Thursday, April 3, 2014

Ikulu yamchoka Warioba

ikulu_c7cbf.jpg
IKULU ya Rais Jakaya Kikwete imesema kuwa muda wa mwisho wa uhai wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ulijulikana, hivyo mtu kujitia kwamba ameisahau siku hiyo ni unafiki wa hali ya juu.Ikulu imetoa kauli hiyo ikijibu madai yanayodaiwa kutolewa na Mwenyekiti wa Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, kwenye moja ya vyombo vya habari jana,akidai Ikulu imeitupia virago tume yake.
Taarifa hiyo ya ufafanuzi ambayo ilitawaliwa na maneno makali dhidi ya Tume ya Jaji Warioba, ilitolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu na kusainiwa na Mkurugenzi wake Salva Rweyemamu.


Katika taarifa hiyo, Ikulu ilisema kuwa muda wa uhai wa tume hiyo ulijulikana, hivyo kwa mtu kujitia ameisahau siku hiyo ni kiwango cha juu sana cha unafiki.
Ingawa Ikulu haikumtaja moja kwa moja Jaji Warioba kuwa ni mnafiki, lakini ukweli ni kwamba kauli ya unafiki ilimlenga Jaji Warioba aliyekaririwa na gazeti moja juzi, akidai kuwa Ikulu imeitupia virago tume yake.

Madai ya Tume ya Warioba kufukuzwa kazi

Salva alisema kuwa itakumbukwa kuwa moja ya mijadala mikali ya awali kuhusiana na mchakato wa katiba mpya ulihusu lini Tume ya Mabadiliko ya Katiba imalize muda wake.
Alisema wengine walitaka tume imalize muda wake baada ya kukabidhi ripoti ya tume na rasimu ya katiba, wengine wakitaka tume baada ya Mwenyekiti wake Jaji Warioba kuwasilisha rasimu yake bungeni na hata wengine wakitaka wajumbe wa tume wawe sehemu ya Bunge Maalumu la Katiba.
"Hatimaye ilikubaliwa kuwa shughuli za tume zingefikia ukomo wake baada ya mwenyekiti wake kuwasilisha rasimu ya katiba kwenye Bunge Maalumu la Katiba kama inavyoelekezwa katika kifungu cha 31 (1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

"Kifungu hicho kinasema kuwa baada ya kuwasilishwa kwa rasimu ya katiba kwenye Bunge Maalumu chini ya kifungu cha 20(3) (cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba), rais, kwa amri itakayochapishwa katika Gazeti la Serikali, atavunja tume.

"Mheshimiwa Warioba aliwasilisha rasimu ya katiba katika Bunge Maalumu la Katiba Jumanne ya Machi 18, mwaka huu, 2014 na siku iliyofuata Jumatano, Machi 19, 2014 na kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, rais alitia saini tangazo la serikali la kuvunja Tume ya Mabadiliko ya Katiba," alisema Salva.

Kwa mujibu wa Salva, tangazo hilo lilichapishwa katika toleo lililofuata la Gazeti la Serikali Machi 21, 2014.
"Hivyo, tokea mwanzo wa mchakato mzima wa katiba mpya na utendaji kazi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba hapakupata kuwepo, hata wakati mmoja, shaka kuhusu siku ya tume hiyo kumaliza kazi zake.

"Mwenyekiti wa tume, wajumbe wote wa tume, sekretarieti ya tume na Watanzania wote waliijua fika siku ya mwisho ya tume kukamilisha shughuli zake. Kwa mtu kujitia ameisahau siku hiyo leo ni kiwango cha juu sana cha unafiki," alisema Salva.
Wajumbe wa tume kutakiwa kurudisha magari Ikulu

Akijibu madai mengine ya Jaji Warioba ya wajumbe wa tume yake kutakiwa kurudisha magari Ikulu, Salva alikiri kuwa kweli wajumbe wa tume walitakiwa kurudisha Ikulu magari ambayo walikuwa wanatumia kikazi kwa sababu kazi ya tume ilikuwa imemalizika.

