Afisa
Habari wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Owen Mwandumbya
akielezea kuhusu kufanyika kwa vikao vya Kamati za Bunge vinavyotarajia
kuanza tarehe 28 Aprili hadi 4 Mei, 2014, Jijini Dar es Salaam kabla ya
kuanza Mkutano wa Bunge wa Bajeti tarehe 6 Mei, 2014.
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
BUNGE LA TANZANIA
TAARIFA KWA UMMA
KAMATI ZA KUDUMU ZA BUNGE KUKUTANA DAR ES SALAAM KUANZIA TAREHE 28 APRILI HADI 4 MEI, 2014
1.0 UTANGULIZI
Kamati
za Kudumu za Bunge zitaanza kukutana tarehe 28 Aprili hadi tarehe 4 Mei
2014 Jijini Dar es Salaam, kutekeleza Majukumu yake, kabla ya Mkutano
wa Bunge Bajeti uliopangwa kuanza mjini Dodoma tarehe 6 Mei na kudumu
hadi tarehe 27 Juni, 2014.
Kwa
kawaida, Kamati za Kudumu za Bunge hupaswa hukutana wiki mbili kabla ya
Mkutano wa Bunge, ama Dar es Salaam, Dodoma au Zanzibar kuendana na
matakwa ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Aprili 2013.
Hivyo,
Wabunge wote wanapaswa kuwa wamewasili jijini Dar es Salaam ifikapo
Jumapili tarehe 27 Aprili 2014 tayari kwa kuanza vikao siku ya Jumatatu
tarehe 28 Aprili, 2014.
2.0 SHUGHULI ZITAKAZOTEKELEZWA
Wakati wa vikao vya Kamati, zitatekelezwa kazi zifuatazo:-
2.1
Siku ya Jumatatu na Jumanne Tarehe 28 na 29 Aprili, 2014 Kamati zote za
sekta pamoja na majukumu mengine, zitapitia masuala yote yaliyojitokeza
wakati wa ukaguzi wa miradi mbalimbali ya Maendeleo
2.2
Siku ya Jumatano tarehe 30 Aprili, 2014 Wabunge wote kwa ujumla wao
watakutana katika Ukumbi wa Julius Kambarage Nyerere kupokea Mapendekezo
ya Mpango, Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali ya 2014/2015 kwa
mujibu ya matakwa ya Kanuni ya 97 ya kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la
2013. Baada ya shughuli hiyo, Kamati zote za Kisekta zitaendelea na
uchambuzi wa Bajeti kuanzia tarehe 1 hadi 4 Mei, 2014
2.3
Kamati zisizo za kisekta zikiwemo Kamati ya Bajeti, Kamati ya
Masuala ya UKIMWI, Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya
Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) zitaendelea na utekelezaji wa
Majukumu yake kama yalivyoainishwa katika Kanuni za Kudumu za Bunge
Toleo la 2013.
2.4
Tofauti na kamati nyingine, Kamati ya Serikali za Mitaa na Kamati
ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) zitaanza kazi zake mapema ambapo
zitatakiwa kuwasili Dar es Salaam tarehe 25 April na kuanza kazi zake
tarehe 26 Aprili, 2014
3.0 SHUGHULI NYINGINE
Shughuli
za Kamati zitamalizika tarehe 4 Mei, 2014 Jijini Dar es Salaam ambapo
Mkutano wa Bunge wa Bajeti utaanza tarehe 6 Mei, 2014 Mjini Dodoma na
unategemewa kumalizika tarehe 27 Juni, 2014.
Aidha,
Bunge linatarajiwa kupitisha Mapendekezo kwamba Bunge liwe likikutana
kuanzia saa Tatu Asubuhi hadi saa Saba Mchana kila siku na kisha
kuendelea Jioni saa Kumi hadi saa Mbili Usiku ikiwa ni pamoja na Siku za
Jumamosi.
Hata
hivyo, siku ya Ijumaa Bunge litakutana kuanzia saa Tatu asubuhi hadi saa
Sita Mchana na kuendelea saa kumi Jioni hadi saa Mbili Usiku. Utaratibu
huu ukiafikiwa utawezesha muda wa kujadili Bajeti kuongezeka zaidi
licha ya siku kupungua
Ratiba za shughuli za Kamati zote zitapatikana kwenye tovuti ya Bunge ambayo ni www.parliament.go.tz
Imetolewa na:
Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa,
Ofisi ya Bunge
DODOMA
No comments:
Post a Comment