WACHEZAJI wa timu ya soka ya Mbeya
City, wamepigwa marufuku kunyoa nywele za pembeni na kuziacha za
katikati 'kiduku' na wameambiwa atakayejitosa kunyoa hivyo itakula
kwake.
Mbali ya hilo, pia wamepigwa marufuku kufuga nywele na kuzisokota 'rasta'.
Kauli ya marufuku hiyo imetolewa na
Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Maka Mwalwisi na kuungwa mkono na Katibu
Mkuu, Emmanuel Kimbe, waliosema wachezaji wa timu yao hawajafikia hatua
ya kunyoa nywele kwa mfumo huo kama wanavyofanya wachezaji wa timu
nyingine.
Mwalwisi alisema kuwa wachezaji wa
Kitanzania wameiga mfumo huo kutoka kwa wachezaji wa nje jambo ambalo
kwao imekuwa ni vigumu kuhudumia nywele zao kutokana na kipato kidogo
wanachokipata.
"Kilichoruhusiwa ni kunyoa upara, hayo
mambo mengine ya 'kiduku' na 'dread' kwetu hayana nafasi, kwanza uwezo
wenyewe wa kuzihudumia hawana maana wakiweka hizo 'dread' zao wanakuwa
kama wachafu," alisema. "Nywele zinahitaji matunzo kama wanavyofanya
wachezaji wa nje pia muda wa kwenda kuzihudumia saluni, hapa Tanzania
hata hao wanaofuga na kunyoa viduku uwezo wao kifedha sio mkubwa,
tumewaambia atakayenyoa hivyo atapewa adhabu kwa mujibu wa taratibu
zetu."
Alisema kuwa kwao nidhamu ya ndani na
nje ya uwanja ndiyo wanaipa kipaumbele kuliko mambo mengine yoyote,
suala ambalo liliungwa mkono na aliyekuwa mwamuzi wa soka, Othman Kazi.
Kazi alisema: "Tangu wapande daraja
nimebahatika kuangalia mechi zao ila sijawahi kuona timu yenye nidhamu
kama Mbeya City, ingawa siwezi kuzungumzia kiundani mechi yao na Yanga.
"Wachezaji wa Mbeya City hawana tabia
ya kumzonga mwamuzi pale anapotoa uamuzi wake na hiyo ndiyo nidhamu
inayotakiwa kwa wachezaji."
Katika mechi ya timu hiyo dhidi ya
Yanga iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Yanga ilishinda
bao 1-0. Hicho kilikuwa kipigo cha kwanza cha Mbeya City katika msimu
wao wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara
No comments:
Post a Comment