tu."

Bila kuyataja makundi hayo Mangula alisema: "Utaongozaje nchi ambayo imegawanyika katika makundi? Watu wameanza kuvuruga chama chetu, kila mtu
ana kundi lake na wakati mwingine wanayatumia makundi kuwabomoa wenzao, hili jambo hatuwezi kulifumbia macho hata kidogo."


Mbali na Lowassa, wengine wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba.

Makamba hivi karibuni amekuwa akitoa misaada kwa vikundi vya waendesha bodaboda katika mikoa mbalimbali, hali ambayo inatafsiriwa kuwa ni kujiimarisha kisiasa.
Hata hivyo, mwaka jana Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM taifa alinukuliwa akisema kuwa sio vibaya kwa wanachama wa chama hicho kuonyesha nia ya kuwania nafasi za uongozi ndani ya chama, lakini siyo kufanya kampeni.

Mei 26 mwaka jana, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akiwa mkoani Iringa, alisisitiza kwamba chama kitamwadhibu bila huruma mwanachama yeyote anayejipitisha katika maeneo mbalimbali na kufanya kampeni za kuwania urais kabla ya wakati.

Akifunga mafunzo ya makatibu na wenyeviti wa wilaya na mikoa mjini Dodoma mwaka jana, Rais Kikwete alisema kuwa inasikitisha kuona kuwa wapo baadhi ya watu ambao wameanza kujipitisha kwa viongozi wa chama na kuwapatia hela kwa ajili ya kuwapigia debe ili wawachague katika nafasi mbalimbali za urais ama bunge.

Alisema kuwa kimsingi kwa sasa wapo watu ambao wameishaanza kuzunguka na kujinadi kutafuta nafasi mbalimbali za kugombea, huku wakipenyeza rushwa jambo ambalo linaendelea kukishushia hadhi chama hicho.

Uchaguzi Serikali za Mitaa

Mangula akizungumzia uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwaka huu alisema, viongozi wote wanatakiwa kufuata taratibu na kanuni na kujiepusha na vitendo vya rushwa.
"Vitendo vya rushwa ndio vilitufanya katika chaguzi zilizopita kufanya vibaya, watu walinunuliwa kadi, sasa viongozi wa matawi wawe makini tusirudi tulikotoka na tukibaini mtu hafuati kanuni tutamwajibisha," alisema Mangula. 

Chanzo: Mwananchi
...............................................
 

ALIYEJIFUNGUA MAPACHA WANNE KWA MKUPUO AENDELEA VIZURI AOMBA MSAADA KWA WASAMARIA WEMA. MBEYA


Aida Nakawala 25 mkazi wa kijiji cha Chiwanda Wilaya ya Momba Mkoa wa Mbeya, hivi karibuni alijifungua watoto wanne  mapacha kwa mkupuo(Quadliplets) katika usiku wa kuamkia Mwaka mpya anaendelea vizuri.

Mwanamke huyo ambaye kwa hivi sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Wazazi ya Meta akiwa na watoto wake wote wanne alijifungua majira ya saa 10 alfajiri usiku wa kuamkia Januari Mosi Mwaka huu katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi na watoto wakiwa na uzito wa kawaida tofauti na matarajio ya Wengi.

Muuguzi na msimamizi wa Watoto katika chumba cha Joto Sista Frolence Maisa amesema hali za watoto ni nzuri ambapo mama mzazi anahitaji kupatiwa vyakula vinavyoweza kumuongezea maziwa mengi kutokana na idadi ya watoto aliyonayo.
Katibu msaidizi wa hospitali ya  Rufaa Mbeya Mwansasu akipokea msaada huo kwa niaba ya mzazi pia kikosi cha blog ya www.mbeyayetu.blogspot.com            Kikiongozwa na Joseph Mwaisango ambacho kilifika kumjulia hali kiliguswa na hali hiyo na kujitolea kamsaada kidogo wa nguo za watoto sabuni  chupa na dishi  hivyo kuwaomba wadau wengine kumsaidia mama huyo ili aweze kuwalea vizuri watoto wake.

KATIKA hali isiyokuwa ya Kawaida Mwanamke mmoja, Aida Nakawala 25 mkazi wa kijiji cha Chiwanda Wilaya ya Momba Mkoa wa Mbeya, hivi karibuni alijifungua watoto wanne  mapacha kwa mkupuo(Quadliplets) katika usiku wa kuamkia Mwaka mpya anaendelea vizuri.
Mwanamke huyo ambaye kwa hivi sasa anaendelea na matibabu katika Hospitali ya Wazazi ya Meta akiwa na watoto wake wote wanne alijifungua majira ya saa 10 alfajiri usiku wa kuamkia Januari Mosi Mwaka huu katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi na watoto wakiwa na uzito wa kawaida tofauti na matarajio ya Wengi.
Kwa mujibu wa Muguuzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mbozi aliyemfanyia huduma mwanamke huyo, Grace Konga alisema mzazi huyo ni miongoni mwa wazazi 9 waliojifungua katika Mkesha wa Mwaka mpya huku yeye akivunja rekodi kwa kujifungua watoto wanne kwa njia ya kawaida.
Muuguzi huyo alisema watoto hao walizaliwa wakiwa na uzito uliotofautiana kwa mtoto  wa kwanza hadi wa mwisho kuanzia kilogramu 1.6,1.5,1.5  na  2.0 ambapo baada ya kuona hali hiyo ilibidi kumpa rufaa kwa ajili ya msaada zaidi katika Hospitali ya wazazi ya Meta ambapo wapo katika Chumba cha Joto hadi sasa.
Aidha kwa mujibu wa Muuguzi na msimamizi wa Watoto katika chumba cha Joto Sista Frolence Maisa amesema hali za watoto ni nzuri ambapo mama mzazi anahitaji kupatiwa vyakula vinavyoweza kumuongezea maziwa mengi kutokana na idadi ya watoto aliyonayo.
Alisema kwa hivi sasa watoto wananyonya vizuri amb  po maziwa yakipungua kwa mama itahitajika msaada wa maziwa ya Kopo aina ya Laktojeni ili watoto waendelee kupatiwa maziwa kama kawaida na afya zao kuimarika.
Kwa upande wake Mzazi wa watoto hao Aida Nakawala alisema hali yake kiuchumi siyo nzuri kuweza kumudu kuwalea watoto hao na kuongeza kuwa mume wake ni mkulima aliyemtaja kwa jina la Web Simkanda hivyo anaomba msaada wa hali na mali kutoka kwa wasamaria wema.
Alisema huo ni uzao wake wanne ambapo mtoto wake wa kwanza anaumri wa miaka saba, anayefuata ana miaka miwili na miezi tisa huku mwingine akiwa amefariki dunia mara baada ya kujifungua kabla ya uzao huu unaofanya kuwa na watoto Sita.
Alipoulizwa kuhusu kuwepo kwa hali kama hiyo ya kujifungua watoto zaidi ya mmoja katika familia yao alisema Mama yake mzazi amewahi kujifungua mapacha wawili tu na hakuna mtu mwingine aliyewahi kuzidisha idadi hiyo ya watoto kama yeye.
Post a Comment