Dar es Salaam/Dodoma.Wakati Wajumbe wa
Bunge Maalumu la Katiba wakiwasili mjini Dodoma, Ofisi ya Bunge
imetangaza kuandaa utaratibu wa malazi kwa wajumbe hao katika hoteli
mbalimbali mjini humo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na
Ofisi ya Katibu wa Bunge na Katibu wa Baraza la Wawakilishi, jumla ya
hoteli 27 zimeainishwa kuwapokea wajumbe hao 640 ambao wanatarajiwa
kuwapo mjini Dodoma kwa muda wa miezi mitatu.
Pamoja na utaratibu wa malazi, taarifa
hiyo pia iliagiza wajumbe hao kuwasili wakiwa na nakala halisi za
vitambulisho vitakavyotumika kwa ajili ya usajili.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa usajili
utafanyika leo na kesho kwenye Ofisi za Bunge, ambapo zoezi hilo
litajumuisha ujazaji wa fomu, upigaji picha za vitambulisho sambamba na
kukabidhiwa vitendea kazi.
Baada ya zoezi hilo Katibu wa Bunge na
Katibu wa Baraza la Wawakilishi watakutana na wajumbe kwa ajili ya
kutoa maelekezo ya awali yanayohusiana na utaratibu wa ukaaji, jiografia
ya viwanja vya Bunge na huduma za utawala.
Kikao cha kwanza cha mkutano huo
kitafanyika Jumanne ijayo, ambapo pamoja na masuala mengine kitahusisha
uchaguzi wa mwenyekiti wa muda atakayesimamia upitishwaji wa kanuni na
uchaguzi wa Mwenyekiti wa Bunge hilo.
Wiki iliyopita Ikulu ilitangaza majina
ya wajumbe 201, yaliyoteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kushiriki katika
uchambuzi wa Rasimu ya Pili ya Katiba na kutengeneza Katiba Mpya.
Mbali ya wajumbe wa Bunge la Katiba, pia wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) wako Dodoma wakiendelea na vikao vyao.
Mji wafurika wageni
Kutokana na kuwapo kwa ugeni huo, Mji
wa Dodoma umefurika wageni wakiwamo wajumbe wa Bunge la Katiba na
Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) huku, maeneo mengi
yakionekana kufanyiwa usafi.
Hata hivyo, wageni wengi walionekana
kuingia jana na baadhi ya watumishi wa hoteli hizo walikiri kuwasajili
baadhi ya wageni, ambao wapo katika orodha hiyo.
Gazeti hili jana lilishuhudia kukiwa
na maandalizi ya mwisho kwa ajili ya mapokezi hayo, huku baadhi ya
maeneo yakiendelea kukarabatiwa ikiwamo kupaka rangi.
Moja kati ya maeneo ambayo wageni wengi wamepangwa kufikia ni Hoteli ya New Dodoma ambayo imepangiwa vyumba 87.
Katika eneo la hoteli hiyo, jana
kulikuwa kukifanyika usafi wa hali ya juu ikiwemo kupata rangi,
kusafisha maji kwenye bwawa la kuogelea, kupulizia dawa baadhi ya maeneo
na katika bustani ikiwamo kufagia paa la juu upande wa vibanda.
Hoteli nyingine ambayo kulikuwa na usafi katika kumbi zake pamoja na mandhari ya nje ni Fifty Six
Na Elizabeth Edward na Hebel Chidawali, Mwananchi
No comments:
Post a Comment