Dar es Salaam. Vigogo sita ambao
wanatajwa kuwa wanajiwinda kwa ajili ya kuwania urais kupitia CCM katika
uchaguzi mkuu ujao, wameitwa mbele ya Kamati ya Ndogo ya Maadili ya
chama hicho, kwa ajili ya kuhojiwa kwa tuhuma za kukiuka maadili.
Habari ambazo zililifikia gazeti hili
jana zinawataja vigogo hao kuwa ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward
Lowassa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven
Wassira na Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye.
Wengine ni Waziri wa mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, aliyewahi kuwa Waziri wa
Nishati na Madini, William Ngeleja na Naibu Waziri wa Mawasiliano,
Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
"Wote wamepelekewa barua za wito wa
kufika mbele ya Kamati ya Maadili inayoongozwa na Mzee Mangula (Philip,
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Bara), ambayo itakutana mjini Dodoma, Februari
14 (kesho kutwa) ," kilisema chanzo chetu cha habari kutoka Ofisi Ndogo
ya CCM, Lumumba, Dar es Salaam na kuongeza:
"Barua hizo zimesainiwa na Mzee Kinana
(Abdulrahman, Katibu Mkuu wa CCM) mwenyewe na tayari zimeanza
kusambazwa leo (jana) mchana."
Kamati hiyo ndogo ya maadili, inaundwa
na Mangula, Kinana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu
na Bunge), William Lukuvi, Shamsi Vuai Nahodha, Dk Maua Daftari na
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Dk Pindi Chana.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM,
Nape Nnauye jana alithibitisha kuwapo kwa Kikao cha Kamati ya Maadili
Februari 14 pamoja na kuitwa kwa baadhi ya wanachama kwa ajili ya
kuhojiwa.
Hata hivyo, hakuwa tayari kutaja
majina yao wala idadi ya walioitwa... "Wewe fahamu tu kwamba kikao hicho
kitafanyika tarehe hiyo uliyoitaja, lakini masuala ya majina na idadi
ya walioitwa yatajulikana kwenye kikao, mimi sina kwa sasa," alisema
Nnauye.
Katika siku za karibuni kumekuwa na
vita ya maneno baina ya makada wa chama hicho, wakituhumiana kutangaza
mapema kugombea urais kabla ya ruhusa rasmi ya chama.
Kauli za walioitwa
Jana, gazeti hili lilizungumza na baadhi ya walioitwa na wengi wao walisema hawakuwa wamepokea barua za wito huo.
Sumaye kwa upande wake alisema: "Kwa sasa niko Mwanza na sijapata barua yoyote ya kuitwa katika kikao chochote cha chama."
Lowassa alipigiwa simu mara kadhaa na
kusema kuwa yuko kwenye kikao apigiwe baadaye. Alipigiwa mara sita na
kusema alikuwa bado kwenye kikao.
Membe kwa upande wake alisema: "Kwangu
si mara ya kwanza kuitwa Kamati ya Maadili, ifahamike kwamba unaweza
kuitwa kutoa ushahid, maelezo au ufafanuzi wa jambo lolote unalokuwa
umeitiwa."
Wassira pia alisema hakuwa amepata
barua hiyo ya wito... "Mimi ndiyo nimeshuka kutoka Bunda, sina hiyo
barua ya kuitwa kwenye Kamati ya Maadili. Mwaliko nilionao ni wa kikao
cha Kamati Kuu kesho (leo) ambao mimi ni mjumbe," alisema Wassira.
Kwa upande wake, Makamba naye alisema
alikuwa hajapata wito huo, wakati Ngeleja hakukanusha au kuthibitisha
kupokea barua hiyo kwa maelezo kwamba yeye siyo msemaji wa CCM, hivyo
asingeweza kuzungumzia suala la kuitwa kwake.
"Kwa kweli wewe fahamu tu kwamba mimi
siyo msemaji wa chama. Chama chetu kina utaratibu wa wasemaji wake,
waulize hao maana watakuwa na taarifa sahihi," alisema Ngeleja.
Katika hatua nyingine, Nnauye alisema
Kamati Kuu (CC) ya CCM, inakutana Dar es Salaam leo, huku Halmashauri
Kuu (NEC) ya chama hicho ikitarajiwa kukutana Jumamosi na Jumapili wiki
hii mjini Dodoma.
Vikao hivyo pamoja na mambo mengine
vinatarajiwa kujadili ushiriki wa wajumbe wake katika Bunge Maalumu la
Katiba ambalo limepangwa kuanza Februari 18, mwaka huu mjini Dodoma.
No comments:
Post a Comment