Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Dar es
Salaam ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha Tanzania
Pharmaceutical Ltd cha Dar es Salaam (TPI), Ramadhani Madabida na
wenzake watano wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
wakikabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kusambaza dawa bandia na
kusababisha hasara ya Sh148.3 milioni.
Wakili wa Serikali, Faraja Nchimbi
aliwataja washtakiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo kuwa ni
Mkurugenzi wa Operesheni wa TPI, Seif Shamte, Meneja Masoko, Simon
Msofe, Mhasibu Msaidizi, Fatma Shango pamoja na wafanyakazi wa Bohari ya
Dawa (MSD), Sadick Materu na Evans Mwemezi.
Akisoma hati ya mashtaka mbele ya
Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Nyigulile Mwaseba, Wakili wa Serikali,
Shadrack Kimaro alisema katika shtaka la kwanza, Aprili 5, 2011,
Madabida, Shamte, Msofe na Shango wakiwa na nyadhifa hizo kwenye kiwanda
cha TPI walisambaza makopo 7,776 ya dawa bandia za kufubaza virusi vya
Ukimwi (ARV) aina ya Antirectroviral.
Kimaro alidai kuwa washtakiwa hao,
walifanya kosa hilo kinyume na kifungu cha 76 (1)(2) cha Sheria ya
Chakula, Dawa na Vipodozi ya mwaka 2003, wakijaribu kuonyesha kuwa dawa
hizo zilikuwa halali na kwamba zimetengenezwa Machi, 2011 na muda wake
wa kutumika unakwisha 2013 wakati wakijua kuwa si kweli.
Katika shtaka la pili, Wakili Kimaro
alidai kuwa Aprili 11, 2011, Madabida, Shamte, Msofe na Shango
walisambaza na kuuza makopo 4,476 ya dawa bandia aina ya Antiretroviral
walizokuwa wakijaribu kuonyesha kuwa zilikuwa na viambatanisho vya
Starudine 30mg, Nevirapine 200mg, Lamivudine 150mg pamoja na fungu namba
OC 01.85.
Alidai kuwa washtakiwa hao waliweka
viambatanisho hivyo wakijaribu kuonyesha kuwa dawa hizo zilikuwa halisi
na kwamba zilitengenezwa Machi 2011 na muda wake wa kutumika ulikwisha
Februari 2013 huku wakijua kwamba ni uongo.
Katika shtaka la tatu wanadaiwa
kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kinyume na Kifungu cha 302 cha
Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka
2002.
Wakili Kimaro alidai kuwa kati ya
Aprili 12 na 29, 2011, washtakiwa hao wakiwa na nia ya kulaghai,
walijipatia Dola za Marekani 98,506 sawa na Sh148,350,156.48 wakijaribu
kuonyesha kuwa kiasi hicho cha fedha ni malipo halali ya makopo 12,252
ya dawa aina ya Antirectrovial yaliyokuwa katika fungu (batch) namba OC
1.85.
Alidai pia kuwa washtakiwa hao
walikuwa wakionyesha dawa hizo bandia zilikuwa zimetengenezwa Machi,
2011 na kwamba muda wake wa kumalizika kutumika ni Februari, 2013 na
wakafanikiwa kujipatia kiasi hicho cha fedha kutoka MSD.
Katika shtaka la nne, Materu na
Mwemezi wakiwa ni Meneja wa Udhibiti Viwango na Ofisa Udhibiti Viwango
wa MSD, kati ya Aprili 2 na 13, 2011 huku wakijua nia ya kutendeka kwa
makosa hayo ya usambazwaji wa dawa bandia, walishindwa kuzuia kinyume na
Kifungu cha Sheria namba 383 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16
iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Katika shtaka la tano, wakili huyo wa
Serikali alidai kuwa kati ya Aprili 5 na 30, 2011, washtakiwa Madabida,
Shamte, Msofe, Shango pamoja na Materu na Mwemezi, kinyume na Sheria ya
Uhujumu Uchumi, walishindwa kutekeleza majukumu yao wakiwa watendaji.
Alidai kuwa katika kipindi hicho,
washtakiwa hao kwa pamoja walishindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo
kwa kusambaza makopo 12,252 ya dawa bandia wakijaribu kuonyesha kuwa
zilitengenezwa Machi 2011 na kwamba zitakwisha muda wake wa kutumika
Februari 2013 na kuisababishia mamlaka hiyo ya Serikali hasara ya
Sh148,350,156.48.
Washtakiwa wote walikana mashtaka
yanayowakabili na upande wa mashtaka ulisema upelelezi wa kesi hiyo bado
haujakamilika. Akitoa masharti ya dhamana, Hakimu Mwaseba alimtaka kila
mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika ambao wanafanya kazi
kwenye taasisi zinazotambulika kisheria na kwamba kila mdhamini
angesaini bondi ya Sh6,181, 256.
Pia alimtaka kila mshtakiwa kutoa
kiasi cha Sh12, 362,513 milioni taslimu mahakamani hapo au hati ya mali
isiyohamishika yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha.
Madabida na Materu waliachiwa huru baada ya kukamilisha masharti hayo huku wenzao wakipelekwa mahabusu kusubiri kuyakamilisha.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 24, mwaka huu itakapotajwa.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment