Thursday, January 2, 2014

SOKO LA KISASA LA MWANJELWA LILILOGHARIMU BILIONI 13 LATELEKEZWA MBEYA




Pichani Soko kubwa la Kimataifa la Mwanjelwa lililopo Jijini Mbeya ambalo lilitakiwa kumalizika mwaka 2010 likiwa limesimama ujenzi wake baada ya mkandarasi kampuni ya Tanzania Building Work(TBW), kuvunja mkataba na mwajiri Halmashauri ya Jiji la Mbeya,soko hilo limegharimu kiasi cha  sh. bilioni 13,ambapo Mkandarasi anadaiwa kulipwa asilimia 10 ya malipo ya ujenzi wa soko hilo ambalo ulitokana na kuungua kwa soko la awali la Mwanjelwa mwaka 2006.
NILIPOTEMBELEA SOKO LA MWANJELWA KUJIONEA HARI HALISI YA UTEKELEZWAJI WAKE AMBAPO HADI SASA UJENZI HUO WA SOKO JIPYA LA KISASA UNA SUASUA KUISHA ILI WANAINCHI WA MBEYA NA NYANDA ZA JUU KUSINI KUFAIDIKA NA SOKO HILI
Soko la Mwanjelwa linavyoonekana kwa nyuma kutoka katika mitaa ya Mwanjelwa
 
DALILI za kumalizika kwa soko la Mwanjelwa lililogharimu zaidi ya sh. bilioni 13 ambalo linatarajiwa kutumiwa na wafanyabiashara  wanaokadiriwa 1000,zinaonekana kugonga mwamba baada ya mkandarasi aliyekabidhiwa kujenga soko hilo kuvunja mkataba.
 
Soko la Mwanjelwa liliungua Disemba 2006 na kusababisha hasara  kubwa ambapo wafanyabiashara waliokuwa wakilitumia soko hilo walihamishiwa katika soko la muda katika uwanja unaomilikiwa na Shirika la Kuendeleza Viwanda Vidogo Nchini (SIDO).
 
Hatua ya Mkandarasi huyo kampuni ya Tanzania Building Works kuvunja mkataba unadaiwa umetokana na msuguano uliopo baina yake na mmiliki wa Soko hilo ambaye ni Halmashauri ya Jiji la Mbeya.
 
Katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo hivi karibuni, wajumbe wa kikao hicho walihitaji kupewa taarifa za maendeleo ya ujenzi wa soko hilo ambao tangu kuanzishwa kwake limekuwa likikumbana na malumbano ambapo mkataba wa awali wa soko hilo ulitakiwa kuishia mwaka 2010.
 
Kwenye kikao hicho Meya wa Jiji la Mbeya Bw.Athanas Kapunga alimzuia Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa Jiji Dkt.Samwel Lazaro kutoa taarifa za maendeleo ya ujenzi wa soko hilo kwa kile kilichoeleza kuwa kinaweza kuibua maswali mengi kutoka kwa madiwani ambao walihitaji kupewa taarifa hizo.
 
Imeelezwa kuwa msuguano huo umetokana na mkandarasi kushindwa kukabidhi soko kulingana na mkataba wake pamoja na kulipwa fedha sh.bilioni 10.6 ambazo ni sehemu ya malipo ya kati ya sh.bilioni 13 ambazo ndizo gharama halisi ya ujenzi wa soko hilo la kisasa lenye ghorofa tatu.
 
Aidha ujenzi wa soko hilo umedaiwa kuiingizia hasara Halmashauri ya Jiji hilo ambapo katika kamati ya Bunge Hesabu za Serikali za mitaa(LAAC) jambo hilo liliibuliwa na kuelezea sababu za kukwamisha mradi huo wa soko ambalo likimalizika linaweza kuhudumia wafanyabiashara zaidi ya 3000.
 
Katika taarifa ya (LAAC) halmashauri ilimlalamikia Mkandarasi kukiuka sheria za mkataba ambapo kila alipokabidhiwa fedha kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa soko hilo inadaiwa kuwa alikuwa akitumia fedha hizo kwa kuendeleza miradi mingine inayoendeshwa na kampuni hiyo mahala pengine. 
 
Awali ujenzi wa soko hilo ulitarajiwa kutumia jumla ya miezi 18 baada ya kuanza kutekelezwa kwa mradi huo Februari 25 mwaka 2010 na kukamilika Agosti 25 mwaka 2011.
 
Pamoja na mkandarasi huyo kushindwa kutekeleza mradi huo kwa wakati, Halmashauri ya Jiji ilimpa muda wa ziada kwa awamu tatu za wiki 20 ambapo alishindwa kukamilisha hadi Juni 19 mwaka huu alipoandika barua ya kuvunja mkataba.
 
 Kwenye barua yenye kumbukumbu SAM/828/RET  ya Julai 19, 2013 inamtaarifu mmiliki( Halmashauri ya Jiji) kusudio lake la kuvunja mkataba kwa kile alichodai kunyimwa nyongeza ya muda wa ziada wa miezi 9 ili amalizie asilimia 80 ya ujenzi wa soko hilo na kulikabidhi.
 
 Kwa upande wake Halmashauri ya Jiji iliridhia ombi la kuvunjwa kwa mkataba wa ujenzi wa soko hilo kwa barua yenye kumbukumbu namba MD/MM/MBEYA/152/2013 ya Julai 25 na kueleza kuwa inchokisubiri ni taratibu za kisheria ili kukubali kuvunja mkataba huo.
Katika sehemu ya barua ya halmashauri ya jiji imeeleza hatua zilizochukuliwa baada ya muda wa makubaliano kumalizika Julai 25 ambapo Halmashauri ilipokea utaratibu wa hatua zinazoendelea wakati wa uvunjaji wa mkataba kutoka kwa mkandarasi kutakiwa kuweka walinzi eneo la ujenzi ili kulinda mali zisitoroshwe. 
 
Imeelezwa kuwa hatua ya Halmashauri kusitisha mkataba wa ujenzi unaweza kuiongezea gharama halmashauri ambapo italazimika kutumia ziada ya sh bilioni 3 ikiwa ni ongezeko la za gharama halisi ya sh. bilioni 6 za kumalizia mradi huo.
 
Ongezeko la gharama kwa Halmashauri ya Jiji litatokana na kutangaza upya zabuni ya kumpata mkandarasi mpya atakayechukua kazi ya kumalizia asilimia 20 ya ujenzi iliyobaki. 
 
Hasara nyingine ambayo itaigharimu halmashauri ya Jiji baada ya kukubali kuvunjwa kwa mkataba na kumtafuta mkandarasi mpya ni pamoja na kumlipa mkandarasi mshauri wa kampuni ya MD ya Jijini Dar es salaam kiasi cha Sh. bilioni 1.2. 
 
Inaelezwa kuwa hali hiyo itasababisha Halmashauri kupangisha wafanyabiashara wenye mitaji mikubwa katika soko hilo ili kupata fedha za kufidia ongezeko la gharama za kumalizia ujenzi wa soko hilo na kuwanyima fursa wafanyabiashara ambao ni wahanga wa soko lililoungua
 
NA RASHID MKWINDA

No comments: