Jaji Joseph Warioba
Dodoma. Wabunge wa
CCM wameendelea kuirarua Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa bungeni na
Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph
Warioba.
Wabunge hao ni Diana Chilolo na Dk
Haji Mponda ambao kwa nyakati tofauti walisema mjadala usingefika hapa
kama sio mawazo binafsi ya Warioba.
Chilolo alimtuhumu Warioba kuwa aliingiza mawazo yake na kuacha walichochangia wananchi.
"Unaweza kuona hata mawazo ya wananchi
wangu wa Singida hayakuingizwa kwenye Rasimu, lakini leo wanasema ni
mawazo ya Watanzania wote, hakuna kitu kama hicho, ni mawazo yake tu,"
alisema Chilolo, ambaye ni Mbunge wa Viti Maalumu.
Mjumbe huyo alisema kuwa mawazo
yaliyoingizwa katika Rasimu ya Pili ya Katiba kwa sehemu kubwa yameacha
mawazo ya wananchi na badala yake yameingizwa mawazo ya watu wengine
wenye utashi wao.
Kwa upande wake, Mbunge wa Ulanga
Magharibi, Dk. Haji Mponda alisema kinacholisumbua Bunge la Katiba ni
mawazo ya Warioba ambayo hayakuzingatia Utaifa na Uzalendo.
Dk. Mponda aliiponda Rasimu ya Katiba
kwamba imejaa mambo binafsi ambayo hayawezi kutekelezeka na kuyaacha
yale ambayo wengi walitarajia yangeibuka.
Tangu kuanza kwa mchakato wa
mabadiliko ya Katiba, CCM imekuwa ikitoa miongozo mbalimbali kwa
wanachama wake na kuwataka waitetee katika mijadala ya Bunge.
Baadhi ya miongozo hiyo ni Muundo wa Muungano kuwa wa serikali mbili na kura za wazi katika kupitisha uamuzi bungeni.
Katika kutetea misimamo hiyo, baadhi
ya wajumbe wa CCM wamekuwa wakipingana na Rasimu ya Pili iliyowasilishwa
bungeni na Jaji Warioba.
Hata hivyo, msimamo huo wa CCM umekuwa ukipingwa vikali na baadhi ya vyama vya upinzani.
No comments:
Post a Comment