Thursday, January 2, 2014

Mama yake IGP Mangu anena ya moyoni & Lowassa atangaza nia kimtindo

DSC 0051 92374

mama 0053e
Mama Mzazi wa Mkuu wa Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, Mwanaidi Msengi, amemsihi mwanawe kufanya kazi kwa bidii asimwangushe Rais Jakaya Kikwete ili asije kujutia kumpa nafasi hiyo.

Mwanaidi alisema licha ya furaha kubwa aliyonayo, anamuasa mtoto wake kuchapa kazi kwa bidii kama njia mojawapo ya shukurani kwa Rais Kikwete kwa kumteua akiwa mwenyeji wa kwanza kutoka Mkoa wa Singida kushika wadhifa huo nyeti.


"Hii ni heshima kubwa sana kwangu binafsi, ndugu zake, wakazi wa Kijiji cha Kihunadi na Mkoa wa Singida, kwa hiyo lengo langu ni kumwombea mtoto wangu Mangu asimwangushe Rais... Eee Baba (Mungu) msaidie mwanangu atimize wajibu wake ipasavyo ili Rais Kikwete siku moja aseme hakukosea kumpa Mangu ukuu wa polisi," alisema Mwanaidi.

Juzi ndugu, jamaa na marafiki walifanya hafla ndogo iliyoambatana na vifijo, nderemo na bashasha na wakazi wa Kijiji cha Kihunadi, Tarafa ya Ilongero, mkoani Singida, alikozaliwa IGP huyo huku wakidai sasa kijiji chao kitajulikana haraka ndani na nje ya Tanzania.
Walisema licha ya kujulikana, changamoto mbalimbali zinazokikabili kijiji hicho zitapatiwa ufumbuzi wa kudumu mapema iwezekanavyo.
Mwanaidi alisema Mangu alianza kumwonyesha mafanikio tangu Shule ya Msingi Kinyagigi, kwani alikuwa na bidii ya kujisomea mara kwa mara alishika nafasi ya kwanza au ya pili.

Kwa mujibu wa Mwanaidi, IGP Mangu ni mtoto wa pili kati ya saba aliowazaa.
"Mangu ni wa pili kati ya watoto wangu saba baada ya kuolewa na baba yao, Jumbe Omari Mangu aliyefariki Aprili 27, 1988. Jina la Jumbe linatokana na kupewa kazi ya ujumbe wa wakoloni wakati wa ujana wake," alisema.

Wenyeji wa kijiji hicho, walisema wamekuwa wakiamini Mangu atafika mbali kwa kushika nafasi za juu za uongozi, kutokana na uadilifu, uchapaji kazi, ukaribu wake na wananchi, uaminifu na uwazi.

Mwanaidi alisema Mangu alipofaulu kwenda sekondari alilazimika kuomba ng'ombe kwa mke mweza, ili akamuuze apate fedha za kugharimia masomo ya mtoto wake.
"Mke mwenzangu alimtoa ng'ombe wake, lakini Mangu alipomuuza kwenye mnada pale Singida mjini, aliibiwa fedha zote na alirudi nyumbani akilia sana," alisema.

Alisema baada ya hapo alimwambia mtoto wake kwamba, ataanza kutengeneza vyungu kwa kutumia udongo wa mfinyanzi ili kupata fedha za kugharimia masomo yake."Nashukuru Mangu alinielewa vizuri kwa sababu alishiriki kubeba kichwani vyungu hivyo wakati wa kuviuza hadi kichwa chake kilikaribia kuwa kipara. Nilibuni chanzo kingine cha mapato ambacho kilikuwa ni kukoroga na kuuza pombe za kienyeji," alisema. Inadaiwa baba yake, IGP Mangu alioa wanawake sita kwa nyakati tofauti, lengo likiwa ni kupata mtoto wa kiume. Wengi wa wake zake walikuwa wakizaa watoto wa kike.
CHANZO MWANANCHI

Lowassa atangaza nia kimtindo

  • lowassa 9c1c5
    Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ametangaza kuanza rasmi kwa safari aliyoiita ya matumaini ya ndoto zake, ambayo amesema itatimiza ndoto za Watanzania za kupata elimu bure, maji safi na maendeleo ya uhakika.
Akizungumza katika ibada ya shukrani na kuupokea mwaka mpya, katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),Usharika ya Monduli Mjini, Lowassa bila ya kutaja safari hiyo ni ipi, aliwashukuru watu wote kutoka maeneo mbalimbali nchini, ambao walimsindikiza katika ibada hiyo.

Lowassa alisema anaamini watu hao waliofika, wana uhakika wa ushindi katika safari hiyo kwa kumtegemea Mungu.

"Nimefarijika sana leo kuwaona hapa marafiki zangu wengi. Ninapowatazama hadi machozi yananitoka na kwa uwezo wa Mungu tutashinda kwani nyote mnajua nia na ndoto yangu,'' alisema Lowassa na kupokelewa na sauti za shangwe kanisani.
Licha ya kutoweka bayana, Lowassa amekuwa akitajwa kuwa ni mmoja wa wanasiasa wanaowania kumrithi Rais Jakaya Kikwete baada ya kumaliza kipindi chake cha uongozi mwakani.

Azungumzia Katiba Mpya.
Akizungumzia Katiba Mpya, ambayo mchakato wake sasa unaelekea katika Bunge Maalumu, licha ya kuipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba alisema ana wasiwasi juu ya muundo wa Serikali Tatu.
"Nina wasiwasi na huu muundo, ni vyema viongozi wa dini, kuliombea taifa tupate Katiba bora kwani maoni ya watu asilimia 40 ambao hawakutaka muundo wa Serikali Tatu lazima yatazamwe," alisema Lowassa.

Ibada katika Kanisa hilo, ambayo iliendana na harambee ya kuchangia hosteli na zaidi ya Sh89 milioni kupatikana, iliongozwa na Kaimu Askofu wa KKKT, Usharika wa Kaskazini Kati, Solomon Masango.

Katika mahubiri yake, Kaimu Askofu Masango alimtakia kila la heri Lowassa katika safari yake hiyo akisema anamtambua kuwa ni kiongozi bora.
Hafla ya nyumbani

Akizungumza katika hafla aliyoandaa baadaye nyumbani kwake, Lowassa alirudia kauli yake ya kuanza safari.Waliohudhuria halfa hiyo ni pamoja na wabunge wengi wakiwa wa CCM, wenyeviti wa CCM, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Wenyeviti wa CCM, Mgana Msindai kutoka Mkoa wa Singida, Mwenyekiti wa Wenyeviti wa UVCCM, Manka Dilu kutoka Mkoa wa Mara na Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Wanawake wa CCM, Diana Chilolo pia kutoka Mkoa wa Singida, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara, Lucas ole Mukusi ambaye ndiye katibu wa wenyeviti wote wa CCM.

Wengine waliohudhuria ni wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), mikoa mbalimbali ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM na viongozi wa dini mbalimbali. Pia alikuwapo aliyekuwa mgombea urais wa Kenya katika uchaguzi uliopita, Profesa James ole Kiapi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Lowassa alisema ndoto ya elimu bure, ajira kwa vijana, kuondoa umaskini zitafanikiwa baada ya kuanza safari yake hiyo hapo jana.
Alisema wakati ukifika wa kutangaza rasmi nia hiyo, ataeleza mengi na akawataka wanaomuunga mkono wasiwe na shaka... "WanaCCM msiwe na shaka, tutavuka kwa nguvu zetu... wingi wenu huu unanipa faraja kuwa katika safari yetu na kwa kumtegemea Mungu tutashinda."

Lowassa aliwataka waungane na kaulimbiu yake, 'Tulifurahi pamoja, tulihuzunika pamoja na tutashinda pamoja' na baada ya kusema maneno hayo, alipokewa kwa sauti za CCM... CCM... CCM.
Waalikwa wazungumza
Akizungumza katika hafla hiyo, Msindai ambaye aliwaongoza wenzake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja na Onesmo Nangole wa Mkoa wa Arusha alisema wanamuunga mkono, Lowassa katika safari yake hiyo.
Alisema anamfahamu Lowassa kwa muda mrefu na kumwelezea kwamba ni kiongozi bora mwenye uamuzi na kwamba haoni sababu ya kutokumuunga mkono.
Mgeja alisema anawashangaa watu wachache ambao wameanza tabia ya kulazimisha watu kuwachagulia marafiki na kuwachafua wengine.
Alisema hakuna ambaye hafahamu kuwa Lowassa ndiye tumaini la Watanzania akisema jina lake linatajwa kila kona kwa kuwa ana uwezo na sababu za kuwa kiongozi wa Taifa.

Mgeja alionya kuwa kuna kundi la watu linalodhani kuwa CCM ni mali ya viongozi kitu ambacho alisema si sahihi, bali ni mali ya wanachama ambao alisema ndiyo wenye uamuzi.

Nangole alisema Lowassa ni kiongozi msikivu na makini ambaye ni tegemeo la Watanzania katika kuwaunganisha kuwa kitu kimoja.Wakizungumza katika hafla hiyo, viongozi hao wa CCM, walisema wanamuunga mkono Lowassa kutokana na uwezo mkubwa alionao.

Manko kwa upande wake alisema UVCCM ina imani kubwa na Lowassa kwani ni mmoja wa makada wa CCM wenye historia ndefu katika chama hicho.
Kwa upande wake, Mbunge wa Chemba Kondoa (CCM), Juma Nkamia alisema Lowassa sasa ni sawa na Simba na kusema wanaomchukia walie tu kwani ni kiongozi bora.

Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM, Hussein Bashe aliwataka wananchi wa Monduli kutunza heshima ya Lowassa na kwamba kazi nyingine watafanya wao.
Alisema safari ya Lowassa ndiyo, imeanza inawezekana na kwamba alipoanguka mwaka 2008, ilikuwa ni mipango ya Mungu kuwezesha safari hiyo. "Lowassa ana sifa zote za uongozi... tunachokiomba kwenu ni ushirikiano tu.

No comments: