Monday, August 18, 2014

MAREHEMU, WALIOACHA KAZI WALIPWA MISHAHARA

hawa-ghasia18_0d5c2.jpg
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi, Hawa Ghasia

UTARATIBU mpya wa Hazina kulipa mishahara moja kwa moja kwa watumishi wa halmashauri, umefichua ‘mchezo mchafu’ wa watumishi waliofariki na watoro kulipwa mishahara.
Akisoma risala ya washiriki mafunzo ya utekelezaji wa awamu ya pili ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES) mwishoni mwa wiki iliyopita, Mwenyekiti wa washiriki hao, Ramadhani Chomolla, alisema Serikali imepata hasara kupitia utaratibu huo.(Martha Magessa)

Aliitaka Serikali kuangalia upya mfumo wa Hazina wa kuwalipa moja kwa moja watumishi, ili kuepusha hasara hiyo ya kulipa mshahara watumishi waliofariki, watoro na walioacha kazi.
“Mshahara wa Julai (mwaka huu), Hazina imewalipa moja kwa moja watumishi, hivyo watoro na waliofariki nao wamepata mishahara, hii imeiingizia Serikali hasara na watoro wameanza kudharau wakuu wa vituo,” alisema Chomolla.

Hata hivyo, akijibu hoja hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia alisema hilo si kosa la Hazina, ila ni halmashauri zenyewe kwa kuwa zinawajibika kupeleka mahitaji ya mishahara na akaunti za watumishi.

“Kama mtumishi amefariki ndani ya mwezi ambao mshahara umelipwa sio tatizo, lakini kama amefariki siku nyingi na amelipwa, hii inaonesha kuwa fedha hizi zingefika kwenye halmashauri zingeliwa na wachache. “Naamini watu wa aina hii watakuwa wawili au watatu, ikiwa zaidi ya hapo basi halmashauri itakuwa na matatizo. Nadhani safari hii marehemu au walioacha kazi wamewazidi ujanja,” alisema.
Alisema hatua ya Serikali ya kulipa mishahara moja kwa moja, ilitokana na kuwapo kwa mabadiliko ya nyongeza za mishahara na kutaka watumishi walipwe mapema.
Akizungumzia mafunzo hayo, Ghasia aliwataka washiriki kuhakikisha changamoto zilizojitokeza kwenye awamu ya kwanza, hazijirudii katika utekelezaji wa awamu ya pili.
Alisema awamu ya kwanza ilikuwa na changamoto kadhaa, ikiwemo udhaifu katika usimamizi wa fedha, matumizi mabaya ya fedha za miradi na kuchelewa fedha za ruzuku za uendelezaji shule.
“Tumewapa mafunzo kwa pamoja watendaji mnaohusika katika utekelezaji wa mpango huu, hivyo hatutegemei changamoto za awamu ya kwanza kujirudia au kutokuwa na ufanisi katika kutekeleza miradi,” alisema.
Aidha, Ghasia alikemea tabia ya watendaji katika baadhi ya halmashauri kusingizia mfumo wa matumizi ya fedha kwa njia ya mtandao (EPICA), kuwa ndio chanzo cha kukwamisha utekelezaji wa miradi.
Washiriki 411 kutoka halmashauri na mikoa 16 walishiriki mafunzo yaliyotolewa na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM).
Mikoa hiyo ni Ruvuma, Simiyu, Singida, Mtwara, Lindi, Tanga, Shinyanga, Geita, Morogoro, Arusha, Manyara, Iringa, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Dodoma na Pwani

No comments: