Monday, February 3, 2014

WOSIA WA MANDELA HADHARAN


nelsonmandela2_a8856.jpg
Marehemu Nelson Mandela enzi za uhai wake

Na Fadhy Mtanga
Nelson Mandela ameacha mali yenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 4.1 kwa mjane wake Graca Machel, familia, wafanyakazi wa taasisi yake, mashule na chama chake cha ANC. Hii ni kwa mujibu wa wosia wake uliotolewa leo.

Ikiwa ni miezi 2 baada ya kifo chake akiwa na umri wa miaka 95, wanasheria wake wanasema Graca Machel amerithishwa nusu ya mali hiyo, ingawa huenda akawa tayari kupokea kiasi kidogo tu ukijumlisha mali zilizopo nchini Msumbiji.

Mtandao wa Africa Review umeandika kuwa mapato kutoka katika vitabu vyake na miradi mingine vimerithishwa kwa mfuko wa familia.
Nyumba yake ya Houghton, Johannesburg ambako Mandela alifia panapo Disemba 5, 2013 itatumiwa na familia ya merehemu mtoto wake wa kiume, Makgatho.

"Ni nina yangu itumike kama pahala pa kuwakusanya familia ya Mandela kwa minajili ya kulinda umoja wake kwa kipindi kirefu baada ya kifo changu." Ameandika Mandela katika wosia huo.
Kila mtoto wa Mandela alikopeshwa dola laki tatu wakati wa uhai wake Mandela. Ambaye hakuwa amerejesha deni hilo atakatwa katika mgao wa urithi.

Mandela ametoa kiasi cha dola 4,500 kwa watumishi wote wa taasisi yake akiwemo msaidizi wake wa muda mrefu, Zelda la Grange.
Pia wosia huo umetoa kiasi cha dola 90, 000 kwa kila moja ya taasisi tano za kielimu. Wanufaika ni vyuo vikuu viwili, Wits na Fort Hare, pamoja na shule zingine tatu.

Chama chake, ANC ambacho alipata kuwa rais wake kitapta pia mgao kwa mujibu wa wosia huo.
Wosia huo wa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini uliandikwa mwaka 2004 na marekebisho ya mwisho kufanywa 2008.
Wosia huo unamaliza sintofahamu iliyoigubika familia ya mwanamapinduzi huyo maarufu barani Afrika na kote ulimwenguni. Vuta n'kuvute ya mgao wa mali ilitawala familia hiyo hata kabla ya kifo chake.

Msimamizi wa mirathi hiyo, Dikgang Moseneke, naibu mkuu wa Mahakama ya Katiba ya Afrika Kusini, amesoma kusomwa kwa wosia huo kumepokelewa kwa hisia tofauti na wanafamilia lakini hadi sasa hakuna aliyeupinga.
Post a Comment