Pili, alisema tume ilijua tokea mwanzo kuwa baada ya kumaliza kazi yao, magari ambayo walikuwa wanatumia wajumbe na maofisa wa tume hiyo yalikuwa yanatakiwa kupelekwa Dodoma kwa matumizi ya shughuli za Bunge Maalumu la Katiba ambalo linakabiliwa na shida kubwa ya usafiri.
"Serikali ilichukua uamuzi kuwa magari hayo yapelekwe Dodoma kwa sababu lisingekuwa jambo la busara kwa serikali kutumia fedha za umma kununua magari mengine mapya wakati yale ya tume bado yanafaa kufanya kazi na wala hakuna bajeti ya kufanya manunuzi ya magari mapya.

"Hivyo, ni kweli magari hayo yako Ikulu, Dar es Salaam, yakisubiri kukamilika kwa taratibu za kuyapeleka Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma," ilisema Ikulu.
Muda wa kukabidhi nyaraka na ofisi

Akijibu madai mengine ya Jaji Warioba kwamba hawakupata muda wa kukabidhi ofisi na nyaraka, Ikulu ilisema kuwa hili nalo ni jambo la kutunga na kuzusha tu.
Alisema Jaji Warioba alikabidhi rasmi Ripoti ya Tume na Rasimu ya Katiba kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein, Desemba 30, 2014, mbele ya wananchi katika viwanja vya Ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam.

"Hivyo, toka siku hiyo, tume haikuwa tena na kazi ya kuandaa ripoti ama rasimu kwa sababu kazi hiyo ilikuwa imekwisha na wala isingeweza kuibadili tena rasimu ya katiba.
"Kwa maana hiyo, toka Desemba 30, mwaka jana, kupitia miezi ya Januari, Februari mpaka Machi 18, mwaka huu, sekretarieti ilikuwa na muda wa siku 77, zaidi ya miezi miwili unusu, kufanya maandalizi ya kukabidhi nyaraka na ofisi kwa sababu ilijua kazi yake ilikuwa inamalizika siku ambayo mwenyekiti wa tume hiyo angewasilisha rasimu ya katiba katika Bunge Maalumu la Katiba.
"Sasa katika muda wote huo, sekretarieti ya tume ilikuwa inafanya nini badala ya kuandaa ripoti ya makabidhiano na wakati maofisa wake walikuwa wanaendelea kulipwa mshahara na serikali? Kwanini walalamike hadharani leo kwa jambo ambalo lilikuwa ni la wajibu wao na wakashindwa kulifanya kwa wakati?" alihoji Salva.

Salva katika taarifa hiyo, pia alijibu madai kwamba wajumbe wa tume watalipwa kiinua mgongo cha sh milioni 200 kila mjumbe.
Alisema hakuna shaka kuwa wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wamefanya kazi nzuri sana na wanastahili pongezi nyingi za wananchi. Lakini kama wanadhani kuwa serikali ina uwezo wa kumlipa kila mjumbe kiinua mgongo cha sh milioni 200 basi wanajidanganya kwani wananchi wa Tanzania hawawezi kuelewa maana kabisa ya malipo hayo makubwa kupindukia.

"Alichokizungumza Rais Kikwete tokea mwanzo wa mchakato ni kwamba atafikiria kuwalipa wajumbe wa tume aina fulani ya kifuta jasho ambacho kiwango chake atakiamua yeye na kwa wakati mwafaka na kulingana na rasilimali za serikali. Mpaka sasa hajafanya uamuzi juu ya jambo hili," alisema Salva.

Ikulu pia katika taarifa hiyo ilitoa ufafanuzi wa habari zinazosambazwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa wajumbe wa tume hiyo walikuwa wanalipwa sh 500,000 (laki tano) kama posho ya vikao kwa siku.

"Ukweli ni kwamba wajumbe wa tume walikuwa wanalipwa sh 200,000 kama posho ya vikao kwa siku. Maofisa waandamizi wa tume hiyo walikuwa pia wanalipwa posho ya sh 200,000 (laki mbili) kwa siku, maofisa wa kati walikuwa wanalipwa sh 150,000 kutwa na maofisa wa ngazi za chini walikuwa wanalipwa sh 100,000 kwa siku kulingana na taratibu za serikali. Anayetangaza vinginevyo anajaribu tu kuwapotosha wananchi," alisema Salva.

Juzi, Jaji Warioba alikaririwa na moja ya magazeti akisema kuwa tume yake ilifukuzwa kazi, na kwamba haikupewa muda wa kuandaa na kuwasilisha nyaraka za kukabidhi ofisi na madaraka.
Kwamba wajumbe wa tume hiyo waliporwa magari ambayo yamewekwa Ikulu.

No comments: