Tumeona jana, kuwa watu wa nchi ya Kusadikika ni watu wa ajabu sana. Katika nchi yao kumetolewa Rasimu ya Katiba ili ije ijadiliwe na baada ya hapo ipigiwe kura ya maoni na Wasadikika wenyewe, lakini, mpaka kufikia hiyo jana, Wasadikika wengi hawajaisoma hiyo rasimu yenyewe, hii ni pamoja na wanasiasa wa nchi ya Wasadikika.
Na muda unakwenda, lakini, watu wa nchi ya Kusadikika huwa hawana mashaka na muda, isipokuwa siku ya mkesha wa mwaka mpya tu, hapo utawaona Wasadikika wakihangaika sana kujua saa sita usiku itafika muda gani ili wauone Mwaka Mpya. Na wakishauona Mwaka Mpya, basi, watu wa Kusadikika uendelea na mambo yao, saa za mikononi hugeuka kuwa mapambo tu.
Kwa sasa Wasadikika wako bize sana kufuatilia majina ya wagombea urais katika nchi ya Kusadikika. Wasadikika wanapenda sana kujadili majina kuliko masuala ya msingi. Na likishapatikana jina la mgombea Urais, basi, Wasadikika huanza tena mjadala na utabiri wa majina ya warithi wa jina la Rais ajaye wa Wasadikika.
Na Wasadikika wana hulka ya kuamka mwishoni. Kwenye kujadili rasimu yao ya Katiba utawaona, itakapofika siku za mwisho za kufanya maamuzi, kuwa Wasadikika watahangaika sana kutaka kujua nini haswa kilichomo kwenye rasimu hiyo.
Ndio, ajabu nyingine ya watu wa nchi ya Kusadikika ni kuitafuta fimbo wakati nyoka ameshawauma...na ameshakimbia!
Nchi ya Kusadikika ni mwendelezo wa fikra dadisi...na si zaidi..( Kama alivyofanya Shaaban Robert)
Maggid Mjengwa,
No comments:
Post a Comment